Jumla ya nyumba 30, bajaji
sita, gari moja, na mifugo ambayo idadi yake haijafahamika mara moja imesombwa
na maji katika kata ya Mji Mpya mjini Moshi kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha tangu juzi.
Aidha mvua hizo zimesomba
pikipiki zaidi ya 20 ambazo ni za wakazi wa kata hiyo ambayo imeathirika zaidi
na mvua za siku tatu katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza katika eneo la
tukio diwani wa kata ya Mji Mpya Abuu Shayo alisema idadi hiyo inaweza kuzidi
kutokana na mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha mkoani hapo.
“Ni kweli mvua zimeanza kunyesha
tangu majuzi, zinatokea ukanda wa juu nyumba zaidi ya 30, magari, bajaji na
miundombinu imesombwa na mvua, mifugo kama nguruwe, bata, kuku,” alisema Shayo.
Shayo aliweka bayana kutoka
siku ya kwanza ya mvua hizo ambazo zilianza kuathiri mtaa wa Kwa Komba ambako
nyumba sita zilianza kusomba na maji
alikwenda kwa mkuu wa wilaya ya Moshi Kippi Warioba kuhusu hali hiyo
lakini hakuridhishwa na majibu ya mkuu huyo wa wilaya.
“Juzi nimekwenda kwa mkuu
wa wilaya, hakunisikiliza ningeomba wakati tunapofika kuwapa taarifa
watusikilize kwa haraka kiukweli nimekwazika jibu alilonipa kama ni suala la
mafuriko nalijua sasa kulijua kwenyewe ndio huo leo ni maafa makubwa,” aliongeza
diwani huyo
Hata hivyo diwani huyo
aliitaka serikali kuchukua hatua za haraka kwani utabiri wa mvua hizi ulitolewa
na mamlaka ya hali ya hewa tangu awali kuwa msimu wa masika ungekuwa na mvua
nyingi ambazo zinaweza kuleta maafa.
“Serikali ichukue hatua
kunusuru maisha ya watu hawa kwani ndio mwanzo tu wa mvua za masika,” alisema.
Usiku wa kuamkia Aprili 21
mwaka huu watu wa kata ya Mji Mpya na Msaranga walijikuta katika kipindi kigumu
baada ya mvua hizo zilizoendelea kunyesha hadi usiku wa manane kuzoa mali za
wakazi hao.
Jeshi la Polisi, Jeshi la
Zimamoto zilionyesha ushirikiano mkubwa baada ya kupokea taarifa za maafa hayo
ambapo lilikwenda na kutoa msaada wa kuwatoa watu waliokuwa wamepanda katika
miti na mapaa ya nyumba kunusuru maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti waathirika wa mvua hizo baadhi yao walisema kwa mara ya mwisho kuziona
ilikuwa ni mwaka 1960 na kuongeza kuwa serikali iwasaidie kwa sasa mahali pa
kujihifadhi.
Kwa upande Mkuu wa Wilaya ya
Moshi Kippi Warioba alisema serikali imeunda timu ya wataalamu wa afya kwa
kushirikiana na Msalaba Mwekundu ili kuangalia wahitaji na kufanya tathmini ya
waathirika wa maafa hayo.
“Ni kweli kuna makazi,
vifaa vimesombwa na maji hivyo kupitia wataalamu wataweza kuleta taarifa ili
waweze kuwasaidia ikiwamo ni pamoja na kuwatafutia makazi kwa waathirika wa
maafa haya,” alisema Warioba.
0 Comments:
Post a Comment