Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira amewataka
wakurugenzi wa halmashauri mkoani humo kutunga sheria ndogondogo ambazo
zitatumika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Corona ikiwamo kupulizia dawa
bodaboda na mabasi kila siku katika halmashauri husika.
Mghwira aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa
habari jana wakati akitangaza kifo cha mtu mmoja aliyepoteza maisha kwa ugonjwa
wa Corona katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mkoani humo.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema ni halmashauri moja pekee ya
Moshi Mjini ambayo imejitahidi kupulizia dawa katika vyombo vya usafiri ikiwa
ni kuunga mkono juhudi za kudhibiti maambukizo hayo.
“Serikali imeweka nguvu kubwa katika stendi kuu ya mabasi mjini
Moshi, magari yote yanapuliziwa wakati wa usiku na kuanza safari alfajiri
isipokuwa huko yanakotoka kuja Moshi hayapewi huduma hiyo hali ambao ni kikwazo
katika udhibiti wa huo. Mwarobaini wa hilo ni wakurugenzi wa halmashauri
nyingine kutunga sheria ndogondogo ili kuvibana vyombo hivyo vya usafiri
kupulizia dawa,” alisema Dkt. Mghwira.
Mbali na hilo Dkt. Mghwira aliwataka wamiliki wa maeneo ya
starehe mjini Moshi ikiwamo Moshi Pazuri na Hugos Pub kufika ofisini kwake
kujieleza ni sababu zipi zinazowafanya kuendelea kukusanya watu katika maeneo
hayo katika kipindi hiki cha udhibiti wa maambukizi ya Corona.
“Moshi Pazuri, Hugos Pub bado yanaendelea kujaza watu sasa
nawataka wamiliki wa maeneo hayo kufika haraka ofisini kwangu kujieleza,”
alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
0 Comments:
Post a Comment