Tuesday, May 12, 2020

Namuona Mbowe kama Julius Caesar akisalitiwa na Brutus

Tumesikia kuhusu wabunge wa upinzani waliokaidi msimamo wa chama chao kukaa karantini kutokana na maradhi ya corona yanayoisumbua dunia kwa sasa.
Wabunge hao kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joseph Selasini (Rombo), Peter Lijualikali (Kilombero), David Silinde (Momba), Anthony Komu (Moshi Vijijini), Jafary Michael (Moshi Mjini), na Wilfred Lwakatare (Bukoba).
Wengine ni Susan Masele, Latifa Chande, Subrina Sungura, Joyce Sokombi na Mariam Msabaha. Wabunge hawa walikataa kata kata msimamo wa chama chao kutokuendelea na vikao vya bunge kwa agizo kutoka kwa mwenyekiti wao Freeman Mbowe.
Pia tukamsikia Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Esther Bulaya akisisitiza kuwa wabunge waliokaidi msimamo wa chama chao wametakiwa kuachia ngazi walizokuwa nazo katika chama hicho kikuu cha pinzani nchini.
Silinde ni miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kujibu kauli ya Bulaya, “Nimemsikia Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akisema wametutaka wote tuliokiuka makubaliano ya chama tujiuzulu nyadhifa zetu, mimi nimeshafanya hivyo na ninaamini tulipaswa kupambana na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi na si kukimbia,”alisema mbunge huyo.
Kabla sijasonga sana mbele nikupe kisa kimoja cha kweli kilichotokea baina ya mtawala wa Rumi Julius Caesar na kijana wake aliyemkuza akafikia ngazi za juu katika utawala aliyefahamika kwa jina la Marcus Brutus.
Caesar ambaye lake kamili ni Gaius Julius Caesar (100-44 KK). Huyu ndiye yule aliyepambana kwa udi na uvumba kuizamisha Jamhuri ya Rumi hadi kuunda Dola ya Rumi. Alifariki dunia akiwa na miaka 55.
Mauaji ilikuwa ndio hatima ya viongozi wengi wa Kirumi. Siku ya kifo chake Caesar alikuwa na mazungumzo na baraza lake la seneti.
Kuna mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mark Anthony alijua nini kitakachokwenda kutokea kwa kiongozi wake.
Aliyafahamu hayo kupitia kamanda wa kijeshi wa karibu kabisa na Caesar aliyefahamika kwa jina la Servillus Casca kutokana na hofu yake ya kutaka kutoonekana mbele ya uso wa Caesar.
Waratibu wa tukio hilo la mauaji walikuwa wakihofia kuwa huenda Anthony angetoa msaada wa kumwokoa Caesar.
Kamanda mwaminifu kwa Caesar aliyefahamika kwa jina la Trebonius ambaye kabla kifo cha Caesar, mnamo mwaka 45 aliteuliwa kuwa gavana cheo cha juu kabisa ndiye aliyejitokeza kumzuia Caesar asifike katika ukumbi wa Pompey ambako mazungumzo hayo yangefanyika.
Aidha vyanzo vingine vinasema Anthony alicheleweshwa na Decimus  Albinus (binamu wa mbali wa Marcus Brutus) ili asiwahi kufika ukumbi.
Huyu Albinus ambaye naye alikuwa kamanda wa jeshi la Dola la Rumi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 38 mwaka mmoja baada ya mauaji ya Caesar.
Anthony alisikia kelele katika ukumbi wa Pompey ambapo alihisi sio dalili nzuri ilimbidi akimbie kwa alijua tayari mambo yameshaharibika.
Julius Caesar alichomwa na vitu vyenye ncha kali hadi umauti unamkuta. Kundi la watu wanaokadiriwa kufikia 60 lilifanya kitendo hicho Machi 15, 44 KK.
Mauaji hayo yanaelezwa kuwa yalikuwa mabaya kuwahi kutokea. Miongoni mwa wauaji alikuwa ni Brutus, mtu ambaye alilelewa na kufikia kushika madaraka makubwa yaliyomfanya atambulike na watu wa Dola la Rumi.
Ulikuwa ni usaliti mkubwa. Mwanamashairi William Shakespeare aliandika katika mojawapo ya kazi zake kuwa usaliti huo ulikuwa mwisho wa Caesar kuendelea kuipambania Dola la Rumi utakumbuka kwamba Caesar alipambana miaka tisa ili kupata kulikamata kabila la Gaul ambalo lilikuwa na upinzani mkali kwa Caesar.
Mtu mmoja anayeitwa Plutarch (46-119 BK) mwanafalsafa wa Ugiriki aliwahi kuandika kuwa Caesar alipomwona Brutus alivuta vazi lake mithili ya blanketi maarufu sana enzi za dola la Rumi ya zamani kwa jina la ‘toga’ na kujifunika kichwani ili asimwone rafiki yake akiwa miongoni mwa wauaji wake.
Mwanahistoria wa Rumi Suetonius (69-122 BK) aliyakaririwa maneno ya mwisho ya Caesar kwa Brutus kabla ya kuuawa kwake, “Na wewe mwanangu?”
Hata hivyo Brutus hakuchukua muda mrefu alijiua miaka miwili baadaye baada ya kushindwa katika vita vya Ufilipi hivyo kuhitimisha mapambano yake ya kuwania madaraka baada ya kifo cha Caesar.
William Shakespeare katika tamthilia yake mwaka 1559 ikimuhusu Caesar alisema “ Waoga hufa mara nyingi kabla ya vifo vyao.” Ikiwa na maana kuwa “Mtu mwoga hufa vifo elfu, shujaa hufa kifo kimoja tu.”
Kilichofanywa na wabunge wa upinzani kukaidi amri ya mwenyekiti ni sawa na kusema wameamua kumsaliti Mbowe kama makamanda wa jeshi la Caesar ambao waliratibu kumuua kiongozi wao.
Hakuna mtu atakayebisha kuwa ninyi wabunge mliokaidi mliketi chini na kupanga namna ya kumsaliti Mbowe na mmefanikiwa. Wengi mlipambaniwa kweli kweli kufika hapo mlipo kama Brutus alivyopambaniwa na Caesar lakini hatimaye mshahara wake ni kumsaliti Mbowe.
Nafikiri Mbowe akiwatazama katika taswira yake ya ubongo anajiuliza, “Na wewe Silinde?….na wewe Lijualikali?…..na wewe Jafary Michael?...”
Kilichokuja kuwakuta majemadari wasaliti wa Brutus ni kwamba waliokuwa upande wa Caesar hawakukubali waliamua kuwatafuta kwa udi na uvumba na kuwamaliza, hivyo natarajia kuona mwisho wenu mliokaidi msimamo wa chama chenu ukifika na ndio sababu walianza kuwaambia muachie ngazi mlizokuwa nazo.
Wengine hapo hamjapigwa hata na risasi kama Tundu Lissu lakini mnasema eti mnawapigania wananchi. Hamjaguswa kama Mbowe alivyoguswa katika maisha yake ya siasa mnamsaliti, ni heri mngeratibu kumuua kabisa Mbowe ili mfaidi matakwa yenu ya mioyo yenu lakini sio kujificha katika kivuli za kusaidia wananchi.
Mnajua fika kuwa corona imeathiri pakubwa dunia kwa sasa mnamsaidia vipi mwananchi leo kwani miaka mitano ya kukaa bungeni mlikuwa wapi, mbona viongozi wa serikali walikuwapo siku zote? Huo ni usaliti kama Brutus alivyofanya.
Enzi za uhai wake Caesar aliwahi kusema “Ni rahisi sana kutafuta watu watakaojitolea kufa, kuliko kutafuta watu ambayo wako tayari kustahimili maumivu kwa uvumilivu.”
Mbowe nafikiri kwa miaka mingi umekuwa ikitafuta watu watakoweza kustahimili maumivu lakini wengi wao wamekuwa wakikukimbia kwasababu hawawezi kustahimili maumivu kwa uvumilivu wa kukatwa posho hivyo wanaona bora wakusaliti.
Pia ninaamini na ndivyo ilivyo waliokaidi msimamo huo katika kipindi kijacho hawatakuwa upande wa Chadema kama Brutus alivyofanya kwani alipofanya mauaji dhidi ya bosi wake alijiunga na Pompey Magnus, kinachosubiriwa ni ninyi kuwaona mkienda katika vyama vingine na sio Chadema tena.
Caesar hayupo ulimwenguni kwa karne nyingi lakini tunayaishi mazuri yake ambayo yanaweza kuwa funzo kwa wanasiasa wanaochipukia hapa nchini kuwa wanapaswa wajifunze mengi kwa watawala waliopita ili wajue kuwa wao sio wa kwanza kufanya hivyo.
Imetayarishwa na Jabir Johnson, kwa maoni au ushauri +255 768 096 793 au baruapepe: jabirjohnson2020@gmail.com

0 Comments:

Post a Comment