Machi 19, 2017 alifariki dunia mwandishi wa habari wa Marekani Jimmy Breslin. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 kwa kichomi (pneumonia) akiwa nyumbani kwake Manhattan.
Breslin alizaliwa Oktoba 17, 1928 Jamaica jijini New York kwa baba yake aliyekuwa mlevi na mpiga kinanda James Earl Breslin na mama yake Frances Curtin aliyekuwa mwalimu na mtafiti wa Idara ya Ustawi ya Jiji la New York wakati wa Anguko Kuu la Kiuchumi la mwaka 1929 hadi 1933.
Inaelezwa kuwa siku moja baba yake alikwenda kununua vitu dukani kwa ajili ya wanaye lakini hakurudi tena nyumbani hapo.
Hivyo Breslin na dada yake walilelewa na mama yao. Breslin alifanikiwa kusoma ambapo alihudhuria masomo ya Chuo Kikuu cha Long Island kutoka mwaka 1948 hadi 1950 lakini aliondoka chuoni hapo bila ya kufanya mtihani wa mwisho.
Breslin alianza kufanya kazi na Long Island Press kama kijana wa kuchapisha magazeti miaka ya 1940.
Baada ya kutoka chuo, alipata nafasi ya kuandika katika gazeti.
Kazi zake za mapema kabisa katika ukurasa wake zilihusu wanasiasa na watu wa kawaida huko Queens Borough Hall.
Pia aliwahi kufanya kazi ya kuandika katika magazeti ya New York Herald Tribune, aily News, New York Journal American, Newsday, Daily Beast, National Police Gazette.
Mnamo mwaka 1962 mhariri wa gazeti wa New York wakati huo Clay Felker alimwigiza katika toleo la Jumapili ambako Breslin aling'ara huko kwani ukurasa wake uliongoza kwa kufuatiliwa na wengi jijini hapo.
Miongoni mwa kazi zake kubwa alizowahi kuzifanya ni ile ya siku moja baada ya mazishi ya Rais wa Marekani John Fitzegerald Kennedy ambapo Breslin alijikita katika mchimbaji wa kaburi la kumzika JFK.
Mnamo Mei 1990 akiwa na gazeti la Newsday mwandishi mwenzake wa makala Ji-Yeon Mary Yuh alimwandika Breslin kuwa ni mbaguzi wa rangi na mnyanyasaji wa kingono.
Hali hiyo ilimletea shida kazini hapo hali iliyomfanya Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo Anthony Marro kumsimamisha kazi kwa majuma mawili.
Hata hivyo baadaye aliomba radhi kwa kitendo hicho. Awali kabla hajasimamishwa kazi Breslin alionekana katika Kipindi cha Howard Stern akijibu kuhusu yaliyoandikwa katika makala na kufukuzwa kwake kwa Wakorea.
Hali hiyo ilimchanganya zaidi mhariri wake ambaye aliamua kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.
Breslin alioa mara mbili katika maisha yake. Mke wake wa kwanza alifahamika kwa jina la Rosemary Dattolico aliyefariki mwaka 1981.
Akiwa na Rosemary walizaa naye watoto sita Kevin, James, Patrick, Christopher, Rosemary na Kelly.
Binti yake Rosemary alifariki dunia Juni 14, 2004 kutokana na damu kuwa kidogo. Pia Kelly naye alifariki dunia akiwa na miaka 44 mnamo Aprili 21, 2009 siku nne baada ya kupata mshtuko wa moyo jijini New York ambao ulisababisha mapigo ya moyo kwenda visivyo.
Baada ya kifo cha mkewe mnamo mwaka 1982 alimwoa mjumbe wa zamani wa Baraza la Jiji la New York Ronnie Elridge ambaye alikaa naye hadi kifo chake.
Siku chake kabla ya kifo chake Breslin alihojiwa na Pete Hamill kwa ajili ya Makala ya HBO Breslin and Hamill: Deadline Artists. Enzi za uhai wake aliandika kazi nyingi na vitabu zaidi ya 20.
Mnamo mwaka 1986 alitunukiwa tuzo ya Pulitzer ambayo hutolewa katika medani ya Uandishi wa Habari uliotukuka.
0 Comments:
Post a Comment