Diwani wa Kata ya Kilimanjaro Priscus Tarimo |
Imeelezwa kikwazo kikubwa katika kuifanya Moshi ya Kijani ni usimamizi wa zoezi zima la upandaji wa miti katika mitaa ya Manispaa hiyo.
Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali inayojishughulisha na Utunzaji wa Mazingira mjini Moshi (Moshi Green Campaign) Priscus Tarimo wakati wa zoezi la ugawaji wa miti kwa wenyeviti wa mitaa ya Shiri-Matunda na Mjohoroni alisema kampeni ya ugawaji wa miti imekuwa ikifanyika mara kwa mara lakini inakabiliwa na changamoto ya usimamizi katika utunzaji wa miti hiyo.
“Wananchi wengi waishio maeneo ya vijijini wanategemea sana kuni kwa ajili ya kupikia, hivyo wawekezaji wa gesi wanatakiwa kujikita zaidi kupeleka huduma hiyo vijijini, lakini katika upandaji wa miti tunakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa hiyo miti tunayowapa ili wakaipanda kwani hadi sasa kwa takribani miaka mitatu tumetoa miti 30000,” alisema Tarimo.
Tarimo alisema viongozi wa serikali za mitaa wamekuwa nyuma katika kuhakikisha miti hii inasimama na kwa kufanya hivyo watakuwa wamefikia malengo ya kuifanya Moshi ya Kijani.
“Wenyeviti vya serikali za mitaa ndio nguzo yetu kubwa katika kuifanya Moshi ya Kijani, lakini kinachotokea ni usimamizi hafifu hali ambayo imekuwa ikisababisha miti kufa na malengo ya kampeni kwenda kwa mwendo wa pole kuliko vile tunavyotaka,” alisema Tarimo.
Hata hivyo Tarimo aliongeza kuwa wanaendelea kutoa elimu kuhusu namna ya utunzaji wa miti hiyo ambayo wanapewa ikiwamo namna ya kuitunza wakati wa kiangazi kikali kwa kutumia mbinu mbadala zenye faida na zisizotumia nguvu nyingi.
“Tumekuwa tukiwaelekeza namna ya kunyeshea miti wakati wa kiangazi kwa mfano kuna ile ya kutumia mabobo (chupa za plastiki) na kufunga na sponji kasha kutoboa tundu na kujaza maji na kulifunga pembezoni mwa mti ambapo lita moja inaweza kukaa siku tatu na mti hautaweza kufa kwa namna hiyo,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimanjaro Gudila Kimboka ambaye ni Katibu wa Kampeni ya Moshi ya Kijani alisema kwa mwaka huu wamefanikiwa kugawa miti zaidi ya 4,000 katika mitaa mbalimbali mjini hapo huku wakitarajia kuongeza mingine 2,000.
“Miti mbalimbali tumefanikiwa kugawa kwa wenyeviti wa mitaa ambao watapanda na kusimamia hadi kukua kwake kwani madhumuni makubwa ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa hali ambayo itasaidia utunzaji wa mazingira kwa ujumla,” alisema Kimboka.
Pia Kimboka alisema miaka ya zamani kabla ya 1980 hali ya mvua mkoani Kilimanjaro ilikuwa ikinyesha bila kusuasua kama ilivyo miaka ya hivi karibuni na joto lililikuwa kiasi tofauti na ilivyosasa.
Kwa upande wake Afisa Mazingira Mkoa wa Kilimanjaro, Emanuel kiyengi, aliwataka viongozi wa Wilaya za Kilimanjaro, kulinda misitu iliyopo kwenye maeneo yao ili kurudisha asili ya Mkoa wa Kilimanjaro kwenye hali ya kijani.
Kauli Mbiu ya kuifanya Moshi ya Kijani ni “Panda mti leo kwa ajili ya kumbukumbu ya Kesho.”
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
STORY BY: Kija Elias & Jabir Johnson
ALL PHOTOS BY: Jabir Johnson
DATE: Aprili 21, 2020
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimanjaro Gudila Kimboka na Diwani wa kata hiyo Priscus Tarimo wakikagua miti kwa ajili ya kugawa kwa wananchi ili iweze kupandwa. |
0 Comments:
Post a Comment