Tuesday, March 17, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Papa Shenouda III ni nani?

Machi 15, 2012 alifariki kiongozi wa juu wa Wakoptiki Papa Shenouda III. Wakoptiki ni wakristo wanaoishi katika eneo la Afrika ya Kanisa ambao kwa kiasi kikubwa wapo nchini Misri. 

Duniani kote inakisiwa kuwa na waumini milioni 20. Katika taifa la Misri ndiyo kundi kubwa zaidi la Wakristo lililopo nchini humo. Pia Wakoptiki wapo kwa wingi nchini Sudan na Libya. 

Kihistoria Wakoptiki huzungumza lugha ya Kikoptiki ambayo ilizungumzwa miaka ya mwanzoni kabisa wakati wa kuundwa kwa taifa la Misri. 

Pia Wakoptiki wanapatikana kwa wingi Mashariki ya Kati. Katika rekodi za hivi karibuni inaonyesha wanachukua asilimia 5-20 ya idadi ya watu wanaoishi katika ardhi ya Misri; licha ya kwamba watafiti hawakuruhusiwa kuweka bayana asilimia kutokana na sheria za taifa hilo ili kuweka umoja wa kitaifa. 

Nchini Sudan na Libya wanachukua takribani asilimia moja ya idadi ya watu katika mataifa hayo. Wakoptiki wengi ni waumini wa Makanisa ya Kikoptiki yaliyo na mlengo wa Kiothodoksi huko Alexandria yakiwa tofauti kiasi na Ukristo wa Magharibi. 

Kuna idadi ndogo tu ya Wakoptiki waliopo katika mrengo wa Ukatoliki hususan Ukatoliki wa Mashariki ambao umekuwa ukifuata baadhi ya kanuni na taratibu za Wakoptiki wa Alexandria.

Jina halisi la Papa Shenouda III ni Nazir Gayed Roufail. Alizaliwa Agosti 3, 1923 mnamo mwaka 1954 alikuwa mtumishi wa kanisa akitumia jina la Father Antonios wa Syria. 

Mnamo mwaka 1958 alipanda ngazi na kuingia katika Uchungaji. Mnamo mwaka 1962 Papa Cyril VI alimtawaza kuwa Askofu Mkuu wa Elimu ya Kikristo na Mwalimu wa Seminari ya Kitheolojia ya Coptic Orthodox. 

Akiwa katika seminari hiyo ndiko alikochukua jina la Shenouda kutokana na Mtakatifu wa Kikoptiki Shenoute wa Archimandrite ambaye aliishi kati ya mwaka 347 hadi 466.

Papa Shenouda III alipewa kukalia kiti hicho cha kuwa Papa wa 117 wa Alexandria na Mwangalizi Mkuu wa Mt. Marko Novemba 14, 1971 takribani miezi tisa baada ya kifo cha Papa Cyril VI wa Alexandria. 

Sherehe za kumsimika kuwa Papa wa Wakoptiki hao zilifanyika katika Kanisa jipya la Mt. Marko lililopo jijini Cairo. Papa Shenouda aliweka rekodi ya kuwa wa tatu kushika wadhifa huo kwa Ukoo wa Alexandria waliochagua kutumia jina la Shenouda na hii ndio sababu anafahamika kama Papa Shenouda III. Jina la Shenouda lilianza kutumiwa kwa mara ya kwanza mwaka 859 hadi 880. 

Mara ya pili lilitumiwa kuanzia mwaka 1047 hadi 1077. Papa Shenouda III alikalia kiti hicho kwa miaka 40, miezi minne na siku nne.

Mnamo mwaka 2000 Papa Shenouda alitunukiwa tuzo na Shirika la Umoja wa Mataifa UNESCO katika tuzo ya Madanjeet Singh kutokana na mchango wake wa kuhamasisha Jamii kuvumiliana na kuachana na vurugu. 

Alipewa tuzo hiyo na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO wakati huo Koichiro Matsuura ambaye wakati anamkabidhi alisema Papa Shenouda alikuwa kiungo muhimu katika kuweka utulivu baina ya Ukristo na Uislamu huko Mashariki ya Kati. 

Miaka mitatu baadaye alipokea tuzo nyingine ya Kimataifa ya Al-Gaddafi kutokana na kuhamasisha Haki za Binadamu

Enzi za uhai wake Papa Shenouda III aliandika vitabu 106 miongoni mwa hivyo ni "How to Deal with Children", "Temptation on the Mountain" na "Adam and Eve, Cain and Abel"

0 Comments:

Post a Comment