Friday, March 27, 2020

Unaikumbuka siku jezi ya Pele ilipouzwa kwa bei ghali?


Machi 27, 2002 jezi iliyokuwa ikivaliwa na mwanasoka wa Kimataifa wa Brazil Pele wakati wa Kombe la Dunia mwaka 1970 iliuzwa tena kwa kitita cha pauni 157,570.

Duka la nguo lililofahamika kwa jina la Christie alitarajia jezi hiyo angeiuza kwa sio chini ya pauni 50,000 lakini mtu ambaye hakufahamika mara moja alipiga simu na kuichukua kwa bei hiyo iliyovunja rekodi ya kwanza ya pauni 91, 750.

Jezi ya mwanasoka wa England Geoff Hurst ilikuwa ikishikilia rekodi hiyo kabla ya kuvunjwa na ya Pele. Hurst aliivaa jezi yake katika Kombe la Dunia mwaka 1966.

Jezi ya Pele iliyouzwa siku hiyo na kuvunja rekodi bado ilikuwa na alama za nyasi katika mechi ya fainali. Pele katika fainali hiyo alianza kwa kuvunja vitasa vya timu la taifa ya Italia  kwenye ushindi huo wa mabao 4-1.

Jezi hiyo iliuzwa dukani hapo na mlinzi wa Italia Roberto Rosato ambaye alibadilisha na Pele baada ya mechi kuisha.

PELE NI NANI?
Jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento.

Alizaliwa Oktoba 23, 1940  Três Corações, katika jimbo la Minas Gerais nchini Brazil. Anashikilia nafasi ya tano kwa ufungaji katika Kombe la Dunia akifunga mabao 12 katika mechi 14.

Mabao hayo aliyafunga katika Kombe la Dunia mwaka 1958, 1962, 1966, 1970.

Nafasi ya kwanza inashikwa na raia wa Ujerumani Miroslav Klose aliyefunga mabao 16 katika mechi 24. Klose amefunga katika Kombe la Dunia mwaka 2002, 2006, 2010, 2014.

Waandishi wa habari na mashabiki wanamtazama Pele kuwa mchezaji bora zaidi wa zama zote.

Alicheza kama mshambuliaji wa kati. Aliisaidia Brazili kutwaa kombe la dunia 1958, 1962 na baadaye tena mwaka 1970.

Aliweka rekodi mwaka 1958 ya kuwa mchezaji mdogo kuliko wote duniani kucheza katika fainali ya kombe la dunia alipocheza akiwa na umri wa miaka 17. Alivuma sana katika miaka ya 1970 duniani kote.

Mwaka 1999 alichaguliwa na shirikisho la mpira wa miguu duniani (FIFA) kuwa mchezaji bora wa karne. Kwa mujibu wa shirikisho la mpira wa miguu alikuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga magoli 1281 kati ya mechi 1363.

Ana wastani wa goli moja kwa kila mechi katika uchezaji wake wote. Katika kipindi cha uchezaji wake alikuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi duniani.

Pelé alianza kuichezea Santos akiwa na umri wa miaka 15 na timu ya taifa ya Brazil akiwa na miaka 16.

Ni mchezaji wa kibrazili anayeongoza kwa magoli mengi zaidi kwa kufunga magoli 77 kwenye mechi 92.

Brazil inamuheshimu kama shujaa wa taifa kwa mchango wake wa kisoka na sera zilizosaidia katika kupunguza umaskini katika nchi hiyo.

Katika uchezaji wake na mpaka kustaafu amepokea tuzo nyingi za timu na za binafsi kwa uwezo wake anapokuwa uwanjani na uvunjaji rekodi wake.

Mwaka 2013 aliulizwa kuhusu mchezaji bora wa kizazi cha sasa kuwa ni Muargentina Lionel Messi. 

Hata hivyo mwaka huu (2020) alipoulizwa tena alisema kuhusu hilo alisema Cristiano Ronaldo ni bora kuliko Messi lakini yeye ni Babalao.

0 Comments:

Post a Comment