Thursday, April 2, 2020

Mwanzilishi wa All Africa Games Jean Claude Ganga afariki dunia akiwa na umri wa miaka 86

Jean-Claude Ganga. (1934-2020)

Mwanzilishi wa Mashindano ya All Africa Games na Rais wa zamani wa Kamati ya Olimpiki barani Afrika (ANOCA) Jean-Claude Ganga amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86 jijini Brazzaville, Kongo.

Enzi za uhai wake Ganga aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Jamhuri ya Kongo ikiwamo ya Waziri wa Michezo. Ganga atakumbukwa kwa kupambana hadi kuanzishwa na kufanyika kwa Mashindano ya All Africa Games kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1965 na yalifanyika Congo-Brazzaville.

Kwa upande wake Rais wa ANOCA Mustapha Berraf katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka Abuja, Nigeria alisema, “Ni pigo kubwa katika medani ya Olimpiki ya Afrika. Rais Ganga alikuwa ni mtu mwenye hekima, alikuwa mhamasishaji na mwenye ushawishi kwa viongozi wengi wa michezo. Alifanya mengi kwa ajili ya kuhamasisha michezo na olimpiki katika bara letu, kazi zake haziwezi kuelezewa kwa maneno machache. Kwa niaba ya vyama vyote vya kitaifa vya Olimpiki hapa Afrika na kwa niaba yangu mwenyewe, ningependa kutoa rambirambi zangu kwa familia na ningeomba wazipokee. Sisi ni waja wake Mungu tulitoka kwake na Kwake tutarudi. Mungu amlaze mahala pema peponi.

Jean-Claude Ganga katika taifa lake alikuwa akifahamika kama ‘Mjenzi Mkuu wa Michezo.’ Alizaliwa Februari 28, 1934 Brazzaville, Congo (zamani ilikuwa ikifahamika kama French West Africa). Amefariki dunia Machi 28, 2020 katika mji wa Mansimou karibu na mto Congo, nje kidogoya jiji la Brazzaville.

0 Comments:

Post a Comment