Halmashauri ya Wilaya ya
Rombo mkoani Kilimanjaro ipo mbioni kufufua utamaduni wa ngoma za asili ulio
hatarini kutoweka wa Iringi.
Akizungumza ofisini kwake,
Afisa Idara ya Elimu Msingi wilayani humo Alice Uforo Makule alisema katika
wilaya yake wanataka kuwa wa kwanza kuweka chachu hiyo kwa kabila la Wachagga.
Makule aliongeza kuwa
makabila mengine yamekuwa na utaratibu mzuri wa kuendeleza ngoma zao za asili
kwa kuwafundisha watoto wenye umri mdogo na kwa njia hiyo yamefanikiwa pakubwa
kutunza asili ya ngoma zao ikilinganishwa na Uchaggani ambako hakuna utaratibu
kama huo.
“Iringi ngoma hii iko
mbioni kutoweka, ukiangalia makabila mengine watoto wenye umri wa chini
wamekuwa wakijifunza ngoma zao huku Uchaggani ni mara chache sana kuona rika
hilo likijifunza,vijana hawataki kabisa,
huwezi kuwaona wakiifuatilia,” alisema Makule.
Afisa huyo aliweka bayana
kuwa wapo katika mazungumzo na Idara ya Utamaduni ya wilayani hapo kuona
uwezekano wa kufanya kwa kuanzia wanafunzi wa shule za msingi ili kuendeleza
ngoma asili ya Wachagga ya Iringi iliyo mbio kutoweka.
“Nikiangalia kwa jicho la
baadaye naona ipo mbioni kutoweka lakini kupitia kitendo cha utamaduni
tunaendelea kuwasiliana kuona jinsi gani tunaweza kufufua,” alisema Makule.
Hata hivyo aliweka bayana
kikwazo kikubwa kinachokabilia jitihada hizo ni mgawanyiko miongoni mwa
Wachagga na kuongezeka kuwa katika halmashauri ya Rombo wanaweza kufanikiwa
lakini maeneo mengine kama Machame, Marangu itapaswa jitihada kufanyika kwa
nguvu zote ili kutunza ngoma hiyo.
“Kikwazo kikubwa ni
mgawanyiko wa wachagga wenyewe kuna wachagga wa Marangu, wa Machame, wa Rombo
jitihada za makusudi zinafaa zifanyike ili kutunza ngoma hii ya Iringi,”
alisema Afisa huyo.
Kabila la kichagga ni
mkusanyiko wa makabila madogo madogo (ya Kichagga) yaliyosambaa kijiografia
kuzunguka mlima Kilimanjaro kuanzia Mashariki Tarakea, Rombo hadi magharibi ya
Kilimanjaro Siha, Machame. Makabila ya Kichagga ni Wa-Rombo, Wa-Marangu,
Wa-Kilema, Wa-Old Moshi, Wa-Kibosho, na Wa-Machame. Makundi mengine madogo ya
wachagga ni Wakirua-Vunjo, Wa-Uru, na Wa-Siha.
0 Comments:
Post a Comment