Saturday, April 4, 2020

Ron W. Davis amlilia Jean-Claude Ganga

Jean-Claude Ganga (1934-2020)
Kocha wa zamani wa riadha wa Tanzania Ron Davis ametoa masikitiko yake kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa Kamati ya Olimpiki ya Afrika (ANOCA) na mwanzilishi wa All African Games Jean-Claude Ganga aliyefariki Machi 28 mwaka huu jijini Brazzaville katika Jamhuri ya Kongo.
Akizungumza na mwandishi wa habari, Davis alisema Afrika imepoteza mtu ambaye alikuwa kiungo muhimu katika michezo yote na kuongeza kuwa mchango wake ulimfanya hata yeye aonekane katika medani ya riadha.
“Nilionana na Ganga jijini Moscow na aliyenitambulisha alikuwa Sam Ramsamy wakati huo ilikuwa ni wakati wa michuano ya Olimpiki mwaka 1980 kuanzia hapo tulianza kuwa marafiki hadi wakati tunakwenda katika michuano ya olimpiki ya Atlanta mwaka 1996. Hakika alikuwa mtu muhimu wa michezo barani Afrika,” alisema Ron Davis.
Davis aliongeza kuwa Ganga ametoweka duniani lakini kuna kazi kubwa ya kufanya ikiwamo kuenzi kile alichokianzisha na kuhakikisha kwamba mambo yanafanyika kwani michezo ndio Morali ya Watu.
“Kwangu mimi namtazama Ganga kama mtu mkubwa barani Afrika na mbeba maono ya Michezo na Siasa hapa Afrika,” aliongeza kocha huyo aliyeipatia Tanzania medali ya kwanza ya Olimpiki.
Kwa upande wake Rais wa ANOCA Mustapha Berraf katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka Abuja, Nigeria alisema, “Ni pigo kubwa katika medani ya Olimpiki ya Afrika. Rais Ganga alikuwa ni mtu mwenye hekima, alikuwa mhamasishaji na mwenye ushawishi kwa viongozi wengi wa michezo. Alifanya mengi kwa ajili ya kuhamasisha michezo na olimpiki katika bara letu, kazi zake haziwezi kuelezewa kwa maneno machache. Kwa niaba ya vyama vyote vya kitaifa vya Olimpiki hapa Afrika na kwa niaba yangu mwenyewe, ningependa kutoa rambirambi zangu kwa familia na ningeomba wazipokee. Sisi ni waja wake Mungu tulitoka kwake na Kwake tutarudi. Mungu amlaze mahala pema peponi.”
Enzi za uhai wake Ganga aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Jamhuri ya Kongo ikiwamo ya Waziri wa Michezo. Ganga atakumbukwa kwa kupambana hadi kuanzishwa na kufanyika kwa Mashindano ya All Africa Games kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1965 na yalifanyika Congo-Brazzaville. Katika taifa lake alikuwa akifahamika kama ‘Mjenzi Mkuu wa Michezo.’




0 Comments:

Post a Comment