Aprili 15, 2020 ilikuwa siku ya majonzi kwa wafuatiliaji wa filamu za
kimataifa baada ya kuondokewa na mmojawapo wa wachezaji wa filamu wa nchini
Marekani Brian Dennehy. Nyota huyo alifariki akiwa na umri wa miaka 81.
Dennehy ni mshindi wa tuzo ya Golden Globe, tuzo mbili za Tonny na tuzo
moja ya Laurence Olivier huku akishiriki tuzo za Emmy takribani mara sita enzi
za uhai wake.
UTAMKUMBUKA VIPI DENNEHY?
Wengi wa vijana wa karne ya 21 wanaweza wasimjue vizuri nyota huyo
lakini wa karne ya 20 na wafuatiliaji wengine wanaweza kuona namna Dennehy
alivyoonyesha umahiri wake katika filamu mbalimbali alizocheza.
Lakini ya kwanza kwa jamii ya Kiafrika naweza kusema ni ile ya First
Blood ambayo alicheza na Sylvester Stallone ‘Rambo’, Richard Crenna ‘Kanali Sam
Trautman’ iliyotoka mwaka 1982. Katika filamu hiyo ya First Blood hakika
alionyesha kuimudu nafasi yake katika Jeshi la Polisi la Marekani. Dennehy
alitumia jina la Will Teasle akiwa ni Afisa Jeshi la Polisi
Katika filamu ya First Blood inaanza ikiwa ni baada ya miaka saba baada
ya kumaliza vita huko Kusini Mashariki wa Asia, veteran wa vita vya Vietnam
John Rambo anaamua kwenda kumtembelea rafiki yake wa siku nyingi, akiwa na
malengo ya kujifunza hapo ilikuwa baada ya rafiki yake kufariki dunia kwa kansa
mwaka mmoja kabla ya safari hiyo, rafiki huyo alifariki kutokana na kemikali ya
sumu iliyokuwa ikitumika wakati wa vita vya Vietnam miaka ile ya 1961 hadi 1971
maarufu kama Agent Orange.
Rambo anaonekana akiendelea na safari yake kuelekea katika mji mdogo wa
Hope, Washington. Wakati anarudi baada ya safari isiyo na mafanikio anakutana
na Afisa wa Polisi Will Teasle ambaye jina lake halisi ni Brian Dennehy.
Will Teasle anamzuia Rambo kuendelea na safari yake akimchukulia kuwa ni
mtu asiyehitajika katika mji huo. Wakati akiwa na Teasle katika gari la Polisi
anamuuliza kuhusu wapi anaweza kupata chakula. Teasle anamjibu kuwa chakula cha
jioni kinapatikana kilometa 30 kutoka walipokuwa. Teasle anamtoa nje ya mji wa Portland
ambako Rambo alikuwa ametokea.
Rambo anashushwa na Teasle kwenye gari na kutakiwa kutorudi tena mjini.
Wakati anataka kumtoa kinguvu Rambo anakataa kuondoka lakini baadaye anakubali
kushuka.
Teasle anaondoka gari lake na kuanza safari ya kurudi mjini, akiwa
kwenye gari anamchungulia kwenye kioo cha pembeni cha gari lake na kumuona
Rambo akirudi tena mjini hivyo anamkamata kwa kosa la uzururaji na kumfikisha
katika kituo cha polisi.
Sasa kutokana na hali yake ya kimaisha alivyokuwa Vietnam Rambo alikuwa
na nywele ndefu na kisu kikali cha kivita. Akiwa kituo cha Polisi anakamatwa na
kunyang’anywa kisu chake kitendo hicho anakifanya Mkuu wa Kituo Msaidizi Art
Galt.
Wasaidizi wa Teasle wanaanza kumtesa Rambo na kumfanyia dhihaka kama
zote, hali ambayo inamkumbusha Rambo kama Mateka wa Kivita (PoW) alipokuwa
Vietnam.
Walipojaribu kutaka kumnyoa nywele zake kwa kutumia wembe mkali ndipo
anafanikiwa kuwadhibiti na kukichukua tena kisu chake na kuingia msituni.
Teasle anaratibu timu ya kumtafuta Rambo msituni. Akiwa msituni Galt
anauawa na Rambo kitendo ambacho Teasle kinamuudhi. Rambo anambembeleza Teasle
kuwa kifo cha Galt kilikuwa ni ajali tu wakashindwa kumwelewa na kuzidi
kumtafuta kwa udi na uvumbi.
Hapo sasa ndio wanaona makali ya Rambo akiwamo Teasle mwenyewe
kunusurika kuuawa kutokana na Rambo kuwa miongoni mwa wanajeshi wa zamani
katika kikosi maalum cha Green Beret.
Rambo ‘anamkwida’ Teasle na kumwelezea kuwa anaweza kuwamaliza wote
endapo watendelea kumfuatilia.
Hatimaye mwalimu wake Rambo, Kanali Trautman anaingilia suala hilo na
kumtia mikononi mwa Polisi Rambo ambaye anahukumiwa jela na kazi ngumu.
Hivyo ndivyo unaweza kumwelezea Brian Dennehy katika filamu ya First
Blood (1982). Alizaliwa Julai 9, 1938 huko Bridgeport, Connecticut.
Alifariki dunia Aprili 15, 2020 huko New Haven, Connecticut. Aliingia
katika taaluma ya uigizaji wa Kimataifa akiwa na umri wa miaka 38.
Aliigiza filamu nyingi ikiwamo ya Death of Salesman (2000) akifahamika
kwa jina la Willy Loman. Pia Gorky Park (1983), Silverado (1985), Cocoon
(1985), F/X (1986), Presumed Innocent (1990), Romeo + Juliet (1996), na Knight
of Cups (2015).
Buriani Brian Dennehy, asante kwa mchango wako katika ulimwengu na
maisha aliyokupa Mwenyezi Mungu hapa duniani.
0 Comments:
Post a Comment