Wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kuipa uzito jinsia ya kike katika maeneo ya kazi ikiwa ni kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 la kutokomeza ukatili na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika umiliki wa rasilimali na nyanja zote za kimaisha.
Akizungumza katika semina ya siku moja ya kuwaweza wanahabari mkoani Kilimanjaro Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bahati Nyakiraria alisema taarifa zinazohusu jinsia ya kike zimekuwa zikitolewa kwa kasi ndogo huku sababu mbalimbali zikianishwa.
“Taarifa kuhusu mwanamke zimekuwa zikitolewa kwa kasi ndogo, unakuta msomaji wa taarifa ya habari ni mwanaume, taarifa zenyewe asilimia 90 zinahusu wanaume jambo ambalo tunadhani linapaswa kuwekwa katika usawa kwani nafasi kwa mwanamke inapokuwa kubwa inafanya hata malengo yale ya SDGs yaende kama yalivyokusudiwa,” alisema Nyakiraria.
Nyakiraria alisema kikwazo kikuu ambacho kimewekwa bayana katika utoaji wa taarifa hizo ni wamiliki ambao wamejikita katika kuangalia maslahi yao binafsi bila kujali jinsia hali ambayo imekuwa ikiminya taarifa nyingi za zitazompa changamoto mwanamke katika kuijenga jamii.
“Tumegundua kuwa makosa mengine yamekuwa yakisababishwa na waandishi wenyewe, hali ambayo inazidisha uminyaji wa taarifa za wanawake, kwa mafunzo haya nina imani tutakuwa mabalozi wazuri wenye kuibua changamoto za mwanamke,” alisema Nyakiraria.
Mwenyekiti wa klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Kilimanjaro (MECKI), Bahati Nyakiraria. |
Pia alisema wakati mwingine Wahariri kwa maoni yao, wamekuwa wakiangalia soko kutokana na namna ya uendeshaji wa chombo husika.
“Wamiliki wakiishi vizuri na wafanyakazi wao itasaidia kupata muda wa kushauriana kwani kuna mawazo mazuri wanayo wafanyakazi wake kuhusu changamoto mbalimbali za wanawake hali ambayo itabadilisha mtazamo wa kuegemea soko zaidi na kuiacha jamii peke yake,” alisema Nyakiraria.
Aidha mwezeshaji huyo alisema kuwa kumekuwa na mfumo wa kiutamaduni ambao umekuwa ukiwafanya wanawake wajione kuwa ni watu wasioweza kufanya lolote bila uwepo wa wanaume na inapofikia wamepata elimu na kazi, jamii huwa inamchukulia kama mtu mwenye dharau asiyeweza kudhibitiwa hivyo kuongeza kundi kubwa la wanawake wasomi ambao hawajaolewa.
Hata hivyo wanawake wametakiwa kutoa ushirikiano wanapokutana na waandishi wa habari badala ya kuogopa kuzungumza mtazamo au changamoto zinazowakabili ili kutokomeza ukatili na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika umiliki wa rasilimali na nyanja zote za kimaisha.
Semina hiyo ya siku moja ilijikita katika kauli mbiu isemayo; “Mtandao wa Waandishi wa Habari Ngazi za Jamii: Habari za Wanawake na Uongozi.”
0 Comments:
Post a Comment