Saturday, March 7, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Mt. Thomas Aquinas ni nani?


Machi 7, 1274 alifariki dunia mwanafalsafa, kiongozi wa dini na daktari wa kanisa raia wa Italia Mt. Thomas Aquinas kwa Kiitaliano alifahamika kwa jina la Tommas d'Aquino.

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 49 huko Abbazia di Fossanova, Fossanova Abbey, katika ardhi ya Italia. Mt. Thomas Aquino alikuwa mwanafalsafa mwenye ushawishi mkubwa, mwanatheolojia na mpenda haki akiwa chini ya mwavuli wa asili wa Uskolastika.

Alikuwa akifahamika na wengi kama Daktari Angelicus au wakati mwingine alifahamika kama Daktari Communis. Miongoni mwa nukuu zake muhimu ilikuwa "The things that we love tell us what we are." ikiwa na maana Vitu tunavyovipenda huwa vinatuambia jinsi tulivyo."

Mafaniko makubwa enzi zake katika masuala ya falsafa ilikuwa ni kuwa aliweka pamoja usanisi (synthesis) usiotikisika, mang'amuzi yaliyokuwemo kwenye kazi za kiwango cha juu sana za kifalsafa za Wagiriki (Wayunani) na Warumi na theolojia ya Kikristo.

Zaidi ya hayo Aquino hasa hasa alikristisha (christianised) falsafa ya Aristotle. Ingawa maelekeo yake ya falsafa talitawaliwa na misingi ya falsafa za Aristotle, lakini Aquino alitambua vilevile uwepo wa mawazo mazito na yenye mpangilio safi yaliyokuwa yameandikwa na watu wa kale, mababa wa kanisa na waandishi wa awali wa enzi za kati wakiwemo wanafalsafa au waandishi wa kiarabu na kiyahudi.

Itakumbukwa kwamba kutoka karne ya saba mpaka ya kumi na tatu wakati wa zama za kati katika falsafa kulikuwa na aina mbalimbali za maendeleo. Uwingi wa maendeleo hayo ulisababisha kuibuka kwa utofauti na ubishano kati ya wafuasi wa mfumo wa kufikiri wa Plato na wale wa mfumo wa kufikiri wa Aristotle.

Ubishani uliendelea hata baada ya karne ya 13  ukichukua sura ya ubishano wa Agustino na wale wa Aquino. Kila mmoja wa wanatheolojia hao walijenga hoja zao chini ya mfumo wa kifalsfa ama wa Plato au Aristotle.

Kwa hiyo kazi zote za Aquino zilitoa shinikizo lenye mvuto wa kiushawishi kwa kuweka bayana na kwa ufikiriko wa hali ya juu maswali ambayo yalihusisha matatizo hayo huku akiheshimu fumbuzi au mapendekezo yaliyotolewa na mamlaka mbalimbali.

Wakati huo huo aliyajibu maswali ya msingi yaliyokuwa yanampinga kuhusu utumiaji wake wa mfumo fikara wa Aristotle kwa kuulezea ukristo kiakili: Kwa namna hii, Aquino aliufikisha kwenye kiwango cha juu kabisa mfumo wa ujenzi wa hoja wa 'Scholastic'.

Hii ndio ilikuja kuzaa kile kinachofahamika kama Uskolastika ambao ulitokana na shughuli za kiakili au kifikara zilizokuwa zikifanyika katika shule zilizokuwa za kikanisa  na wahusika wa Uskolastika walikuwa wakifahamika kama madktari au wanafikara wakuu katika shule za kanisa hasa Katoliki.

Aquino kupitia Uskolastika aliainisha mfumo tawala wa kufikiri au kuongoza mjadala na hoja uliokuzwa na madaktari wau wasomi wakuu katika mashule na ulikuwa ni mfumo maalum walioutumia katika kufundisha falsafa.

Falsafa ya Scholastic kwa hiyo, iliibuka kama jaribio la kuweka pamoja mfumo maalum unaoambatana , shikamana, au fungamana na mawazo ya kimapokeo kuliko kutafuta kwa moyo mang'amuzi makuu yawezayo kupatikana.

Kikubwa zaidi Aquino alichokifanya katika mfumo huo ni ule mfumo ambao ulitegemea unyambulisho mantiki (logical deduction) katika uendeshaji wa hoja zake ambapo hoja sahihi  huja kwa kufuata taratibu na misingi maalum za ujengaji wa hoja hiyo.

Thomas Aquinas alizaliwa Januari 28, 1225 huko Roccasecca karibu na Naples. Baba yake alikuwa ni lodi wa Aquino. Baba yake alifikiri au alitarajia kuwa mtoto wake angekuwa siku moja amepata nafasi ya juu katika utawala wa kanisa.

Kwasababu hii Thomas alipelekwa kwenye utawa huko Monte Cassino akiwa kija wa umri wa miaka mitano. Na miaka tisa iliyofuata, alichukua masomo yake katika Utawa wa Wabenediktino. Akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na Chuo Kikuu cha Naples.

Lakini akiwa katika jiji hilo alivutiwa zaidi na maisha ya baadhi ya Watawa wa Kidominikani ambao walikuwa wanaishi katika nyumba ya kitawa iliyokuwepo karibu na shule aliyokuwa anasoma. Mvuto huo ulimfanya Thomas aamue kujiunga na Utawa wa Wadominikani.

Kwa vile wadominikani walijihusisha na hasa na kufundisha, Thomas baada ya kujiunga nao katika huo utawa, aliamua kwa moyo wote kujitoa mwenyewe katika maisha ya kitawa na ufundishaji.

Miaka minne baadaye mnamo mwaka 1245 alijiunga na Chuo Kikuu cha Paris ambapo alikutana na mwanataaluma wa ajabu (prodigious scholar) ambaye mafanikio yake makubwa ya kifikara yalimpatia jina la Albert the Great (Albertus Magnus) na mwalimu wa dunia. 

Huyu Albertus Magnus alitoa mvuto wa kiushawishi  kwa kiasi kikubwa kwa Thomas Aquino. Katika kipindi chote cha uhusiano wa karibu sana na Albert kote Paris na Cologne akili ya Thomas ilitengenezwa na kuwa yenye ukali ukali wa ajabu, ukali uliosababishwa na aina mbalimbali za mafundisho ya Albert na mitazamo yake juu ya matatizo mbalimbali ya kitaaluma. Albert alikuwa ameona na kutambua umuhimu wa falsafa na sayansi katika kutengeneza msingi wa imani ya kikristo na kwa kukuza uwezo wa akili ya binadamu.

Wakati wanatheolojia wengine waliiangalia taalum ya masomo ya kidunia kichongo chongo au katika mtazamo wa mashaka mashaka mashaka. Albert alihitimisha kuwa wanafikara wa kikristo ni lazima wawe na ujuzi wa kutosha wa falsafa na mafundisho ya kisayansi katika nyanja zote.

Kwa mantiki hii, akili yake ilijua mambo mengi sana ya kielimu zaidi kuliko ya kiuibuaji wa fikara mpya. Albert alimwona Aristotle kama mwanafalsafa mashuhuri kuliko wanafalsafa wote. Hivyo ilikuwa ni kitu kisichoepukika, chini ya mazingira ya aina hii kuwa, mwanafunzi wake Thomas Aquino angeona vilevile katika Aristotle, mawazo yenye ubora wa juu sana na yenye nguvu ya kujenga msingi imara ya theolojia ya kikiristo.

Baada ya kipindi cha muda fulani wa kufundisha chini ya himaya ya Papal Court kutoka mwaka 1259 hadi 1268, Thomas alirudi tena Paris na alikwenda kujihusisha katika ubishano mkubwa wa wafuasi wa fikara za Averroes.

Katika mwaka 1274, Papa Gregori X alimwita Thomas Aquino kwenda Lyons kushiriki katika mtaguso, na akiwa njiani kuelekea huko alifariki dunia katika monasteri iliyokuwepo kati ya Naples na Roma akiwa na umri wa miaka 49. Thomas Aquino aliacha kumbukumbu kubwa sana.

Aliacha maandiko ambayo yamepata umamlaka mkubwa mno.

Kazi zake zinawaacha watu wengi kwenye mshangao hasa pale kazi zake zote alizoziandika ambazo ni kubwa ajabu alizifanya kwa kipindi cha miaka 20 tu.

Hata hivyo kuna kazi kubwa mbili ambazo zinamfanya Thomas Aquino aonekanae mtu wa pekee katika ulimwengu wa kisomi na kitaaluma nazo ni 'Suma Contra Gentiles' na 'Suma Theologica'.




0 Comments:

Post a Comment