Sunday, May 3, 2020

Mabadiliko ya sheria ya viboko yarudisha kicheko shingo upande Saudia Arabia


Licha ya mapambano dhidi ya virusi vya Covid-19 lakini maisha yanaendelea kama kawaida kutokana na kwamba ulimwengu unaendeshwa kwa sheria za asili tangu kuwekwa kwake.

Hivyo wakati taarifa mbalimbali zikiendelea kutawala vichwa vya habari duniani kuhusu corona nchini Saudia Arabia mwezi Aprili mwaka huu imeonyesha njia katika jambo ambalo halikudhaniwa kama lingeweza kupata suluhisho katika ardhi hiyo.

Jambo hilo ni kuondolewa kwa adhabu ya viboko kwa washtakiwa kwenye baadhi ya makosa nchini humo.  Utawala wa Mfalme Salman na mwanamfalme Mohammed bin Salman umefikia mwafaka wa kuondoa adhabu hiyo mwanzoni mwa mwezi Aprili.

Hatua hiyo inazifanya mahakama za nchini humo kutoa adhabu ya kutupwa jela, faini au vyote kwa pamoja. Awali ilikuwa kuwa majaji walikuwa wanazitafsiri sheria za kidini ‘Sharia’ au sheria za Kiislamu kisha kuweka uamuzi wao.

Miongoni mwa makosa yaliyokuwa yakihusisha adhabu ya viboko ni pamoja na kutoka nje ya ndoa na ugomvi. Tukio hilo limepokelewa vizuri kiasi na mashirika ya haki za binadamu kama Human Rights Watch na Amnesty International kuwa jambo hilo lilipaswa kufanyika muda mrefu.

Mahakama za juu nchini Saudi Arabia zinasema kufanya hivyo ni kurudisha ufalme huo katika kujali haki za binadamu. Hata hivyo huenda ufalme huo umefanya kwa shinikizo kutokana na hali ilivyo kwa sasa ukilaumiwa kwa kuminya uhuru wa wananchi wake tangu mwaka 2017 wakati ambao Mfalme Salman alipomteua mwana mfalme Mohammed.

Kwanini wachambuzi wa masuala ya Kimataifa kuhusu siasa za Saudia wanaona Mfalme Salman amefanya hivyo kutokana na shinikizo la kimataifa? 

Sababu kubwa ni mauaji ya mwanahabari Jamal Kashoggi mwaka 2018 ambaye utawala huo unanyoshewa kidole cha lawama licha ya kupinga madai ya mauaji ya mpinzani wao ambaye aliuawa ndani ya Ubalozi wa Saudia Arabia jijini Istanbul huko Uturuki.

Pia uondoaji wa viboko hivyo unakuja wakati ambao mwanaharakati Abdullah al-Hamid (69) kufariki dunia kwa kuchapwa viboko hivyo. 

Mwanaharakati huyo ambaye alikuwa mwanzilishi wa Chama cha Kutetea Haki za Raia na Haki za Siasa (Acpra) alihukumiwa kwenda jela miaka 11 mnamo Machi 2013 na adhabu ya viboko. Mwanaharakati huyo sio wa kwanza kutupwa jela na kuhukumiwa adhabu ya viboko.

Mnamo mwaka 2014, mchapishaji wa maudhui mtandaoni (Blogger) Raif Badawi alihukumiwa kwenda jela miaka 10 na viboko 1,000 kwa kuutukana Uislamu katika mojawapo ya machapisho yake mtandaoni. Badawi alitunukiwa tuzo na bunge la Ulaya mwaka 2015 katika harakati zake za kutetea haki za binadamu kwa kupokea tuzo ya Sakharov.

Jambo la msingi ambalo tunaweza kujifunza katika hatua zinazochukuliwa na Saudi Arabia mojawapo ya ngome imara ya Uislamu duniani ni kwamba hakuna kilicho na mwanzo kinachokosa mwisho.

Saudia ilionekana ni ardhi ambayo ingekuwa ngumu kuingia katika mfumo wa kisiasa na kuachana na taratibu zake za kiimla kwa miaka mingi lakini kinachoonekana kwa sasa tayari watu wa ardhi ile wameona kuna haja ya kuingia katika mfumo wa dunia wa kisiasa ambao bila ya kuwa na huo huwezi kutoboa.

Hapo ndipo ninapomkumbuka Thomas Hobbes aliposema kupitia kile alichokiita ‘Social Contract’ ikiwa na maana kwamba kunapaswa kuwepo na makubaliano baina ya wananchi na watawala inapokosekana huwa ni vurugu.

Hata hivyo Hobbes ni mwanafalsafa na mwananadharia wa Kiingereza aliyeishi miaka ya 1588-1679. Pamoja na kuwa aling’ara sana katika nyuga za siasa na falsafa, mtaalamu huyu pia alifanya maelezo ya kisayansi aliyoyatoa kuhusu vipengele vya ufutuhi.

Maelezo yake kuhusu sababu za kutokea kwa kicheko na ucheshi yalionekana kuwa na mashiko kuliko maelezo ya awali.

Kwa jumla, nadharia hii inadai kuwa mtu hucheka kwasababu ya kujiona kuwa yuko katika hadhi ya juu; na kwamba, wakati huo mtu hujikweza na kujiweka huru zaidi akiwa amejitenga na hali yoyote ya uduni. Kutokana na msingi huo, nadharia hii hujulikana pia kama ‘Nadharia ya Ugandamizaji.’

Kucheka hapa kunanasibishwa moja kwa moja na kutosheka au kuridhika kwa nafsi ambako, aghalabu, huzaa furaha. Yaani, mtu anapocheka, hutawaliwa na raha ya aina fulani na kujiona yuko katika tabaka la pekee hata kama anazungukwa na matatizo. Punde atokapo nje ya muktadha wa kicheko chake ndipo huweza kurudi katika kuyawazia matatizo yake.

Kwa muda mrefu watu wa Saudia Arabia walikuwa wakionekana kuwa na furaha lakini hali haikuwa hivyo kwani inapomalizika walikuwa wakirudia katika hali zao za kuyawazia ukomo wa matatizo yao.

Utakumbuka wakati wanawake waliporuhusiwa kuendesha magari katika ardhi hiyo hakika kicheko kilitandaa kwa wanawake wa huko. 

Ni matumaini yangu kwamba licha ya uamuzi wa shingo upande kwa Mfalme Salman na mwanamfalme Mohammed lakini imeleta ahueni kwa wana Saudia Arabia hali ambayo itaongeza shinikizo la kufanya marekebisho mengine katika sheria kandamizi kwa watu wa taifa hilo.



0 Comments:

Post a Comment