Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Dkt. Anna Mghwira amesema watembea kwa miguu katika mpaka wa Tanzania na Kenya
ni changamoto kubwa katika makabiliano ya kusambaa kwa virusi vya Corona licha
ya juhudi zinazoendelea katika kudhibiti janga hilo linalotikisa dunia kwa
sasa.
Hayo yanajiri ikiwa ni siku
chache baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapo kuwakamata waendesha bodaboda
watano kwa tuhuma za kuwasaidia watu kutoka nchini Kenya na kuwaingiza nchini
kinyemela.
Akizungumza katika
mahojiano maalumu na Radio Fountain ya mjini Moshi Aprili 13 mwaka huu, Dkt. Mghwira alisema
watembea kwa miguu kutoka Kenya wamekuwa wakiingia kwa njia za panya hali
ambayo inakuwa ngumu kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Covid-19.
“Iko wazi katika mpaka wa
Tanzania na Kenya kwa upande wa Kilimanjaro kuna njia zaidi ya 400 za panya ambazo
ni ngumu kudhibiti kwa kutumia jeshi la Polisi pekee,” alisema Dkt. Mghwira.
Dkt. Mghwira aliongeza kuwa
ili kudhibiti watembea kwa miguu ni lazima jamii iliyopo katika mpaka huo
ishirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata watu wanaovuka kutoka
Kenya kuingia Tanzania.
“Ushirikiano na wananchi
waliopo katika mpaka ni muhimu katika kudhibiti wanaoingia kinyemela, wananchi
wanaokaa hapo wanawajua watu wanaotoka huko,” alisema Dkt. Mghwira.
Kwa upande mwingine katika
tukiola kukamatwa kwa vijana watano waendesha bodaboda Mkuu wa Wilaya Rombo Agness
Hokororo alisema kuna vijana wa bodaboda ambao wanafanya biashara ya kuingiza
watu kutoka nchi jirani ya Kenya kwa kutumia njia za panya huku kukiwa na
malipo fulani wakipatia aliwaonya kuacha kufanya hivyo kwani wakibainika hatua
kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Kwa sasa kuna madereva wa
bodaboda watano walikamatwa wakiwa wamebeba watu kutoka Kenya ambao walikuwa
wakiwavusha kwa kutumia njia za panya,
tuliwakamata na kwa sasa wako kwenye karantini
kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa kwa siku kumi na nne, na mara
baada ya kutoka huku watafunguliwa
mashtaka,” alisema.
Hokororo alisema serikali
imekuwa ikitoa elimu kwa waendesha bodaboda juu ya kuacha kuwabeba watu
wanaotoka Kenya na kuwaleta huku Tanzania lakini kuna watu wachache bado wanaendelea kukaidi na kwamba wale ambao
wanaoshindwa kutekeleza amri ya serikali wamekuwa wakikamatwa.
Hata hivyo Mkuu huyo wa
Wilaya ya Rombo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kupokea wageni hasa katika
kipindi hiki ambacho ni hatari kwa nchi.
0 Comments:
Post a Comment