Walimu Wakuu wa
shule za sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), wameagizwa kuhakikisha wanasimamia maadili na uwajibikaji wa
waalimu na wanafunzi ili kuwezesha shule hizo zinazomilikiwa na Jumuiya
ya Wazazi kushindana katika ufaulu na shule za serikali nchini.
Hayo yamesemwa na
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Jumuiya ya Wazazi Paulo
Kirigiri, wakati alipokuwa akifungua semina ya siku moja ya Walimu wa
shule za Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Kilimanjaro, semina iliyofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Mwanga.
Kirigiri alisema kuwa
ili kuweza kuwa na uimara katika shule za Wazazi, ni lazima kukawa na mpango
maalumu wa kuziimarisha shule hizo kwa kuzijengea heshima ili ziweze kupambana
katika ubora na ufaulu na shule za serikali.
Alisema kuwa Walimu
wakuu wa Jumuiya ya wazazi kote nchini wanatakiwa kuhakikisha kila shule
inakuwa na mpango mkakati ili kujua muelekeo wa malengo yaliyopangwa na Jumuiya
hiyo katika kutimiza majukumu ya kila siku ya shule zao.
“Nawaombeni sana
tusimamie nidhamu mashuleni hususan kwenye shule zetu za wazazi, ili
tutengeneze kizazi ambacho ni cha viongozi wenye nidhamu, bila hivyo taifa
litapata wala rushwa, mafisadi hii yote ni kutokana na kutokuandaliwa vizuri
watoto,”alisema.
Kwa
upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoa wa Kilimanjaro,
Lugano Mwafongo, aliitaka idara ya ukaguzi wa shule kusimamia ubora wa elimu
nchini kwa kuhakikisha kuwa sera, sheria, kanuni na
viwango vya elimu vilivyowekwa katika mfumo wa utoaji elimu vinazingatiwa
ipasavyo kwa kuhakikisha mitaala na viwango vya elimu
vilivyowekwa vinafuatwa ili kuongeza ufanisi na ubora katika utoaji wa elimu.
“Mratibu elimu
wa Kata kama msimamizi wa shule aliye karibu na shule akisaidiana na mwalimu
mkuu ambaye ni msimamizi wa shule wa ndani, kwa pamoja wana nafasi
kubwa sana katika kusimamia elimu katika maeneo yao, kwani wataweza kutayarisha
taarifa na kuzitoa kwa wadau kwa wakati, vilevile zitasaidia wakaguzi wa
shule kufahamu mahali gani panahitaji marekebisho au kutiliwa
mkazo.”alisema Mwafongo.
Aidha Katibu huyo
alisikitishwa na baadhi ya maafisa wa elimu ngazi ya mkoa wamekuwa sehemu ya
kuzisemea vibaya shule za Wazazi, kwa kuwapigia simu wazazi na kuwaambia kuwa
wasipeleke watoto kwenye shule za Jumuiya ya Wazazi.
”Sisi kama chama
tunazo taarifa, wako baadhi ya maafisa wa elimu ngazi ya mkoa wamekuwa sehemu
ya kuzisemea vibaya shule zetu za Wazazi, wamekuwa wakiwapigia simu wazazi na
kuwaeleza kuwa wasipeleke watoto kwenye shule zetu za wazazi jambo hilo sio
zuri hata kidogo tunayo majina yao na tunatarajia kuyakabishi kwenye ngazi za
juu za uongozi,”alisema.
Alifafanua
kuwa wapo maafisa hao wamediliki hata kuzuia matokea ya kidato cha
nne ya shule ya Sekondari Minja kwa kutilia mashaka tu, na baadae
wakaja kujua ukweli kuwa matokea hayo yalikuwa na ukweli.
0 Comments:
Post a Comment