Hussein Msaki ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali Miembeni Action & Passion For People with Disability. |
Watu wenye ulemavu
mkoani Kilimanjaro wametoa masikitiko yao katika vita dhidi ya maambukizi ya
virusi vya Covid-19 wakisisitiza kuachwa nyuma katika juhudi za kuzuia
maambukizi ya maradhi hayo yanayotikisa dunia kwa sasa.
Akizungumza na JAIZMELA hili ofisini kwake Hussein Msaki ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo
ya Kiserikali Miembeni Action & Passion For People with Disability yenye
makao yake makuu mjini Moshi alisema, “Ili kuondokana na ugonjwa huu maana yake
ni kupata maelekezo sahihi ambaye yatakuwa suluhisho la kuzuia kuenea kwa
corona. Lakini kundi la watu wenye ulemavu linakabiliwa na wakati mgumu katika
kipindi hiki.”
Msaki alisema
changamoto katika kundi la wenye ulemavu ni kubwa kutokana na kwamba asilimia
kubwa ya familia zenye ulemavu zipo katika dimbwi kubwa la umaskini na zimekuwa
zikishindwa kupata huduma kama watu ambao sio walemavu.
“Sisi kama taasisi
kwa muda mchache ambao ugonjwa huu umeikamata dunia na kuingia nchini kwetu,kundi
la wenye ulemavu limekuwa katika mtego, umaskini umekuwa changamoto katika
mapambano haya…taasisi yetu imefanya utafiti ambapo asilimia 80 ya familia
ambazo zenye wenye ulemavu zimekuwa zikilelewa na mzazi mmoja; pia asilimia 70
ya familia zenye mwenye ulemavu zimekuwa chanzo cha kugawa familia hiyo,”
alisema Msaki.
Mkurugenzi huyo
aliongeza kuwa maagizo yamekuwa yakitolewa na mamlaka husika lakini wenye
ulemavu wamekuwa wakisahaulika hali ambayo imekuwa ikizidisha hofu kwa kundi
hilo kila kukicha katika mapambano dhidi ya Corona.
“Mtu ni kiziwi
maelekezo ya kujikinga na Corona anayapataje?, mtu ni kipofu anaionaje ndoo ya
kunawia maji, mtu ni kiwete anaifikiaje hiyo ndoo?,nimefika katika hoteli moja
nikiwa na wheelchair ndoo ya maji ya kunawa ipo juu nafanyaje sasa hapo, ndoo
si rafiki, unaona jinsi gani mwenye ulemavu ametengwa, ” anahoji Msaki.
Hata hivyo Msaki anaziangukia
taasisi zisizo za kiserikali, watu binafsi na serikali yenyewe kuliangalia
kundi hilo la wenye ulemavu ili kutatua changamoto hizo wakati dunia ikiwa
kwenye mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya Corona.
“ Tunaiomba serikali
na mamlaka zake iliangalie suala hili ili kutafuta namna ambavyo wanaweza
kuwasaidia watu wa kundi hili, nao wanahitaji kuishi. Wizara husika
zishirikiane na taasisi husika za wenye ulemavu; gharama za vifaa vipo juu
mashirika ya kijamii yajitokeza kutusaidia. Katika kipindi hiki kigumu kundi
ambalo linaweza kuangamia kwa kasi kubwa ni la wenye ulemavu,” alisisitiza
Msaki.
Hussein Msaki ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali Miembeni Action & Passion For People with Disability akinawa mikono kabla ya kuingia ofisini kwake. |
0 Comments:
Post a Comment