Wananchi mkoani
Kilimanjaro wamewataka wakuu wa mikoa wengine nchini kuiga mfano wa Mkuu wa
Mkoa huo Dkt. Anna Mghwira kutokana na uamuzi wake wa kujitangaza kupata
maambukizi ya virusi vya Corona na kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi hayo
wakiwa katika utendaji wao wa majukumu yao ya kiserikali.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti wananchi hao walisema kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya
viongozi wengi nchini kuhusu afya zao hali ambayo imekuwa ikiwafanya kupata
vifo vya ghafla.
“Alichokifanya mama
ni jambo la kuungwa mkono na wakuu wa mikoa wengine katika mapambano ya maradhi
haya ya corona kwa kweli sikufichi viongozi wengi wamekuwa na tabia ya kutoweka
bayana afya zao kitu ambacho kuna baadhi yao hufa vifo vya ghafla,” alisema
Noela Lyimo wa Rombo.
Wananchi hao
waliongeza kuwa wakuu wa mikoa wamekuwa mbele katika kufuatilia mambo ya watu
wao huku wakisahau afya zao na kuziweka wazi pindi wanapokutwa na maradhi.
“Nafikiri viongozi
wengine hususani wakuu wa mikoa wanatakiwa kuiga mfano wa mkuu wetu wa mkoa kwa
kutangaza hali yake ya afya hasa kipindi hiki cha maradhi ya corona,” alisema
Elizabeth Mallya wa Moshi.
Hata hivyo wananchi
waliongeza kuwa uwazi unahitajika zaidi katika kukabiliana na maradhi haya ili
kuchukua tahadhari ya maambukizi ya corona badala ya kujikita katika kujifariji
tu.
“Unajua siku hizi
dunia ni kijiji huwezi kumdanganya mtu kuhusu yanayoendelea duniani hivyo
kuweka wazi kuhusu maambukizi haya ni jambo jema kwani hii Tanzania
tusipojijali wenyewe hakuna wa kutujali,” alisema James Mtui.
HULKA YA DKT.
MGHWIRA
Licha ya wengi
kuunga mkono wakuu wa mikoa wengine na viongozi wa serikali kuweka wazi taarifa
zao za afya hawakusita kufunguka kuwa kuambukizwa kwa mkuu huyo wa mkoa
kunatokana na hulka aliyonayo katika ya ukarimu.
“ Mama ni kiongozi mzuri sana
anawajali watu wake, amekuwa mkarimu na ndio maana akasema haelewi aliipatia
wapi. Binafsi namfahamu kuwa hupenda kusalimia na kuonana na watu kila wakati
sasa kipindi hiki cha Corona ni hatari kwa kweli,” alisema Ayubu Temu wa Hai.
Kwa upande wake
mwananchi aliyejitambulishwa kwa jina la Eliakunda Mosha wa Siha alisema Dkt.
Mghwira atakuwa amepatia maambukizi ya Covid-19 katika ziara zake za mara kwa
mara za kuwatembelea baadhi ya watu ikiwamo katika mafuriko ya hivi karibu na
kuongeza kwamba ni funzo kwa wakuu wengine wa mikoa ambao hawachukui tahadhari
ya ugonjwa huo.
Pia Dkt. Massawe wa
Mjini Moshi anayejishughulisha na tiba mbadala amesifu afya ya Mkuu huyo wa
mkoa ya kupenda kufanya mazoezi na kula vyakula vya kuujenga mwili.
“Hakika mama yuko
imara kwani nilimsikia akisema hakuona dalili zozote hadi alipopima, hiyo ni
kutokana na kufanya mazoezi na kula vyakula vya kuujenga mwili. Hiyo inaweza
kutufundisha kitu kuwa yatupasa kuzingatia afya zetu ili kuinua kinga za miili
dhidi ya maradhi mbalimbali sio tu corona hata magonjwa mengine,” alisema Dkt.
Massawe
HALI IKOJE KATIKA
MASOKO MJINI MOSHI?
Awali kabla ya
taarifa za mkuu wa mkoa kuathirika kwa corona katika masoko maarufu ya Mbuyuni
na Memorial kulikuwa na sura mbili kuhusu uvaaji wa barakoa na kunawa mikono.
Mfanyabiashara wa
soko la Memorial aliyetambulisha jina moja la Shayo alisema zoezi la kunawa
mikono linakwenda vizuri isipokuwa barakoa.
“Kunawa wengi
wamekuwa wakilazimishwa kunawa kabla ya kupata huduma ndio maana unaona
limeelewa kwa uzito mkubwa, barakoa imekuwa ikienda mwendo wa pole sasa kitendo
cha Mama yetu (Dkt. Mghwira) kujiweka wazi kimeongeza uzito wa uvaaji wabarakoa
kwani kuna watu walianza kuzembea kutokana na taarifa mbalimbali walizokuwa
wakipata,” alisema.
Inavyoonekana sasa
hali imekuwa tofauti kutokana na wengi kuingiwa na hofu kuwa maradhi yamebisha
hodi mkoni humo kwa kasi tofauti na ilivyodhaniwa.
“Sikuwa nachukulia
kwa uzito mkubwa sana katika uvaaji wa barakoa kwani niliona taarifa nyingi
zinanichanganya tu lakini kwa sasa alivyojitangaza mkuu wa mkoa hakika naamini
tuko kwenye hatari,” alisema mfanyabiashara katika soko la Mbuyuni.
Aprili 29 mwaka huu
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira aliweka bayana kuhusu kupata
maradhi ya Corona.
“Nimepima na matokeo
yamekuja yameonesha nimeambukizwa virusi vya corona, sioni dalili za ugonjwa
sina homa sikohoi lakini vipimo vimeonesha, hii ni dalili kwamba Watu wengi
tunaweza kuwa tunetembea tukiamini tuko salama kumbe hatuko salama, sijui niliambukizwa
lini,” alisema Dkt. Mghwira.
0 Comments:
Post a Comment