Friday, May 22, 2020

Elimu mwarobaini wa Uzururaji, Uchagudoa, Ombaomba

Paul Makonda

Hivi karibuni mkuu wa Dar es Salaam Paul Makonda alikaririwa akisema kuhusu kuwakamata wabunge waliokimbia vikao vya bunge ambao wengi wao ni wa upinzani lakini kuna maneno mawili aliyasema vizuri bila kupepesa mdomo, maneno hayo ni uzururaji na uchagudoa.

Pia RC Makonda aliwahi kuendesha operesheni jijini hapo ya kuwaondoa ombaomba, kwa kauli kwamba atakayepatikana akiwapa msaada ombaomba ambao husimama katika kando ya njia atatozwa kiasi cha shilingi laki mbili.

Nafahamu hayo yote ni makosa ya jinai kuyafanya katika mipaka ya nchi yetu kutokana na sheria zetu zilivyo licha ya mkanganyiko wake lakini swali moja muhimu ni kwamba yanaweza kuondoka kirahisi kama tunavyodhani, kabla sijasonga mbele niangazie hili.

Kosa la jinai ni tendo lolote ambalo limekatazwa kwa sheria, ambapo mtu yeyote akilitenda anakuwa ameikosea Jamhuri. Katika makosa ya jinai, mlalamikaji anakuwa ni Jamhuri, ikiwakilishwa na mwendesha mashitaka wa Serikali.

Mtu binafsi aliyedhurika kwa tendo la kijinai siye anayeshitaki mahakamani. Yeye anabakia kuwa ni shahidi tu, na ni mara chache kwamba Mahakama inaweza kuagiza kulipwa fdia kwa mtu aliyedhuriwa na tendo la kijinai.

Katika Makosa ya Jinai, mtu anayepatikana na hatia huadhibiwa, na anayeonekana hana hatia huachiwa huru. Adhabu za makosa ya Jinai ni pamoja na: kuachiwa kwa masharti, kifungo cha nje, faini, kifungo gerezani kwa muda maalum, kifungo cha maisha na kunyongwa hadi kufa.

Makosa yote ya Jinai sharti yawe yameandikwa katika sheria mbalimbali. Hata hivyo, kwa nchi yetu ya Tanzania, makosa mengi ya Jinai yametajwa katika Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania).

Hivyo Kifungu cha 176A kinasema Mtu yeyote akiwa ni muuza kilabu ya pombe, hoteli, nyumba, duka, chumba au mahali pengine panapofikiwa na watu mara kwa mara kwa ajili ya kununua au kunywa viburudisho vya namna yoyote, anayeruhusu au kukubali kwa makusudi makahaba wa kawaida kukusanyika na kubaki katika jengo lake kwa ajili ya ukahaba, mtu huyo atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atawajibika.

Pia kifungu cha 177(a) kinasema Yeyote miongoni mwa watu wafuatao- mtu aliyepatikana na makosa kwa mujibu wa fungu la 176 baada ya kuwa alipata kuonekana na makosa zamani ya kuwa mzembe na mzururaji; atahesabiwa kuwa ni muhuni na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miezi mitatu jela, na kwa kila kosa litakalofuata kifungo cha mwaka mmoja jela.

Baada ya kuangazia hapo, niseme mtu yeyote yule haidhuru awe mbali vipi na shughuli za kisayansi, mapambano ya kisiasa, harakati za kimapinduzi na kadhalika, huwa anakuwa na hamu ya kutaka kujua vile ulimwengu utakavyokuwa kwa wakati ujao. Mustakabali wake ukoje? Maafa ya vita au furaha ya maisha ya amani.

Dunia na maumbile yake, yakiwemo majani, miti, wanyama, ndege, pamoja na binadamu mwenyewe atakuwaje? Atasalia milele au yote yenye uhai yataangamia kutokana na maendeleo ya kisayansi na ufundi?

Je, unyonyaji na ukandamizaji, unyonge pamoja na maovu mengine yaliyoiandamana jamii ya binadamu, yatakomeshwa kabisa na milele au la maovu yote hayo yatadumu daima?

Malimwengu yamzungukayo mwanadamu hayana kikomo wala mipaka yoyote ile na hatimaye hujaa siri ambazo mwanadamu anaweza kuzigundua kwa taratibu tu, hatua kwa hatua lakini hadi sasa binadamu huyu hajafaulu kamwe kuzijua zote kwa ukamilifu.

Mtaalamu wa Elimu ya Jamii nchini Uingereza Herbert Spencer (1820-1903) alisema kuwa wanadamu wa rangi nyeusi wamejaliwa kuwa akili na akili isiyoweza kujizamisha katika uwazaji mtupu. Spencer aliongeza kusema akili yake Mwafrika ni akili iliyojifungia katika mitokezo tu (yaani vinavyoonekana). Kitendo hicho humfanya Mwafrika huyu kutegemea hisia zaidi kuliko mawazo. Hali ambayo itamfanya ashindwe kupokea fikara za daraja la juu.

Sasa muono huo wa Spencer ulienda sambamba na ule wa  msomi wa Ujerumani Georg Wilhelm Friedrich Hegel (1771-1831) ambaye alisema Afrika imezama katika dimbwi la giza ambapo akili yake haijafikia  kwenye kiwango cha fikara pembuzi (objective thinking). Hivyo kwa mantiki hiyo Mwafrika hawezi kuibua muono wake wa daraja la juu ambao utaweza kupita mfumo wa kufikiri kwa hisia.

Kwa maana nyepesi ni kwamba mfumo wa Mwafrika akiwamo Mtanzania umejengeka katika imani na mapokeo, hakuna hali ya ujikosoaji (self-criticism) na mawazo pinganifu. Watu huwaza na kuyapokea mambo kama yanavyoelezwa katika mfumo wa mapokeo hali ambayo huwafanya waishi katika ulimwengu wa mitholojia.

Kwa upande mmoja mtazamo huo unaweza kuwa na afya katika kuondokana na watu wanaozurura, machagudoa na ombaomba lakini sio kazi nyepesi kama inavyochukuliwa, binafsi ni mwamini wa binadamu mmoja kubadilika na sio kama kundi.

Hapa kuna pande zote mbili utawala na wananchi husika wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, nini kifanyike katika kufikia kudhibiti kabisa hali hii ambayo tumeitungia sheria miaka na miaka lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu? Tumuangalie mtu huyu.

Mwanafalsafa ya Ugiriki Socrates katika suala juu ya maadili alisema elimu na maadili ni vitu vinavyokwenda sawa. Kama maadili yanaendana na kuifanya roho kuwa nzuri kadri iwezekanavyo ni lazima kujua kitu gani kinachoifanya roho iwe nzuri.

Socrates aliona kuwa matendo yetu ambayo ni mabaya au mazuri ni matokeo ya elimu tuliyonayo, basi matendo yetu ni lazima yatendwe kulingana na ama elimu yetu au maumbile.

Pamoja na ukweli huo Socrates alikuwa tayari kukubali ukweli kuwa binadamu anatenda vitendo vya dhambi. Alisema Mtu kama kiumbe mwenye akili; shughuli yake maalum ni kuongoza maisha yake kulingana na maumbile yake yaani kiumbe mwenye kufikiri.

Hata hivyo Socrates aliona kuwa kila binadamu ana tamaa isiyoepukika ya kupenda kuwa na furaha au kuwepo kwa hali nzuri ya roho yake hivyo huchagua vitendo fulani kwa matumaini kuwa vitamletea furaha.

Anahoji Socrates ni tendo gani au tabia gani itampa furaha huyu mtu? Socrates alifahamu kuwa baadhi ya tabia huonyesha kama zinatoa furaha lakini katika ukweli halisi hazitoi furaha. Hivyo basi kwa namna hivyo mtu huyu hupenda kuwa na madaraka, anasa za mwili na kumiliki vitu ambavyo huviona ni alama ya mafaniko na furaha huku akishindwa kufahamu kuwa anachanganya hivi vitu na msingi halisi wa furaha.

Unaweza kumuona mtu anayemsaidia ombaomba anadhani kwa maoni yake kuwa anamsaidia maskini na kwamba atapata thawabu peponi siku moja. Utamsikia mtu akisema “…mimi bila kusaidia ombaomba sioni kama nabarikiwa (yaani kuwa na furaha)…” huku akisimamia imani na mapokeo.

Pia unaweza kuona mtu amekuwa na maisha mazuri ana gari, nyumba, fedha lakini kila siku ni kulala na wanawake wa kila namna kwa imani kwamba anapata furaha bila kufahamu kuwa anachanganya mafaili.

Machangudoa wanasimama katika vichochoro mbalimbali kwasababu kuna watu ambao uwezo wao wa kufikiri umekaa katika hisia tu na ndio sababu kila siku tunatukanwa na wazungu kuwa watu tusiojiweza kila siku tunawategemea wao.

Hivyo ukibadilika na kutambua ukweli kuhusu furaha ya kweli ni utulivu wa roho hautakwenda kuwafuata machagudoa hali ambayo itawafanya wapungue kumsubiri mtu kama wewe.

Kwa upande wa utawala mwarobaini mwa changamoto hizi ni kama alivyosema mwanafalsafa wa Ugiriki mwanafunzi wa Socrates, Plato katika kitabu chake cha Republic (Jamhuri) kwa kutumia uhusiano uliopo kati ya meli na nahodha, alisema kama ilivyo katika meli ambapo uwezo wa uongozi wa nahodha unategemea elimu yake ya majini, ni hali hiyo hiyo inatawala kwa meli ya nchi, kwamba meli ya nchi lazima iongozwe na nahodha ambaye ana elimu thabiti au elimu ya kutosha.

Plato aliamini kuwa elimu ya viongozi ilipaswa ihusiane na nidhamu ya hali ya juu ya kiakili ambapo mkazo ulikuwa kwenye masomo ya sayansi ya uendeshaji na uendeshaji vitu kisayansi.

Elimu kwa  kadri ya Plato ilikuwa siyo jambo la kusoma vitabu mbalimbali na kupata shahada bali ni ile hali inayomfanya mtu awe na uwezo wa kujua ukweli kama ulivyo na kuishi kadiri ya misingi ya elimu hiyo na kwamba elimu lazima imfanye mtu abadilike kutoka kwenye ulimwengu wa kivuli na kwenda kwenye ulimwengu wa mwanga.

Hata wewe mtanzania uliye mzururaji, changudoa, ombaomba unaweza kubadilika kutoka hivyo ulivyo na ukawa mtu mwingine mzuri ambaye jamii itakukubali. Tuachane na dhana ya kutumia njia ngumu kutatua tatizo hili bali itumike njia ya kisayansi kwa kuwapelekea elimu kwa njia mbalimbali watu hao hatimaye hawa wazungu wataacha kuicheka Tanzania na Afrika kwa ujumla.


0 Comments:

Post a Comment