Tuesday, April 14, 2020

Namna ya kujiponya na uraibu wa kamari

Uraibu wa Kamari sio wazo au jambo geni miongoni mwa jamii nyingi ulimwenguni hususani Tanzania. Nafahamu kuna wengi wetu kwa sasa wamekuwa waraibu wa Kamari hadi imekuwa ni maradhi yanayowatesa wengi hususani vijana.

Watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea nao wameonekana kuongezeka kwa wingi katika uraibu huu wa Kamari. Lakini kwa uchache, Uraibu wa Kamari ni hali ya kushindwa kuacha kucheza michezo ya kubahatisha.

Maambukizi ya virusi vya Covid-19 yamekuwa janga la dunia kwa sasa hali ambayo inazidi kutishia uchumi wa kila taifa. Hata hivyo kuna maisha baada ya janga hili kupita. Corona imeathiri kila taifa, sekta mbalimbali na mtu mmoja mmoja.

Kuanzia miaka ya 2013 suala ya Kamari za michezo maarufu kama Sports Betting lilianza kwa kasi hadi wakati wa kabla ya maambukizi ya Corona hayajazuia ilikuwa ni shida. Vijana wengi mamia kwa maelfu hawataki kufanya kazi wanaona fursa ipo katika kucheza Kamari hizo na nyinginezo. Kuna uwezekano mkubwa wa kupata uraibu wa Kamari katika michezo, katika mtandao na michezo mbalimbali.

DALILI ZA URAIBU WA KAMARI

Watu ambao wamekumbwa na matatizo ya kamri walianza na tabia ya kudanganya na baadaye kujificha au kukaa mbali na familia zao, marafiki na wengine wanaowazunguka. 

Pia watu walioingia katika Kamari walianza michezo hiyo kwa kupoteza kwa maana kila wanapocheza wanaliwa. Sasa waliendelea kutumia zaidi pesa, wakiwa na matumaini siku moja wataweza kushinda na kuibuka na kitita kikubwa cha fedha.

Lakini wakiwa na matumaini hayo wamejikuta wakiwa na madeni yasiyoisha hali ambayo imewaletea matatizo. Hata hivyo matatizo ya kamari hizi huwafanya watu wa jinsi hiyo kuwa ni watu wa kukopa.

Kama ilivyo kwa wenye uraibu wa pombe na dawa za kulevya, mtu mwenye uraibu wa Kamari atazidi kutafuta namna ya kuufurahisha moyo wake kwa kuendelea kubeti au kucheza hiyo Kamari.

Wengi wa wacheza Kamari inawawia vigumu kuachana nayo bila kujali ni kwa kiasi gani wanataka. Endapo watajaribu kujitoa wanawaza kwamba watapata matatizo mengine ya upweke na mawazo. Kwa waraibu wa Kamari wanaishia kuharibu maisha yao ya kijamii, kiuchumi na kitaaluma.
NAMNA YA KUTIBU URAIBU WA KAMARI

Katika mambo yote chini ya jua hakuna kinachoshindikana. Hivyo hata hili lina mlango wa kutokea kwa waraibu wote. Zifuatazo ni mbinu za kupambana na changamoto hii ya uraibu wa Kamari.

Mosi, Kukubali. Kama ilivyo katika uraibu mwingine hatua ya kwanza katika kuponya kabisa ni kukubali kwamba una changamoto ya uraibu wa Kamari. Ukishindwa hapo hakuna tena dawa kwani hata njia nyingine hazipenya na kuleta muarobaini wa uraibu huo. Wengi waliposhindwa kukubaliana na changamoto hiyo hakuna kilichofanikiwa na hatimaye wakateketea kabisa.

Pili, Pata usaidizi. Katika maisha tunayoishi huwezi kuwa peke yako katika changamoto zako. Ndio kuna wengine wamefanikiwa lakini kwa asilimia ndogo. Usaidizi kutoka kwa watu wako wa karibu ikiwamo familia inaweza kukusaidia kurudi katika hali nzuri na ukaendelea na ujenzi wa taifa.

Tatu, Tafuta mbadala wa Kamari. Unapaswa kujiepusha na kukaa katika maeneo ambayo shughuli za uchezaji wa Kamari zinafanyika. Unaweza kutafuta shughuli nyingine ya kufanya kama kukimbia au kufanya michezo mingine kama kuogelea na hibi nyingine unazozipenda nje ya Kamari. Lakini katika uchaguzi wa hobi hizo chagua zilizo chanya usijiingize katika zile ambazo zipo kinyume.

Nne, Jiepushe na marafiki wako wa zamani mliokuwa mnacheza wote Kamari itakusaidia. Marafiki wana sehemu kubwa mno ya kuathiri tabia zako hivyo uapojiepusha nao na kuwa na marafiki wapya inakusaidia na uraibu huishia hapo. Ukitaka kufanikiwa kuwa karibu na marafiki waliofanikiwa usipende kujifunza au kuwa na marafiki walioshindwa, watakuchelewesha kukifikia malengo yako ya kuondoka na uraibu wa Kamari.

Tano, Tafuta usaidizi wa Kitaalamu. Uraibu wa Kamari umebeba pia masuala ya kiafya. Hivyo tafuta wataalamu wa afya wataweza kukupa ushauri nasaha wakiwamo wataalamu wa saikolojia. Kwa kufanya hivyo haurudi tena katika uraibu huo na utakuwa mjenzi mzuri wa taifa lako.

Kipindi hiki cha makabiliano dhidi ya Corona inaweza ikawa ndio wakati mzuri kwa uliye mraibu wa Kamari kujitafakari na kutambua kuwa unaweza kurudi katika hali yako nzuri ya zamani kabla hujaanza kucheza Kamari.

0 Comments:

Post a Comment