Machi 5, 1870 jiji la London lilikuwa mwenyeji wa mechi ya kimataifa ya kwanza katika mchezo wa soka baina ya wachezaji wa soka wa timu ya England na kundi la wachezaji wa Uskochi waliokuwa wakiishi jijini London.
Mchezo huo ulimalizika kwa sara ya 1-1. C.W. Alcock wa Old Harrovians ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha England na ambaye baadaye alikuwa mwanzilishi wa Kombe la FA ndiye aliyeratibu mchezo huo kati ya nchi hizo mbili na alikuwa nahodha wa kikosi cha timu ya England.
Kikosi cha kwanza cha Uskochi kilichaguliwa na Arthur Kinnaird na nahodha alikuwa James Kirkpatrick. Kinachovutia zaidi ni uwepo wa William Gladstone wa Old Etonia ambaye baba yake alikuja kuwa Waziri Mkuu.
Timu hizo zilikutana katika uwanja ambao ulikuwa na matope kutokana na mvua iliyokuwa imenyesha ambapo zilicheza hadi mapumziko kila timu ilishindwa kuvunja kitasa cha mwenzake.
Baada ya mapumziko timu hizo zilibadilisha upande, wakati huo ilikuwa ni jambo geni kubadilisha upande lakini wakati wa vikao kabla ya mchezo huo ilitangazwa kuwa ni sheria mpya hivyo utekelezaji wake ulianza katika mchezo huo.
Dakika ya 75 ya mchezo Alcock alimpandisha mlinda mlango juu zaidi huku akiacha lango likiwa wazi ambapo Mskochi Robert Crawford alifunga bao.
Hata hivyo Alfred Baker aliisawazishia England katika dakika ya 89 hivyo ikiwa sare ya 1-1. Baada ya mchezo huo zilifuata mechi nyingine nne kati ya Novemba 1870 na February 1872 ambazo moja ilikuwa sare na ushindi mara tatu kwa timu ya taifa ya England.
Licha ya kwamba zilichezwa lakini Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilizikataa kama mechi za kimataifa kwasababu zote zilichezewa London.
0 Comments:
Post a Comment