Machi 11, 1870 alifariki dunia Mfalme wa Lesotho aliyefahamika kwa jina la Moshweshwe I.
Mfalme huyo alizaliwa huko Menkhoaneng kaskazini mwa Lesotho wakati huo ilikuwa ikifahamika kama Botha-bothe.
Moshweshwe I alikuwa mtoto wa kwanza Mokhachane ambaye alikuwa ni chifu mkuu wa ukoo wa Bamokoteli Koena.
Akiwa mtoto alifanikiwa kumsaidia sana baba yake kupata nguvu kutoka kwenye koo ndogo ndogo katika ardhi hiyo. Inaelezwa kuwa Moshweshwe alipofikisha umri wa miaka 34 alianzisha ukoo wake na kuwa Chifu mkuu.
Moshweshwe ikambidi ahame kutoka eneo alilozaliwa na kukulia na kwenda zake katika milima ya Butha-Buthe ambako yeye na wafuasi wake walikaa huko.
Moshweshwe alisoma shule ya awali na akiwa huko alipewa jina la Letlama ikiwa na maana 'Muunganiko Imara.'
Akiwa kijana alionekana mapema kuwa ni jasiri kwani alikuwa akifanya matukio ya kuvamia ng'ombe wa jamii ya Ramonaheng.
Pia Moshweshwe alikuwa akipendelea kujisifu kupitia mashairi ya jamii yake. Inaelezwa na wafuatiliaji wa masuala ya historia kuwa Moshweshwe alikuwa akijifananisha na 'Wembe ambao unatumika kunyoa nywele' akiwa na maana kuwa yeye ni wembe ambao unanyoa nywele za wapinzani wake hususani Ramonaheng.
Hiyo ilitokana na matukio mengi ya uvamizi na kuchukua mifugo kwa nguvu kupata mafanikio makubwa. Kwa lugha ya Sesotho inaelezwa kuwa wembe huwa unatumika kutengeneza mlio wa 'Shwe....Shwe' na ndio sababu ya kuitwa Moshweshwe ikiwa na maana ya Mnyoaji au Kinyozi.
Pia Moshweshwe alikuwa akijisemea kuwa ni wa kizazi cha Monaheng ambaye ndiye asili ya Watu wa Bakoena huko Lesothoisipokuwa Bamolibeli.
Moshweshwe na wafuasi wake wengi wao ni wa Bakoena Bamokoteli, lakini baadhi ni wa Bafokeng ambao ni kutoka upande wa mama yake na baadhi ya koo ikiwamo ukoo wa Amazizi waliamua kukaa katika milima ya Butha-Buthe.
Huko walikokaa ndiko baadaye kulikuja kumwibua miongoni mwa Wafalme wenye nguvu katika historia ya Afrika Shaka Zulu. Shaka Zulu alionekana wakati ule wa Vita vya Mfecane (Difaqane).
Mwanzoni mwa karne ya 19 Shaka alivamia jamii ndogondogo zilizokuwa Pwani ya Mashariki ya Afrika Kusini ambayo kwa sasa eneo hilo linafahamika kama Kwa-Zulu Natal na kuwaunganisha katika uchifu wa Zulu.
Koo ndogondogo zililazimika kuukimbia Ufalme wa Zulu. Hapo ndipo vita ilipoanza ya Mfecane ambayo huwa inafahamika kuwa ni wakati wa mateso ambao haujawahi kutokea kwa watu wa Lesotho.
Kipindi hiki WaSotho waliteswa na kunyanyaswa na ukoo uliovamia wa Nguni (Wangoni).
Sasa Moshweshwe alilazimika kuondoka na kwenda zake katika uwanda wa Qiloane ambapo baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa Thaba Bosiu au Mlima wakati wa Usiku. Jina hilo lililotokana na imani yao kwamba nyakati za usiku kulikuwapo na mlima na kunapokucha unatoweka.
Hali almbayo iliwasaidia katika kujilinda dhidi ya maadui. Hata ukienda leo Thaba Bosiu utaelezwa kuhusu historia ya Moshweshwe I na wafuasi wake kuhamia hapa.
Moshweshwe na wafuasi wake walitoka Butha-Buthe mnamo mwaka 1824 ikiwa ni mpango kamili wa kujiepusha na vita vya Mfecane.
Uwanda huo ulikuwa na ngome za asili hivyo ilikuwa ni ulinzi tosha kwa watu wa Basotho wakati wa vita.
Mnamo Julai 1824 Moshweshwe na wafuasi wake walianza kukaa rasmi na Moshweshwe ndiye aliyepaita mahali hapo Thaba Bosiu kutokana na kwamba watu wake waliwasili usiku.
Ili kuwaogopesha maadui zake alieneza habari kuwa nyakati za usiku mlima ulikuwa unakua mkubwa.
Moshweshwe alikuwa na uwezo wa kuwasaidia watu waliokimbia vita kwa chakula, malazi na makazi.
Na eneo hilo lilikuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua mifugo wengi na pia milima iliyokuwa pembeni iliweza kutoa ulinzi kwa mifugo na watu wake.
Moshweshwe ataendelea kukumbukwa kwani alipoona koo au watu waliokimbia vita wameshajitosheleza ndio aliweza kuwaambia waende zao lakini walio wengi hawakutaka kutoka wakasalia kuwa mikononi mwa Moshweshwe.
Mfalme huyo alisifika kwa moyo wake wa kutaka maridhiano na sio vita. Pia eneo hilo la Thaba Bosiu ndiko mwanzo wa kuzaliwa kwa taifa la Basotho na wakati wa ujio wa wageni kutoka Ulaya ilikuwa ni sehemu nzuri iliyotumika kupanga mipango namna ya kuwadhibiti wageni hao.
Mnamo mwaka 1852 wageni kutoka Ulaya pamoja na Makaburu wa Orange Free State walitaka kumchomoa kivungu Moshweshwe katika eneo hilo lakini walishindwa.
Makaburu ya Kidachi walizingira ngome ya Thaba Bosiu Agosti 18, 1865 wakiwa na askari akali ya 6,000 mikononi mwa Louw Wepener hawakufanikiwa kumwondoa Moshweshwe.
Makaburu hao waliendelea kuizingira Thaba Bosiu mpaka mwaka 1866 ndipo Moshweshwe alipokubali kusaini Mkataba wa Thaba Bosiu Aprili ya 1866.
Moshweshwe alikubali kuachia mifugo hususani ng'ombe akali ya 3,000 na theluthi mbili ya eneo la kilimo kwa makaburu hao. Mnamo mwaka 1867 ilipigwa tena ya vita ya tatu,
Makaburu walikuwa wameunda Dola Huru la Mto Orange ili waweze kumshambulia vikali lakini Moshweshwe aliamua kuwaendea Waingereza na hakutaka kulikabidhi kwa makaburu ambapo mwezi Machi 1868 Moshweshwe alikubali Basotho iwe koloni la Uingereza kwa masharti ya kupewa ulinzi.
Hivyo basi katika eneo lote la Basotho, Thaba Bosiu inasalia kuwa eneo ambalo halikukubali kushindwa kirahisi ukilinganisha na maeneo mengine.
Mnamo mwaka 1967 serikali ya Lesotho ilitangaza kuwa eneo hilo la mlima kuwa ni tunu ya taifa. Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) liliunga mkono hatua hiyo ya serikali ya Lesotho kwamba litaweka mkono wake ili eneo hilo liendelee kutunzwa kwa historia ya vizazi vijavyo.
Moshweshwe I alifariki mwaka 1870 na kuzikwa hapo Thaba Bosiu na hadi leo kaburi lake ni miongoni mwa vivutio nchini Lesotho.
0 Comments:
Post a Comment