Monday, May 25, 2020

Unayakumbuka maneno haya “Get up and Fight sucker”


Mei 25, 1965 bondia Muhammad Ali alimtandika mwanasumbwi aliyekuwa na mvuto kwa wengi na fundi Sonny Liston na kuanzia hapo ufalme ukahamia kwa Ali ambaye wakati huo alikuwa akifahamika kwa jina la Cassius Clay Jr. kabla hajaanza kujiita Muhammad Ali.

Maneno haya yenye ukali na kejeli ndani yake hayatasahaulika baada ya Ali kumwangusha chini Liston, “Get up and Fight sucker” ikiwa na maana “Inuka na Upigane sasa”.  

Pambano hili linachukuliwa kuwa fupi kuliko mapambano yote ya uzito mkubwa katika historia. Katika mikusanyiko midogo walikuwa hata hawajakaa katika viti vyao wakati pambano likimalizika. Mara ya kwanza ilielezwa kuwa pambano lilisimama katika dakika ya kwanza (1:00) jambo ambalo halikuwa sahihi. Liston alianguka sakafu katika dakika ya 1:44 kisha akanyanyuka katika dakika ya 1:56 na mwamuzi wa mchezo Jersey Joe Walcott alisimamisha pambano hilo katika dakika ya 2:12

Ilikuwa hivi, mapambano baina ya Ali na Liston yanaingia katika rekodi ya dunia kuwa ni mapambano yaliyokuwa na mkanganyiko wa hali ya juu, miamba hii ya uzito mkubwa ilipigana kati ya Februari 25, 1964 – Mei 25, 1965. Pambano la kwanza lilichezwa huko Miami Beach, Florida ambapo Clay aliishia kwa kupigwa baada ya Liston kufunguka katika raundi ya saba ikiwa ni kazi nzuri aliyoifanya katika raundi ya sita.

La pili lilipigwa Mei 25, 1965 huko Lewiston, Maine na Ali alimzabua kwa KO katika raundi ya kwanza Promota wa zamani wa ngumi nchini Marekani Harold Conrad aliwahi kusema, “Watu wanamzungumzia Mike Tyson kabla ya kupigwa lakini kwa Liston ilikuwa zaidi ya ukali, ngumu kumsambaratisha….Wakati Sonny akikutazama kwa jicho baya. Sijali wewe ni nani, utabonyea hadi mita mbili”. Sasa baada ya pambano la kwanza Clay alitangaza hadharani kujiunga na Black Muslims na akawa anajiita Cassius X na mwezi mmoja baadaye alibadili jina lake kwa heshima ya kiongozi Elijah Muhammad.

Alizungumziwa kila kona kutokana na uamuzi wake huo hata Martin Luther King Jr. alikaririwa akisema "Wakati Cassius alipojiunga na Black Muslims na kuanza kujiita yeye mwenyewe Cassius X, amekuwa bingwa wa ubaguzi wa rangi.”

Kwa upande wake Liston naye alikamatwa na makosa ya kuendesha gari kwa kasi kupitiliza, kuendesha bila kuwa na leseni na pia kukutwa na silaha kinyume cha sheria.

Wakati akikamatwa Afisa wa Polisi alisema Liston alikuwa katika mwendo wa 122–128 kmh tena kwenye ukanda wa makazi ya watu jambo ambalo ni kosa. Pia alikutwa na silaha aina ya bastola revolver yenye risasi 22 na ndani ya gari Liston alikuwa na mwanamke ambaye hakukamatwa.

Afisa wa Polisi alisema ndani ya gari lake alizikuta chupa tupu za pombe kali aina ya vodka. Baada ya visanga hivyo kupita pambano likaandaliwa.  Laiti kama Liston angejua nini kingemkuta asingethubutu kupanda ulingoni siku hiyo huko Maine. Ali alimzabua kwa kile kinachofahamika kama “Phantom Punch” na Liston akaanguka sakafuni kama gunia na ukumbi mzima ukazizima kwa maneno “Fix”.

Baada ya pigano hilo kumalizika Ali alipoulizwa ni pigo la namna gani akasema linaitwa “the anchor punch” na alipoulizwa alifundishwa na nani akasema alifundishwa na mchekeshaji na mwigizaji wa filamu Stepin Fetchit ambaye naye alijifunza kutoka kwa Jack Johnson.

Ali alikuwa na nickname yake ‘Louisville Lip wakati Liston alikuwa akiitwa Big Bear. Kwa sasa wote wawili ni marehemu Ali alifariki akiwa na umri wa miaka 74 na hiyo ilikuwa Juni 3, 2016 huko Scottdale, Arizona na Liston alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 40 mnamo Desemba 30, 1970 huko Las Vegas, Nevada.

0 Comments:

Post a Comment