Saturday, March 21, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Chinua Achebe ni nani?



Machi 21,2013 alifariki dunia mwandishi maarufu wa vitabu duniani Chinua Achebe. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 huko Boston nchini Marekani. 

Taarifa iliyotolewa kwa niaba ya familia yake, ilimwelezea Chinua Achebe kuwa mmoja wa waandishi wakubwa wa vitabu vya fasihi katika kipindi chake, ambaye busara yake ilikuwa kichocheo cha kumwiga kwa wale wote waliomfahamu.

Chinua Achebe alizaliwa mwaka 1930 ikiwa nimiaka 30 kabla ya uhuru wa Nigeria  katika Jimbo la Mashariki Kusini mwa Nigeria katika jamii ya Waigbo.

Anajulikana kama baba wa fasihi barani Afrika ambaye aliandika riwaya, mashairi na kitabu cha kumbukumbu ya maisha (memoir), ambacho kilikuwa kinasubiriwa kwa muda mrefu na watu wengi. Kimechapishwa mwaka 2012.

Chinua Achebe anasifika kuwa ni baba wa fasihi ya Afrika. Kila mtoto wa shule barani Afrika atakua amesoma kitabu chake mashuhuri kabisa Things Fall Apart. Kimefasiriwa kwa lugha kadhaa mkiwemo ya Kiswahili.

Achebe amewahamasisha watunzi wa barani Afrika na duniani kote na tungo zake zimesifiwa kwa kujivunia utamaduni wake wa Kiigbo kusini Mashariki mwa Nigeria.

Uzalendo wake kwa Afrika ulimfanya atupilie mbali jina lake la kwanza la Kiingereza-Albert-na badala yake kujiita Chinua.

Sifa za Chinua Achebe zinatokana na jinsi tungo zake zilivyosaidia mwamko wa mageuzi ya kimapinduzi katika Afrika.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Nigeria katika miaka ya 60 aliunga mkono Jamhuri iliyojitenga ya Biafra.

Baada ya vita Achebe alijitosa katika kampeni za kutetea demokrasia na utawala bora.
Kimsingi, vitabu alivyoandika viligusia maisha ya watu, athari na madhara ya ukoloni, rushwa katika jamii na jitihada za kuleta mabadiliko katika nchi yenye demokrasia.

Kitabu chake cha kwanza alichoandika, yaani ‘Things Fall Apart’ yaani 'Hamkani si Shwari Tena' kilichochapishwa mwaka 1958, kililenga katika kuonyesha mkanganyiko uliokuwapo kati ya mila na desturi za Kiafrika na zile za Wazungu na jinsi mila na desturi zetu zilivyoathiriwa na wakoloni.

Kitabu hiki kimetafsiriwa kwa lugha zaidi ya 50 na kuchapishwa zaidi ya nakala milioni 10.

Achebe alisema “ Mzungu ni mjanja sana. Alikuja kimyakimya na bila shari akatuletea dini yake.Tulifurahia ukimya wake na kumruhusu kuishi nasi. Sasa amewashikilia ndugu zetu na hawawezi tena kufurukuta. Amefanikiwa kuuvunja umoja wetu na ametumia kisu cha kukata yale mambo yaliyotuunganisha na sasa tumesambaratika.”

Mwandishi huyu alitumia lugha ya Kiingereza kuandika vitabu vyake, ili ujumbe wake uweze kuenea sehemu nyingi duniani,kwani lugha hii ilifahamika na watu wengi kuliko lugha yake ya Igbo.

Baba yake alibatizwa na kujiunga na madhehebu ya Kikristo ya Anglikana. Alifuatana na baba yake alipokuwa anatembea jimboni kuhubiri dini.

Alipokuwa Lagos ndipo alipokutana na mkewe mwaka 1961 na kufunga naye ndoa na kuzaa naye watoto wanne.

Vitabu alivyoandika ni vya riwaya, mashairi na insha na baadaye akawa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Nigeria.

Aliwahi kupewa tuzo na marais wawili wa Nigeria ambao ni Olusegun Obasanjo mwaka 2004 na Goodluck Jonathan mwaka 2011 lakini alizikataa akisema:

“Iko faida gani kuwa na demokrasia wakati wananchi wana njaa, hawana mahali salama pa kuishi na miundombinu haipo?

Usalama haupo na sehemu mbalimbali za nchi yetu zimetengana kutokana na misuguano ya kikabila na kidini na hakuna kinachofanyika kukabiliana na hali hii?

Mwaka 2012 alichapisha kitabu cha kumbukumbu ya maisha kilichoeleza maisha ya Biafra yalivyokuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya vita, wakati wananchi wa kabila la Igbo walipotaka kujitenga na Nigeria

Alilelewa na wazazi wake wa kabila la Waigbo katika mji wa Ogidi, jimbo la Anambra, kusini mashariki mwa Nigeria.

Achebe alikuwa mwanafunzi mahiri ambapo alipata tuzo ya kujifunza udaktari lakini akabadili mawazo na kujifunza fasihi ya Kiingereza kwenye chuo kikuu cha Ibadan.

Alipenda kujifunza masuala ya dini mbalimbali duniani na utamaduni wa Kiafrika. Baadaye akaanza kuandika hadithi akiwa bado mwanafunzi wa chuo kikuu.

Baada ya kuhitimu masomo yake alifanya kazi Shirika la Utangazaji la Nigeria (NBS) na baadaye akahamia Lagos.

Kitabu cha Things Fall Apart alichokiandika mwishoni mwa miaka ya 1950 kilimpatia jina kubwa duniani. Baadaye aliandika No Longer at Ease (1960), Arrow of God (1964), A Man of the People (1966), na Anthills of the Savannah (1987).

Achebe aliandika vitabu vyake kwa Kiingereza na alitetea matumizi ya Kiingereza, "lugha ya wakoloni" kwenye tamthiliya ya Kiafrika. Mwaka 1975, hotuba yake An Image of Africa: Racism in Conrad's "Heart of Darkness" ilimkosoa mwandishi Joseph Conrad kama mbaguzi wa rangi. Pamoja na kuzua utata, ilichapishwa kwenye jarida la The Massachusetts Review

Katika riwaya yake ya A man of the People; aliyoiandikwa  mwaka 1966 inaelezea hadithi ya kijana aliyeelimika aitwaye Odili, na vita vyake na Chief Nanga, mwalimu wake wa zamani ambaye aliingia katika siasa katika nchi ya kisasa ya Afrika isiyotajwa. Odili anawakilisha kizazi kipya; Nanga anawakilisha desturi ya Nigeria.

Odili anapokea mwaliko kutoka kwa mwalimu wake wa zamani, Chief Nanga, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Utamaduni. Kama waziri, kazi ya Nanga ni kulinda mila za nchi yake, na ingawa alijulikana kama "A Man of the People," anatumia nafasi hiyo kuongeza mali yake binafsi. Utajiri na nguvu wa waziri unamvutia mpenzi wa Odili, ambaye alimsaliti na kulala na waziri. Kutafuta kisasi, Odili anaanza kumfuata mpenzi wa waziri.

Odili anakubali kuongoza chama cha upinzani dhidi ya rushwa na vitisho na vurugu. Odili anapata ushindi juu ya waziri, hata hivyo, wakati vikosi vya mapinduzi ya kijeshi vinamlazimu mwalimu wake wa zamani kutoka ofisi. Kitabu kinaisha na mstari: "wewe ulikufa kifo kizuri kama maisha yako yalimhimiza mtu kuja mbele na kupiga risasi kifuani mwa muuaji wako - bila kuomba kulipwa."

Pia katika kitabu chake 'Things Fall Apart' yaani 'Hamkani si Shwari Tena' alichokiandika mwishoni mwa miaka 1950 kinaaminika ndicho kitabu chake bora zaidi, ni kitabu kilichosomwa kwa wingi zaidi katika vitabu vya tamthiliya ya Kiafrika.
Mhusika mkuu anaitwa Okonkwo, tajiri na mkulima katika kijiji cha Umuofia. Okonkwo anapambana kuhifadhi mila na utamaduni wake licha ya shinikizo kutoka wakoloni Waingereza. Huyo Okonkwo anaonekana kufuata vizuri sana mila na desturi za Waigbo ili kumshinda baba yake ambaye ni duni.

Katika kufuata hizo mila alifika hatua ya kumuua mwana wake wa kambo na wanakijiji wakakubali. Siku moja, lakini, Okonkwo kwa bahati mbaya alimuua mwanakijiji mwingine akahukumiwa kuondoka kijijini kwake kwa miaka saba zinavyoamuru mila za kijiji.

Huko uhamishoni Okonkwo alikutana na wamisionari Wazungu, akasikitika sana kugundua mwana wake mwenyewe aliacha mila za Kiigbo na kukubali dini ya Ukristo.

Okonkwo aliporudi kijijini baadaye akakuta hata maisha ya kijijini yameathiriwa na hiyo dini mpya. Akaanza kuupiga vita Ukristo, hatimaye lakini aliona kuwa haiwezekani kurudi kwa maisha ya kimila akajiua kwa kujinyonga.

Chinua Achebe alizikwa Machi 23, 2013 karibu na nyumba ya familia yake mjini Ogidi, kwenye mji mdogo wenye vilima huko Anambra.

0 Comments:

Post a Comment