Tuesday, March 24, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Johan Cruyff ni nani?

Machi 24, 2016 alifariki mwanasoka wa kimataifa wa Uholanzi Johan Cruyff akiwa na umri wa miaka 68. Alhamisi ya Machi 24, mkongwe huyo alishindwa vita na Saratani, lakini mfumo wake wa kipekee utakumbukwa milele, na soka lenyewe kwa kiasi kikubwa linamshukuru sana Johan Cruyff. (1947-2016)

Cruyff alikuwa mbunifu, mwana mitindo, mwelimishaji, mchezaji soka mahiri, kocha bora, mwanafalsafa na kila sifa katika soka la ulimwengu wa kisasa. 

Cruyff aliondoka lakini timu aliyoisaidia kutawala soka la dunia na penalti yake maarufu ya pasi aliyopiga 1982 ilirudiwa tena na Lionel Messi na Luis Suarez.

Alikula Ini la Ng'ombe, lakini kazi zake zitadumu milele. Johan Cruyff alibadili soka: kama mchezaji, kocha, mshauri na moja wa wanazuoni wakubwa wa soka, Mdachi huyu ameacha urithi utakaodumu siku zote. Alifanya mageuzi ya soka katika zama za kileo.

Cruyff alipenda kuwa tofauti. Alilenga kufanikiwa kama mchezaji mdogo kwani baba yake alifariki akiwa mdogo sana, Johan akiwa mdogo (akifahamika kwa jina la kuzaliwa Hendrik Johannes) alikuza ujuzi wake na kuwa mchezaji mahiri.

Mama yake alifanya kazi kama mfanya usafi wa Ajax na baba yake wa kambo alikuwa mfanya kazi wa klabu ya Amsterdam. Hivyo Cruyff alijifunza thamani ya kufanya kazi kwa bidii akiwa na umri mdogo na alikuwa akivifanyia kazi kwa juhudi nyingi vipaji vyake, alijiunga na akademi ya Ajax na akawa mchezaji bora zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Cruyff aliiongoza Ajax kutwaa vikombe vitatu vya Kombe la Ulaya na alitwaa tuzo ya Ballon d'Or mara tatu pia. Chini ya mwana mapinduzi Rinus Michels, Johan alikuwa mchezaji hatari zaidi wa kipindi chake. Total Football Na kwa pamoja wawili hao waliiongoza Uholanzi kutinga fainali ya Kombe la Dunia 1974 - ambapo waliishia kufungwa na Ujerumani Magharibi mjini Munich.
Licha ya kipigo hicho, walikonga nyoyo za mashabiki wote wa soka duniani kwa uchezaji wao kushirikiana.

"Tumepoteza moja ya mchezo muhimu sana katika maisha yetu, lakini nadhani hilo limetupatia umaarufu ambao huenda tusingeupata kama tungekuwa tumeshinda," alisema baadaye. "Kwa sababu watu walitaka tushinde, jambo hilo lilivuta usikivu wa wengi, na upendo. Kwa muda wa majuma manne katika michuano hii hakuna aliyekuwa akizungumzia kushinda ama kufungwa - hadhira ya ulimengu ilitaka kuona kandanda safi likichezwa. Kwa hiyo si kwamba tunajitetea, ni kweli - matokeo ya fainali hayaniumizi sana."

Uholanzi walipoteza fainali ya 1978 pia, lakini kipindi hiki Cruyff hakuwepo. Aliamua kuyakosa mashindano kwa sababu zake binafsi; lakini alikuwa akijiandaa kwa ajili ya sehemu yake mpya : Barcelona. 

Ajax walitaka kumuuza kiungo huyo Real Madrid, lakini Cruyff alikuwa na mtazamo tofauti.
"Nakumbuka safari yangu kwenda Hispania ilikuwa na mikingamo mingi," alisema. Watu walisema nilikuwa nikienda kwenye nchi ya kifashisti. Rais wa Ajax alitaka kuniuza Real Madrid. Lakini nilizaliwa muda mfupi tu baada ya vita na nilifundishwa kutokukubali mambo kiholela. Barcelona hawakuwa katika kiwango walichokuwa nacho Real Madrid kisoka, lakini ilikuwa ni changamoto kuichezea klabu ya Catalan, Barcelona ilikuwa zaidi ya klabu."

Na ikiwa na Cruyff ilikuwa klabu kubwa zaidi. Mwaka wake wa kwanza Camp Nou ulikuwa mzuri kwani walishinda ubingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza tangu 1960, wakiifunga Real Madrid 5-0 msimu huo na kuweka alama yao iliyodumu hadi hivi leo.

Kipindi chake chote alichodumu Katalunya hakikuwa na mafanikio sana, lakini alikuwa mshauri wa rais Josep Lluis Nunez kabla ya kuondoka. Cruyff alimtaka mkurugenzi wa klabu kuunda akademi yenye mfumo wa Ajax na kukuza wachezaji wenye vipaji kama yeye alivyotokea Amsterdam. Aliamini wakifanya hivyo wangeweza kushindana vizuri na Real Madrid.

Mara nyingi Cruyff alikuwa akienda Marekani, akarejea tena La Liga akiwa na Levante na aliiongoza Feyenoord kutwaa taji katika nchi yake ya nyumbani.  

Aliporejea Barcelona kuendelea na kazi ya ukocha aliyoianza kwa mafanikio Ajax, kilikuwa tena ni kipindi cha utawala wa Real Madrid. Cruyff aliwasili mnamo 1988, Nunez aliamini kumrejesha mdachi huyo kungebadili mambo yote -  na alikuwa sahihi.

Ilichukua muda lakini wachezaji wadogo walikuwa wakitokea kwenye timu ya vijana na Cruyff aliwaunganisha na wachezaji bora wa dunia. Timu ya ndoto ya wengi ilizaliwa, ikashinda taji la La Liga mfululizo kati ya mwaka 1991 na 1994, hali kadhalika na Kombe la Ulaya. Ghafla Barca hawakuwa chini ya kivuli cha Madrid tena.

Wiki moja baada ya kurejea klabuni, Cruyff alikwenda kuangalia timu ya vijana, akamwona kinda Pep Guardiola akicheza kama kiungo wa kulia. Alimtaka mchezaji mwenzake wa zamani Carles Rexach kumuingiza Pep kati kipindi cha pili ili acheze sehemu muhimu zaidi. Aliimudu nafasi hiyo mara moja na punde akaingizwa kwenye kikosi cha kwanza.

Guardiola alikuwa kocha wa Cruyff dimbani na Pep alizivuta nyuzi vilivyo katika timu iliyokuwa imesheheni vipaji kipindi hicho, ilikuwa ni Barca yenye mafanikio mno katika historia.

Baadaye katika utawala wake, Cruyff aliungua shinikizo la moyo na alishauriwa kuacha kazi ya ukocha na daktari wake. Alipoondoka 1996, hakufanya kazi nyingine lakini bado alikuwa na ushawishi.

Akirejea tena kama mshauri wa Joan Laporta, alipendekeza kuteuliwa kwa Frank Rijkaard mnamo 2003. Kwa mara nyingine tena Barca walipata mafanikio, wakitwaa mataji ya ligi na Ligi ya Mabingwa Uefa 2006.

Lakini tena bado kulikuwa na mengi zaidi. Baada ya kushindwa kufanya vizuri kwa kiwango fulani, Laporta aliponea tundu la sindano na kikosi kilihitaji kuimarishwa tena. Rijkaard aliondoka klabuni, ingawa Jose Mourinho alikuwa akitamani kibarua hicho Camp Nou, Cruyff alimchagua Guardiola.

Wengi walimsonda kidole kwa kudai kuwa hana uzoefu wa kazi ya ukocha, lakini Mdachi alisema: "Kipimo kikubwa kwa kocha katika timu kama Barca ni nguvu ya kufanya maamuzi na uwezo wa kuzungumza kwenye vyombo vya habari, kwa sababu huo ndio uongozi. Baada ya hapo ni rahisi kwa wale wanaojua soka. Lakini si wengi wanaofahamu." 

Mnamo mwaka 2009 wakati akihojiwa na Goal.com Cruyff aliwahi kusema, "Watoto wanahitaji msaada kutoka kwetu"

Nyota huyo aliongeza,"Nilijielimisha mwenyewe mitaani. Niliendesha baiskeli, nilicheza soka, nilikimbia nikifanya kila kilichowezekana, lakini leo nipo kwenye gari na hakuna sehemu ya kucheza mtaani. Hivyo inabidi nibuni kitu kingine tofauti. Mwili unaozaliwa nao ndio unaokufa nao. Naam unaweza kubadili mambo machache lakini si kila kitu. Leo magari, kompyuta na mtandao wa intaneti na kila kitu mazoezi ya viungo hayana nafasi tena na soka pekee ndilo linaloweza kukupa mazoezi."
Johan (Hendrik Johannes) Cruyff, mwanasoka huyo mahiri alizaliwa Aprili 25, 1947.

0 Comments:

Post a Comment