Sunday, March 22, 2020

Covid-19: Ali Baba Ramadhani aendelea na mazoezi

Mwanamasumbwi wa Kilimanjaro Alibaba Ramadhani amesema licha ya kitisho cha virusi vya Covid-19 kwa sasa duniani lakini mazoezi yake kuelekea pambano lake dhidi ya bondia wa Tanga hayajasimama.

Akizungumza wakati wa mazoezi yake kuelekea pambano lake dhidi ya Shafii wa Tanga, Alibaba alisema, "Ni kweli Corona inatisha lakini najitahidi kuchukua tahadhari zote lakini siwezi kuacha mazoezi nataka nipambane na huyo dogo (Shafii)."

Aidha kauli ya Alibaba inakwenda sambamba na wito uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alioutoa jana wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu la Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma akiwataka watanzania kuendelea kuchapa kazi na kujenga uchumi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga kuambukizwa ugonjwa huo kama zinavyotolewa na wataalamu.

Alibaba alisema pambano lake la uzito wa Light Middle lilitakiwa kufanyika Aprili 12 mwaka huu lakini bado promota wake hayatoa ratiba nyingine ama ya kuahirisha au la licha ya kitisho cha Corona.

Mwanamasumbwi huyo mwenye umri wa miaka 42 atapambana ulingoni dhidi ya Shafii wa Tanga mwenye umri wa miaka 24 katika uzito wa Light Middle litakalofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati wowote zuio la Covid-19 litakapoondolewa.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu umri wake na wa mpinzani wake kama ataweza au la, Alibaba alisema, "Ninaamini katika fitness (uimara), ishu ya umri sio sana kwani mpaka sasa nimejipima kuwa ninaweza dhidi ya huyo dogo, na kitisho hiki cha Corona ndio kinanipa morali zaidi ya kujiweka fit zaidi, nikampe dawa yake."

Kwa mujibu wa Fightsrec ya nchini Marekani hadi sasa Ali Ramadhani amepanda ulingoni katika mapambano ya kimataifa 25, akishinda 12 na kupoteza 13. Mapambano hayo aliyacheza kati ya mwaka 2003 na 2015. Nyota huyo alizaliwa Machi 23, 1977.

STORY & PHOTO BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
DATE: Machi 21, 2020

0 Comments:

Post a Comment