IMEELEZWA uwepo wa
umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa wakazi wengi mkoani Kilimanjaro
umeokoa ukataji wa miti kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na kabla ya nishati
hiyo kutua katika maeneo hayo.
Akizungumza katika
zoezi la upandaji miti 250 katika mtaa wa wa Shauri Moyo katika kata ya Majengo,
mjini Moshi Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kibo Enviroment
Conservation Group Daniel Mvungi alisema wakala wa umeme vijijini umekuwa
sehemu ya kuzuia ukataji wa miti na matumizi makubwa ya kuni na mkaa kwa wakazi
wengi wa vijijini hali ambayo imekuwa ikitoa ahueni kwa maeneo ya miji.
“Jadi ya mwafrika
hususani mtanzania ni kutumia kuni na mkaa lakini nyakati zinabadilika kutokana
na ongezeko la watu na mahitaji yao, sasa ujio wa REA umesaidia kupunguza matumizi
hayo kwa sasa mwananchi anaweza kutumia vifaa baadhi vya umeme ambapo zamani
isingewezekana,” alisema Mvungi.
Aidha Mvungi alisema
Umeme wa REA umekuwa sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati bora katika
shughuli za uzalishaji, kilimo, viwanda vidogo vidogo na vya kati, na biashara
ili kukuza uchumi vijijini.
“Umeme wa REA umewezesha
upatikanaji na matumizi ya nishati bora kwa ajili ya huduma za kijamii vijijini
kama vile afya, elimu, maji na mawasiliano,” alisema Mvungi.
Aidha Mvungi
aliongeza kuwa uwepo wa nishati bora kama gesi umekuwa mbadala wa matumizi ya
kuni na mkaa hali ambayo imesaidia hata mijini kusiwepo ongezeko kubwa la mkaa
ukilinganisha na miaka ya nyuma hali ambayo imepunguza uchafu wa hewa katika
maeneo ya mijini.
“Serikali imefanya
jambo la msingi kusambaza gesi hadi maeneo ya vijijini jambo ambalo limesaidia
kupunguza ukataji wa miti,na uchafuzi wa hewa,” alisema Mvungi.
Mwenyekiti wa Mtaa
wa Shauri Moyo Omar Danga alisema kwa sasa elimu kuhusu mazingira inazidi
kupenya katika vichwa vya wakazi wengi wa mijini na vijijini na kuongeza kwamba
hiyo inatokana na juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali wa mazingira
kuelimisha watu kuhusu faida za uwepo wa miti katika maisha ya kila siku.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana wa Utetezi na Uwajibikaji Ansila Malawiti
alisema mpaka sasa katika kikundi chao chenye vijana wapatao 20 wamekuwa
wakijishughulisha na upandaji wa miti na utoaji wa elimu ya mazingira katika
mitaa mbalimbali mjini Moshi ambapo mita zaidi ya miti 6,000 imepandwa katika
kipindi cha miezi 12 iliyopita.
0 Comments:
Post a Comment