Tuesday, March 31, 2020

Watoa huduma kwa jamii hatarini kueneza Covid-19


Afisa Afya wa Mkoa wa Kilimanjaro Jonas Mcharo
 Watoa huduma katika taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali wapo hatarini kueneza maambukizi ya virusi vya Covid-19 endapo hawatazingatia tahadhari kuhusu ugonjwa wa Corona.

Hayo yalibainishwa na Afisa Afya wa Mkoa wa Kilimanjaro Jonas Mcharo, wakati akizungumza kwenye semina ya siku nne inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa na  kuwashirikisha Wataalamu wa Afya na Waandishi wa habari mkoani humo.

Mcharo alisema kumekuwa na tahadhari mbalimbali za kuchukua ikiwamo uvaaji wa mask na gloves ikiwa ni sehemu ya kujikinga lakini zote hazijathibitisha kitaalamu kama zinaweza kupunguza maambukizi ya kusambaa kwa virusi vya Covid-19.

“Kunawa mikono kwa sanitizers ndiko ambako Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha uvaaji huu wa mask na gloves bado haujathibitishwa kwani virusi hawa wanaambukiza kwa kasi kupitia kugusa na ndio sababu tunasisitiza kunawa mikono,” alisema Mcharo.

“Wahudumu wanaolengwa hapo ni katika maeneo ya kazi kama benki, madaktari wenyewe wanapaswa kuzingatia tahadhari; haishauriwi kuvaa mask hata kama utavaa je ni za ubora unaotakiwa?” alisisitiza.

Pia Mcharo aliongeza kuwa wahudumu wa benki wapo katika hatari ya kuambukiza wengine kutokana na uvaaji wa gloves zao wanapohudumia wateja pasipo kubadilisha.

“Kuna wahudumu wa benki wanavaa gloves ukiangalia ni kwamba anajikinga yeye je wewe kwani anawahudumia wengi bila kubadilisha. Sisi wenyewe madaktari tunavaa gloves kwa kila mgonjwa mmoja, wanapaswa kulitambua hilo,” aliongeza Mcharo.
Alisema mara nyingi virusi vya havina kinga ya chanjo,  silaha kubwa ya virusi ni kupambana na chanjo, hivyo  ni  vema Udhibiti wa  Maambukizi ya virusi ya ugonjwa wa Covid-19 mahali pa kazi ukadhibitiwa.

Alifafanua kuwa wataalamu wa afya wanahudumia wana jamii hivyo kama hawajapata elimu ya kujinga na virusi hivi  vinaweza kusababishwa kuenezwa kutoka kwa mtoa huduma za afya  kwenda kwa mgonjwa. kudhibiti maambukizi  kwenda kwa jamii.

Hata hivyo aliwatoa wasiwasi watanzania kuhusu juhudi ambazo serikali imekuwa ikiendelea kuzichukua dhidi ya ugonjwa huo akisisitiza kutosimamia habari za uongo zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu hali ya ugonjwa huo kwani watoaji wakuu wa taarifa ni Waziri wa Afya, Waziri Mkuu na Waziri wa Afya Zanzibar.

Wataalamu wa Afya kutoka wilaya za Siha, Rombo Hai, Same, Moshi DC, Mwanga na Manispaa ya Moshi ndio wanaopata semina hiyo kuhusu namna ya kupambana na maambukizi ya Covid-19.

STORY & PHOTO BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
DATE: Machi 30, 2020


















0 Comments:

Post a Comment