Dunia bado ipo
katika kitendawili cha kutafuta chanjo ya maradhi ya Covid-19. Walimwengu bado
wana hofu kuhusu hali ya mambo kila mmoja kwa taifa lake. Wengine wanahofia
nafasi zao katika siasa, uchumi na afya zao. Kwa kifupi kila mmoja yupo chini
akitafakari hatma ya ugonjwa huu wa corona kwa sasa.
Hata hivyo kuna
kundi ambalo halizungumzwi sana katika mapambano haya licha ya umuhimu wao.
Kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakijitahidi kusisitiza ulazima wa kutunza
mazingira kwa afya ya mwanadamu lakini wengine wameuawa kutokana na juhudi zao.
Kundi hilo ni Watetezi wa Mazingira.
Mauaji yanaendelea
kwa watetezi hawa wa mazingira utakumbuka huko Latin Amerika mwaka huu wameuawa
watetezi wa mazingira Isaac Hererra, Adan Vez Lira na Zezico Rodrigues kutokana
na harakati zao za kutetea mazingira. Kinachoonekana ni maslahi binafsi ya baadhi
ya watu kuhusu malighafi zinazopatikana katika mazingira.
Wanasayansi
wamethibitisha kuwa magonjwa na maambukizi mbalimbali yanayotokea katika maisha
ya binadamu yanatokana na uharibifu wa mazingira.
Kuna upande
mwingine ambao unasema mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanatokana na mwanadamu
huyu kumkosea Muumba wake hao siwapingi wana hoja zao kwa upande mmoja.
Tujikite katika
utetezi wa mazingira. Wasomi na wataalamu mbalimbali wanasema magonjwa mengi yanayomkumba
binadamu yametoka kwa viumbe vidogo na vikubwa, kwa hivyo, mabadiliko katika
makazi ya watu hawa yanaweza kuathiri mtindo wa maisha na tabia zao.
Kuongezeka kwa
uharibifu unaoendelea wa mazingira ndiko ongezeko la uwezekano wa magonjwa
yanayosababishwa na viumbe hivi.
Wote tunajua kuwa
majanga yaliyoikumba dunia miaka ya nyuma kutokana na kubadilika kwa hali ya
joto, mvua na unyevunyevu kulisababisha uwepo wa maradhi ya kuambukiza.
Kwa mfano mwaka
1878 kusini mwa Marekani kuliibuka maradhi ya homa ya manjano yaliyokuwa
yakisambaa kupitia mbu aina ya Aedes aegypti.
Watu zaidi ya
100,000 walipatwa na maradhi hayo huku 20,000 wakipoteza maisha yao. Pia uchumi
wa taifa hilo ulishuka kutokana na hali ya dharura ya kuokoa uhai wa watu hao.
Miji iliyokuwepo katika Bonde la Mto Mississippi katika karne ya 18 na 19
ilipatwa na athari hizo.
Mabadiliko ya hali
ya hewa kati ya mwaka 1793 na 1905 yalisababisha kuibuka mara tisa maradhi hayo
yakifuatiwa na mvua kali za El Niño zilizoikumba Marekani mara saba katika
kipindi hicho.
Taasisi ya Utafiti
ya nchini Marekani katika gazeti lake Bulletin of the American Meteorological
Society mnamo mwaka 1999 ilichapisha kuwa mbu aina ya Aedes aegypti ndiye
msambazaji mkuu wa maradhi ya homa ya manjano.
Watalaamu wanasema
mabadiliko ya hali hewa ikiwamo mvua na joto yamekuwa yakiathiri chakula
ambacho wanyama kama Popo, Nyani, Pangolin na kulungu huishi kwa hicho hivyo
mabadiliko hayo yamekuwa yakisababisha kubadilika kwa maumbo yao na idadi yao
kuwa kubwa hali ambayo imekuwa ikifanya ukaribu wao kwa binadamu kuongezeka na
vijidudu hao kuingia katika mfumo wa binadamu.
Mwishoni mwa mwaka
1999 na mwanzoni mwaka 2000 wanasayansi wa Los Santos huko Panama walitambua
kwa mara ya kwanza katika Amerika ya Kati dalili za maradhi ya HPS (Hantavirus
pulmonary syndrome) ambayo hushambulia mfumo wa kupumua.
Watalaamu hao
walikuta virusi vikiwa kwenye mate, mkojo na vinyesi vya panya. Lakini mvua
zilizoikumba Los Santos mwezi Septemba na Oktoba 1999 ziliwafanya panya wale
wahame kutoka makazi yao na kutafuta makazi mengine hivyo wanadamu waliathiriwa
na ujio wa panya hao.
Mvua zinapokuwa
kubwa zisizomithirika husababisha ukuaji mkubwa wa virusi ambao huathiri
mamilioni ya watu kutokana na kwamba binadamu anaweza kuvisafirisha virusi (enterovirus)
hao kupitia mfumo wake wa chakula.
Pia uchunguzi
umefanyika kuwa ongezeko la watu na uhamaji wa makazi hayo kwa wanyama na
binadamu katika karne hii umeongoza kwa kiasi kikubwa kusambaa kwa virusi
wanaoshambulia mfumo wa upumuaji.
Hivyo udhibiti wa
mazingira unaweza kuokoa hatari ya virusi hao kusambaa kutoka wanyama kwenda
kwa binadamu.
Uchafuzi wa hali
ya hewa unaotokana na viwanda umekuwa chanzo cha mabadiliko ya hali ya hewa
hali inayoongeza kusambaa kwa virusi hao kutoka kwa wanyama kwenda kwa
binadamu kutokana na mabadiliko tabianchi.
Kazi nyingine za
binadamu kama ufugaji wa makundi makubwa ya wanyama umekuwa chanzo cha kuharibu
mazingira hali ambayo imekuwa ikisababisha ukame au mvua zisizotarajiwa.
Mamlaka za hali ya
hewa zimekuwa zikijitahidi kutoa taarifa kuhusu mabadiliko hayo hali ambayo
ukichunguza kwa makini utagundua kuwa imesababishwa kwa asilimia kubwa na kazi
za binadamu mwenyewe.
Watetezi wa
Mazingira ni walezi wazuri kuliko serikali peke yake, jeshi au polisi kwani
wanakuwa na muda mzuri wa kuielemisha jamii faida za utunzaji wa mazingira.
Hata hili la
Covid-19 ni mwendelezo wa muundo wa maisha ya binadamu mwenyewe unaofanya
wanyama kama popo kuhamia karibu na mazingira ambayo binadamu anaishi.
China na Marekani
ni miongoni mwa mataifa ambayo yameendelea kiviwanda hivyo hata uharibifu wa
mazingira umekuwa mkubwa huku watetezi wa mazingira wakipewa nafasi ndogo ya
kuelimisha umma.
Aidha utumiaji wa
kemikali za kupulizia kuua virusi hivyo bado tena ni janga kwani kemikali hizo
zitahamia kwenye udongo, maji na mfumo mzima wa maisha wanyama na binadamu
utaathiriwa. Utunzaji wa mazingira ndiyo utaiponya dunia dhidi ya maradhi ya
mlipuko.
0 Comments:
Post a Comment