Wakazi wanaoishi kuzunguka Dampo la Takataka
la Kaloleni mjini Moshi wametishia kufanya maandamano kwa kile wanachodai
kuzibiwa riziki zao wakati ambao manispaa hiyo inajiandaa kulifunga jalala hilo
kutokana na sababu za kiusalama.
Hayo yanajiri wakati ambao Manispaa ya Moshi
ipo katika hatua za mwisho za kuanza kutumia dampo jipya lililopo umbali wa
kilometa 15 kutoka mjini hapo, ikiwa ni sehemu ya kuboresha afya na mazingira ya
mji ambao umekuwa ukisifika kwa usafi na utunzaji wa mazingira nchini.
Wakizungumza mbele ya Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Moshi Raymond Mboya alipofanya ziara ya kushtukiza katika dampo
hilo walisema wamekuwa na ajira binafsi kwa muda mrefu kupitia dampo hilo kwani
wamekuwa wakijipatia kipato kwa kuokota mabaki ya vifaa mbalimbali ambavyo
wanapokwenda kuviuza huwapatia fedha za kujikimu.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukijipatia kipato
kupitia dampo hili sasa Meya unapotaka kulihamisha sisi tunakuwa kwenye
mazingira gani, tumesomeshea watoto wetu na kuwalisha kupitia dampo hili. Kwa
hili hatutakubali,” alisema mwanamke mmoja (jina tunalihifadhi).
Aidha wakazi hao walidai mbele ya Mstahiki
Meya kuwa kuliweka mbali na mji ni kuwafanya kuanza upya maisha yao ambayo
walizoea hapo.
“Ni kweli tunaonekana kama hatuna thamani
kwani tunashinda kwenye dampo hili lakini mwanamke anayefanya hapa dampo na yule
wa Mbuyuni na Manyema ni tofauti hata katika maisha, kwa mfano mimi kwa wiki
napata sio chini ya laki moja na pia nimeajiri vijana ambao kwa siku nawalipa
sio chini ya 4,000 kunisaidia wakati wa kule hawezi kufanya hivyo,” aliongeza
mwanamke huyo.
Pia walipoulizwa kuhusu usalama wa afya zao
licha ya maisha waliyoyazoea katika dampo hilo walisema uhai wa mtu hauko
mikononi mwa mtu upo mikononi mwa Mungu na ndio sababu wamezaa watoto wakiwa
hapo na watoto hao wamekulia hapo kwa kazi ya dampo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya Mboya alisema
hakuna namna ya kufanya zaidi ya kulifunga kwani wananchi ndio walisogea kwenye
eneo la dampo kwa miaka mingi lakini kwa sasa limejaa na linatishia usalama.
Mboya alisema uongozi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, umeridhishwa na ujenzi wa jalala la kisasa (Dampo), ambalo linatarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa
mwezi Aprili mwaka huu.
“Manispaa hiyo inatekeleza mradi wa ujenzi wa
dampo la kisasa ili kuwezesha wananchi kupata eneo la kutupia taka ngumu ambazo
zimekuwa zikizalishwa majumbani na masokoni, dampo la Kaloleni limejaa hali
ambayo inahatarishaafya kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka dampo lilo,”alisema.
Mchakato wa ujenzi wa dampo jipya la Mtakuja
ulianza tangu mwaka 2019, hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha zaidi ya
Sh bilioni 2 chini ya usimamizi wa kampuni ya ukandarasi ya Rocktrotinic Ltd.
ya mjini Moshi.
Gazeti la Tanzania Daima Aprili 4, 2020 uk. 18....Wakazi wa Kaloleni watishia kuandamana. |
0 Comments:
Post a Comment