Friday, March 13, 2020

Unaikumbuka siku mashabiki wa PSG na Galatasaray walizua vurugu uwanjani?

Machi 13, 2001 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baina ya Paris Saint Germain na Galatasaray kuliibuka vurugu baina ya mashabiki wa timu hizo katika mchezo uliochezwa katika dimba la Parc des Princes. 

Miamba hiyo miwili ilikuwa inakutana kwa mara ya pili katika msimu huo  ikiwa ni kwenye hatua ya makundi. Katika mchezo wa kwanza miamba hiyo ya Uturuki Galatasaray iliibuka na ushindi wa bao 1-0. 

Walipotua jijini Paris ulikuwa ndio mchezo wao wa mwisho katika hatua ya makundi. Galatasaray kwa wakati huo walikuwa wakitaka kujiimarisha kileleni mwa kundi hilo huku PSG ikiwa inatafuta ushindi wa kwanza katika hatua hiyo ya makundi. 

Nyota wa Brazil Christian aliipa uongozi PSG katika dakika ya tatu ya mchezo na katika dakika ya 24 nyota huyo alitupia tena na hivyo wenyeji wakawa mbele kwa mabao mawili. 

Mchecheto na kuchanganyikiwa kulikumba mashabiki wa Galatasaray waliosafiri kutoka Uturuki ambao walionyesha wazi kutoridhishwa na kiwango cha timu yao katika mchezo huo. Hapo ndipo walipoanza kuimba kuonyesha kutokubali kwao kwa hali hiyo. 

Hata hivyo mchecheto ulizidi zaidi kipindi cha pili walianza kung'oa viti na kuwatupia mashabiki hali iliyosababisha utulivu kukosekana katika majukwaa. Baadhi ya mashabiki waliumizwa na damu kumwagika. 

Katika dakika ya 59 mwamuzi Vitor Manuel Perreira alisimamisha mchezo huo na aliwaamuru wachezaji waondoke uwanjani na kwenda katika vyumba vya kubadilishia ili waweze kujadili na maofisa kuhusu hali iliyokuwapo uwanjani. 

Baada ya dakika 20 za majadiliano walikubaliana mechi iweze kuendelea. Mechi ilimalizika kwa mabao 2-0. 

Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), lilizipiga faini timu zote mbili PSG wakipigwa faini ya Shilingi bilioni 1.1 za Tanzania sawa na pauni 410,000 na Galatasaray walipigwa faini ya shilingi milioni 238.9

0 Comments:

Post a Comment