Shirika la Reli Tanzania (TRC), limewataka wakazi wa
Klimanjaro na viunga vyake kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya reli,
ikiwemo kufyatua matofali, kuchunga mifugo, kulima, kujenga na kuchoma mkaa
karibu na miundombinu hiyo.
Akizungumza na JAIZMELA Meneja mradi wa ufufuaji wa reli
Kanda ya Kaskazini Shadrack Massawe alisema TRC inaendelea kutoa elimu kuhusu
mambo ya kuzingatia katika maeneo ya miundombinu ya reli kwa wananchi waishio
karibu na miundombinu hiyo.
Alisema kuwa wapo baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia
ya kufanya shughuli zao mbalimbali kwenye hifadhi ya reli ikiwemo ujenzi na
kilimo hivyo kuathiri miundombinu ya reli hiyo.
“Ni marufuku kwa
mwananchi yeyote kufanya shughuli zozote katika eneo la hifadhi ya reli ikiwa
ni pamoja na kuchunga mifugo, kulima, kujenga kufyatua matofali na kuchoma mkaa
hairuhusiwi,”alisema Massawe.
Katika hatua nyingine kutokana na maoni ya wakazi wengi
mkoani hapo kutaka vivuko, meneja mradi huo wa ufufuaji wa reli aliwataka
wananchi kutambua kwamba sio kila eneo linafaa kuwekwa kivuko cha barabara
kwani vivuko vingi huathiri uendeshaji wa treni.
“Tumepokea maombi mengi kutoka kwa wananchi wakiomba
wawekewe vivuko, lakini ukweli ni kwamba huwa hatuweki vivuko kila mahali,
vivuko havitakiwa kuwa vingi sana kwenye njia ya reli kwa sababu itaathiri
uendeshaji wa treni hivyo tunapenda kuwajulisha kwamba wale wote walioomba kuna
timu inapita kwenda kukagua pale walipoomba na kama wataona panakidhi vigezo
vya kuwekwa kivuko vile ambavyo vitakuwa vinakidhi tutawapatia
taarifa,”alisema.
Pia Massawe aliwaasa wananchi kuwa makini wawapo karibu
na miundombinu ya reli kwa kuepuka kukaa, kufanya biashara katika maeneo ya
reli na kuacha kutumia spika za masikioni wanapokuwa karibu na reli kwa kuwa
zinahatarisha usalama wa maisha eneo la kivuko kwa watu kushindwa kusikia honi
ya treni pindi inapopita.
“Ukifika kwenye eneo la makutano ya barabara na reli
inapaswa kutulia na kuangalia pande zote kwa umakini kabla ya kuvuka ,na kwa
wanao tumia vyombo vya moto wawe makini pindi wanaposikia treni inakuja”,
alisema.
0 Comments:
Post a Comment