Tuesday, April 14, 2020

KNCU yalirejesha Shamba la Lerongo lisiloendelezwa

Shamba za Lerongo ambalo halijaendelezwa kwa takribani miaka mitatu kutoka mwaka 2016-2020. (Picha na Kija Elias)

Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa mkoani Kilimanjaro (KNCU) limepokea shamba la Lerongo lililokuwa mikononi mwa mwekezaji ambaye hakuwa kulipa kodi  kwa takribani miaka mitatu.

Hayo yanajiri ikiwa ni baada ya kushtukia mchezo mchafu wa mwekezaji waliyempa kushindwa kulipa kodi inayofikia kiasi cha Shilingi Milioni 250.

Kaimu Meneja wa KNCU (1984) Ltd Godfrey Massawe alisema  mwekezaji Otaru Manufacturing & Trading Co. Ltd alipewa kuwekeza shmba hilo mwaka 2016 kwa makubaliano ya kuliendeleza lakini ndani ya miaka mitatu hakukuwa na mafanikio ambayo walitarajia kuyapata kutoka kwa mwekezaji huyo.

“Tangu mwaka 2016 Mwekezaji hakuwahi kulipa kodi na hivyo hadi kufikisha deni la Tsh Ml 250 , KNCU ilifikia hatua ya kutumia Wakala wa kukusanya madeni ambaye tulikuwa tukimdai mwekezaji huyo ambaye hadi kufikia Desemba 2019 KNCU ilikuwa inamdai kodi ya takriban dola za Marekani 100,900 Sawa na Tsh Ml 250 ambayo ni limbikizo la kodi ya miaka mitatu,” alisema Massawe.

Hata hivyo Massawe aliweka bayana kuwa shamba hilo la Lerongo linarejeshwa kwa mara ya pili baada ya mwekezaji mwingine mwaka 2004 kushindwa kufikia malengo waliyoingia mkataba na KNCU.

“Mwaka 2004 KNCU ilimilikisha mwekezaji  kwa ajili ya kuliendeleza kwa nyakati tofauti, na ilifika wakati mwekezaji huyo alishindwa kabisa kuliendeleza kama ambavyo mkataba ulivyomtaka  na kufanyika mashauriano mbalimbali. Ili kuhakikisha kuwa yeye anarudisha kwenye nguvu yake ya kuendeleza eneo hilo,” aliongeza.

Massawe alisema mwekezaji huyo alikuwa hajailipa KNCU ambapo alipewa notisi ya siku 30 kuanzia Desemba 27, 2019 hadi Januari 31, 2020 ili kukamilisha deni hilo na walipoona ameshindwa waliamua kulirejesha mikononi mwao kwa ajili ya kutafuta mwekezaji mwingine.

“Tupo katika hatua za kutafuta mwekezaji mwingine mwenye dhamira ya kuwekeza kwenye shamba hili ili tuweze kuendeleza zao la kahawa  na kutoa ajira kwa wananchi,” alisema Massawe

Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 541 ni miongoni mwa mashamba yanayomilikiwa na KNCU mengine ni Gararagua, Lerongo, Lyamungo na Molomo.

Kwa upande wake Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro John Henjewele, aliwataka wawekezaji wote kuhakikisha mashamba yote yanaendelezwa ipasavyo na kwamba watakwenda kwenye mashamba yote kuyakagua ili kuona kama yanaendelezwa na wale watakaoshindwa watanyang’anywa.

Henjewele aliongeza kuwa madhumuni ya mashamba hayo ni kuhakikisha kwamba mashamba yote yanaendelezwa ili kuzalisha mali, ajira kwa vijana na serikali iweze kupata kodi yake.
Afisa, Nyumba, Miradi na Mashamba ya KNCU Wilbard Lyimo



0 Comments:

Post a Comment