Aprili 29, 2020 alifariki dunia Mwanaharakati wa
Kupinga Ubaguzi wa Rangi nchini Afrika Kusini Denis Goldberg. Alifariki dunia
akiwa na umri wa miaka 87 nyumbani kwake Hout Bay, Cape Town.
Goldberg alikuwa miongoni mwa watu wawili waliokuwa
wamebaki baada ya harakati za kupinga ubaguzi wa rangi (Apartheid) nchini
Afrika mnamo mwaka 1963-1964. Goldberg alikuwa na Nelson Mandela aliyefariki
akiwa na umri wa miaka 95 mwaka 2013, Walter Sisulu (1912-2003) na Ahmed
Kathrada (1929-2017) ambao nao walishafariki dunia.
Aliyebaki kwa sasa baada ya waliokuwepo wakati wa
harakati hizo ni Andrew Mokete Mlangeni.
Goldberg alifariki dunia kwa kansa ya mapafu na
kutangazwa na serikali ya Afrika Kusini huku Rais Cyril Ramaphosa akitoa salamu
za rambirambi na kusema aliyatoa maisha yake kwa ajili ya watu.
Tuangazie maisha yake Golberg; Sheria zilizopasishwa
na wazungu katika kipindi hicho ziliwatambua watu weupe kuwa ni raia wa daraja
la juu ambao walipaswa kupewa haki na fursa zote za kijamii, kisaisa, kiuchumi,
kielimu na kiutamaduni.
Suala hili lilijenga ukuta na mtengano katika jamii ya
Afrika Kusini ambayo katika upande mmoja ilikuwa na wazungu na watu weupe, na
upande wa pili kuliwepo wazalendo weusi. Kila kitu kilitofautiana baina ya
pande hizo mbili.
Vyuo na shule za watu weupe zilitenganishwa na zile za
watu weusi. Goldberg alikuwa mzungu mweupe ambaye aliyepinga utengano huo hatua
iliyofanya atupwe jela la Pretoria Central.
Hata jela zilikuwapo za weupe na weusi ambapo
alikotupwa Goldberg ilikuwa maalumu kwa washtakiwa wa kizungu. Jela la Robben
Island ilikuwa kwa ajili ya weusi kama Nelson Mandela
Goldberg alianza kutafutwa mwanzoni mwa mwaka 1963
hatimaye Julai 11, 1963 polisi walivamia makazi ya wanaharakati wa African
National Congress huko Rivonia kitongoji kilichokuwapo Kaskazini Mashariki mwa
Johannesburg katika mkutano ambao wanaharakati hao walipanga kukutana huko.
Nyumba hiyo ya Liliesleaf ilikuwa inatumiwa na
wanaharakati hao kwa siri takribani miaka miwili. Goldberg alikamatwa na
wenzake katika shamba hilo Walter Sisulu, Govan Mbeki, Raymond Mhlaba na Rusty
Bernstein.
Baada ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria
ilibainika kuwa wakati kina Goldberg wakikamatwa Mandela alikuwa tayari yupo
jela na walibaini kuwa alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakifanya kazi kupitia
vielelezo mbalimbali walivyovikuta huko Liliesleaf hivyo ikabidi wamwongeze
kwenye kesi hiyo iliyopewa jina la Rivonia Trial.
Siku moja baada ya kukutwa na hatia Goldberg alikutana
na wanasheria wake Bram Fischer, Joel Joffe, Arthur Chaskalson na George Bizos
ambao walimwambia kwamba mashtaka ambayo alikuwa akikabiliwa nayo yalikuwa ni
magumu ambayo asingeweza kukwepa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Nelson Mandela na Denis Goldberg |
Goldberg aliazimia moyoni mwake kumlinda Mandela na
viongozi wengine hivyo akaamua kuchukua wajibu huo kujibu mashtaka ya
utengenezaji wa silaha na kwamba mpango huo uliandikwa na yeye na hawezi
kukataa. Ilipangwa Goldberg atoroshwe lakini ilishindikana.
Goldberg alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa tawi la
kijeshi la ‘uMkhoto we Sizwe’ ndani ya ANC.
Hata hivyo madai ya kuwapo jela haikuwa mara ya kwanza
kwa Goldberg kwani mnamo mwaka 1957 alijiunga na chama cha Kikomunisti
kilichokuwa kimefutwa mwaka 1950.
Mnamo Machi 30, 1960 alikamatwa na makaburu kwa kuunga
mkono migomo katika miji kadhaa nchini humo baada ya Mauaji ya Sharpville
yaliyotokea mnamo mwaka 21, 1960.
Akiwa na mama yake waliswekwa jela kwa miezi minne
bila kupanda kizimbani. Hatua hiyo ilimfanya apoteze kazi yake ya uhandisi
akiwa na Kampuni ya Athlone Power Station.
Wakati alipopandishwa kizimbani Juni 12, 1964 alikuwa
na miaka 31 ambapo alikuwa ni umri mdogo kuliko wengine katika kesi hiyo na
alikuwa pekee mtu mweupe (White Man). Wakati anahukumiwa mama yake alikuwapo
siku hiyo, inaelezwa kuwa hakumsikia Jaji wakati akitoa hukumu kwa ajili ya
Goldberg kwenda jela akamuuliza kwa sauti, “Denis, nini? Jaji amesema nini?”
Goldberg alimjibu, “ Maisha, na maisha ni ya Kustajaabisha.”
Mnamo Machi 1950 akiwa na miaka 16 alianza masomo yake
ya Uhandisi (Civil Engineering) katika Chuo Kikuu cha Cape Town.
Akiwa hapo ndipo alipokutana na mwanadada
mwanaharakati wa Kikomunisti Esme Bodenstein na alimwoa mnamo Januari 1954.
Walizaa mtoto anayeitwa Hillary (1955) na David (1957).
Hatimaye baada ya mapambano marefu mfumo usio wa
kibinadamu wa Apartheid huko Afrika Kusini ulifikia kikomo mwaka 1991 na mnamo
Mei 11, 1994 Mandela alikuwa Rais wa kwanza mweusi kuongoza taifa hilo.
Mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid ni miongoni mwa
sura za ukatilii na unyama wa kutisha na ubaguzi wa kizazi uliotawala Afrika
Kusini kwa miaka mingi kwa maslahi ya wazungu walio wachache dhidi ya wazalendo
weusi.
Kwa dunia yetu ya sasa vita imekuwa ikipiganwa ndani
na nje ya nchi husika. Kila taifa kwa sasa linahaha kutafuta namna
litakavyoponya uchumi wake kutokana na janga la Corona.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe
Magufuli naye kwa staili yake anaokoa uchumi wa taifa lake kwa staili yake
ambayo huenda haiwapendezi watu, hata hivyo nakubaliana naye kuwa mtazamo wa
Kimagharibi umekuwa haupati nafasi kwake huenda aliwahi kumsoma Walter Rodney,
namna Wazungu walivyoinyonya Afrika na kuifanya ishindwe kuendelea. Huenda
ndiyo sababu ameenda kwa Andry Rajoelina kusaka suluhu baada ya mwenzake
kugundua dawa ya kuzuia corona.
Pia JPM huenda alifuatilia kwa karibu kauli za msomi
wa masuala ya jamii wa Uingereza Herbert Spencer ambaye aliwahi kusema mtu
mwenye rangi nyeusi hana uwezo wa kufikiria katika daraja la juu zaidi ya
kutumia hisia na muonekane.
Huenda watanzania hawaoni nia ya ndani ya JPM katika
hilo kama ambavyo Wafaransa walishindwa kuiona nia ya ndani ya Gustave Eiffel
aliyetengeneza Mnara wa Eiffel uliopo pale Champs de Mars jijini Paris na kwa
miaka mingi imekuwa nembo ya Ufaransa. Vilevile Wajerumani waliposhindwa kuiona
nia ya ndani ya Otto von Bismarck ya kuifanya Ujerumani izungumzike Ulaya yote.
Goldberg umeondoka lakini mwambie Mandela bado
tunaendelea kupambana na wasaliti wanaosaliti mambo ambayo yanaweza kuifanya
Afrika yetu ikawa katika mwonekano ambao utakuwa wa sisi wenyewe. Mlipambana
kuondoa mfumo uliokuwa ukiwatenganisha watu wa rangi na mbari mahsusi,
kuwalazimisha kuishi maeneo mahsusi na kuwanyima haki zao zote za kisiasa,
kijamii na kibinadamu.
Lakini kwa sasa nafikiri kwa sehemu utakuwa uliona
enzi za uhai wako namna viongozi wa siasa hapa Afrika wanavyoendelea kusaliti
maono yenu ya kuiweka Afrika na watu wake katika usawa. Kumekuwa na wasakatonge
tu kwa kizazi chetu wanaojificha kwa kivuli cha kusaidia wananchi hatimaye
wanawasaliti.
Hawako tayari kuvumilia mateso ya maumivu kama
ulivyofanya wewe Goldberg na wenzako. Ulikubali kuachishwa kazi ili uwatetee
weusi waliokuwa wakibaguliwa licha ya kwamba ulikuwa mweupe. Hakika tunakushukuru
kwa jitihada zako licha ya kwamba hufahamiki na katika ardhi yangu ya Tanzania.
Nina mengi ya kunena juu ya hili lakini niseme tu,
“Kwaheri Denis Goldberg msalimie Nelson Mandela mwambie Tunapambana na Corona
na Wasaliti.”
Ahmed Kathrada, Walter Sisulu, Nelson Mandela na Denis Goldsberg enzi za uhai wao. |
0 Comments:
Post a Comment