Apple Gabriel |
Mauti au kifo ni
mwisho wa uhai; kwa lugha ya biolojia mwisho wa michakato yote ndani ya
kiumbehai ambayo ni dalili za uhai.
Kifo hutokea kutokana na sababu mbalimbali
kama vile umri mkubwa unaosababisha michakato ya kimsingi mwilini kusimama
polepole, muda mrefu wa maisha unaoruhusu makosa na kasoro kujumuika na
kusababisha madhara (mfano: saratani).
Licha ya sababu zote
hizo bado kifo hakizoeleki, pindi umpendaye anapofariki dunia basi machozi,
huzuni na simanzi hutawala. Hivyo ndivyo ndani ya juma moja simanzi, huzuni,
majonzi na machozi vilitawala ulimwengu
wa reggae pale wasanii watatu wa muziki huo kufariki dunia.
Wasanii hao ni
Apple Gabriel, Delroy Washington, na Bob Andy.
Katika makala ya leo tutawaangazia hao.
APPLE GABRIEL
Huyu ni mwanzilishi na
mwanachama wa zamani wa kundi maarufu la muziki wa reggae la Israel Vibration.
Jina lake halisi ni Albert Craig. Mauti
yalimkuta Jumatatu ya Machi 23, 2020. Chanzo cha kifo chake ni magonjwa
mchanganyiko lakini sio ugonjwa Corona kama wengi walivyodhani.
Apple Gabriel alikuwa
akipigania uhai wake kutokana na maradhi ya Polio tangu akiwa mmtoto na mwili
wake haukuwa katika hali nzuri huku ripoti zikisema miaka 10 iliyopita alikuwa
amedhoofu na hali ya kimaisha haikuwa nzuri kwake.
Mara ya mwisho
kuonekana katika mitandao ya kijamii hususani Facebook ilikuwa ni Machi 7 mwaka
huu ambapo alikuwa akizungumzia namna kiharusi kilivyomfanya hata upande mmoja
wa mwili wake kupooza huku akiruhusiwa pasipo kufahamu mahali sahihi pa kwenda.
Maisha ya nyota huyo
hayakuwa mepesi hata kidogo, aliendelea kupanda na kushuka baada ya kuachana na
Israel Vibration mnamo mwaka 1997.
Alianza vizuri katika maisha yake ya kuongoza uimbaji (solo career)
albamu yake ya Another Moses ya mwaka 1999 ilipokelewa vema. Pia alifanya kazi na wasanii wengine na bendi
kadhaa wakiwamo Groundation or Jahcoustix.
Haikutosha aliopanda
katika matamasha jukwaani kama mwaka 2009 nchini Israel. Baadhi ya nyimbo
maarufu na kali wakati akiwa na Israel Vibration We A De Rasta, Why You So
Craven, Oh Jah Solid Rock, Mud Up, Rude Boy Shuffling, Friday Evening na Walk
The Streets of Glory.
DELROY WASHINGTON
Alifariki dunia Machi
27, 2020 jijini London, Uingereza kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19. Alizaliwa mnamo mwaka 1952 Westmoreland nchini
Jamaica na familia yake ilihamia nchini Uingereza wakati akiwa mtoto miaka ile
ya 1960.
Alianza muziki akiwa
meneja wa kuratibu ziara na mara chache katika vipindi vya muziki katika bendi
ya Rebel. Wakati alipoingia kikamilifu katika uimbaji alikuwa solo akirekodi na
Count Shelly na baadaye akimsaidia Bob Marley
na The Wailers katika albamu mbalimbali.
Alikuja kuwa rafiki
wa karibu wa waimbaji maarufu miaka ya 1970 na baadaye aliwavutia wengi nchini
Uingereza kutokana na mistari katika nyimbo zake.
Mnamo mwaka 1976
alitoa albamu yake ‘I Sus’ na mwaka 1977 alitoa albamu iliyofahamika kwa jina
la Rasta. Mbali ya mchango wake mkubwa katika muziki alileta mabadiliko makubwa
alipofanikiwa kuwa mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Muziki
wa Reggae nchini Uingereza ambako alifanya kampeni ya kutambuliwa kwa London
Borough huko Brent kama makao makuu ya Muziki wa Reggae nchini Uingereza na
Ulaya kwa ujumla.
BOB ANDY
Keith Anderson
maarufu Bob Andy alifariki dunia Machi 27 mwaka huu akiwa na umri wa miaka 75
kutokana na kuugua kwa maradhi ya saratani.
Nyota huyo aliaga
dunia nyumbani kwake Stony Hill, St. Andrew jijini Kingston huko Jamaica baada
ya kupambana na saratani kwa muda mrefu. Mwanzilishi huyo wa kundi The Paragons
alichukuliwa kuwa miongoni mwa waandishi wa muziki huo wenye ushawishi mkubwa
ulimwenguni.
Haikutosha kutoa
nyimbo kali kwa sauti yenye kuvutia kama I've Got to Go Back Home, Feeling Soul
or Too Experienced bali Bob Andy alionyesha uwezo mkubwa kwa nyimbo kali kama I
Don't Want To See You Cry for Ken Boothe na ile ya Feel Like Jumping for Marcia Griffiths.
Baadaye alikuja
kupata umaarufu mkubwa pale walipoungana wawili Bob na Marcia kwa ajili ya
kulikamata soko la kimataifa na wakafanikiwa kufanya hivyo miaka ile ya 1970,
nyimbo kama Young, Gifted And Black or Pied Piper zilijidhihirisha wazi kuwa
Bob Andy alikuwa na kipaji kikubwa mno katika medani ya muziki wa reggae.
Baada ya Marcia
kuondoka na kwenda zake kuungana na I-Threes, Bob Andy aligeukia kategori ya
kucheza na kuigiza. Ziara mbalimbali za muziki zilimfuata mkongwe huyo pale
alipotua jijini Addis Ababa huko Ethiopia wakati wa kumbukizi ya miaka 60 ya
kuzaliwa kwa Bob Marley mnamo mwaka
2005. Boby Andy alizaliwa Oktoba 28, 1944 Kingston Jamaica. Hakika mtakumbukwa.
Gazeti la Tanzania Daima Aprili 3, 2020 |
0 Comments:
Post a Comment