Saturday, March 7, 2020

Unaikumbuka siku Roy Makaay alipoweka rekodi ya bao la mapema kuliko yote Ulaya?


Machi 7, 2007 nyota wa Bayen Munich Roy Makaay aliifungia timu yake bao la mapema katika mashindano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Bao hilo lililingai katika rekodi ya kuwa bao la kwanza lililofungwa mapema kuliko bao lolote kwenye historia ya mashindano hayo.

Makaay alifunga bao hilo katika sekunde ya 10 ya mchezo dhidi ya Real Madrid.

Mchezo huo ulikuwa wa hatua ya 16 mzunguko wa pili ambapo katika mzunguko wa kwanza Real Madrid ilishinda katika uwanja wake wa nyumbani wa Santiago Bernabeu kwa mabao 3-2 lakini mabao mawili ya ugenini ya Bavarians yalikuwa na umuhimu mkubwa katika kuamua hatma ya kutinga hatua ya robo fainali.

Bayern walikuwa nyumbani katika dimba la Allianz mbele ya watazamaji 69,500 ambao waliona wakati Makaay akiweka rekodi ya bao hilo.

Real Madrid walianza mchezo huo lakini upokeaji mbovu wa Roberto Carlos uliruhusu nyota wa Bayern Hasan Salihamidzic kuuiba na kuizunguka safu ya ulinzi kisha kumwekea Makaay ambaye alimalizia vizuri mbele ya  mlinda mlango Iker Casillas ikiwa ni sekunde ya 10.12

Bao hilo lilivunja rekodi ya awali iliyowekwa na Mbrazil Gilberto Silva mnamo mwaka 2002 wakati huo akihudumu na Arsenal alitupia bao dhidi ya PSV Eindhoven katika sekunde ya 20.02 ya mchezo.

Mchezo ulimalizika kwa bao la Lucio katika kipindi cha pili (66') na Real Madrid katika mchezo huo walipata bao pekee kupitia kwa nyota wake Ruud van Nistelrooy katika dakika ya 83.

Bayern ilisonga mbele kwa mabao ya ugenini lakini ilipoteza katika robo fainali dhidi ya AC Milan.


0 Comments:

Post a Comment