Sunday, March 29, 2020

Bomoa bomoa Siha kwa wasiozingatia sheria


Wananchi   wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuzingatia Sheria wakati wa ujenzi wa makazi yao ili kuepuka kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa jambo linalosababisha bomoa bomoa isiyo ya lazima.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Juma Jani, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa Sanya Juu  ambao walifika  ofisini kwake kwa ajili ya kutoa malalamiko yao ya kuwepo kwa ujenzi holela usiofuata utaratibu  unaoendelea katika mji huo.

Makamu mwenyekiti huyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya  Sanya mjini alisema kuwa ni vyema wananchi wazingatie sheria kabla hawajaanza kujenga makazi yao husika kwa kutoa taarifa kwenye ofisi husika ili kuepuka ukiukwaji wa sheria za nchi katika ujenzi wa makazi yao.

“Niwaombe wananchi  wa wilaya ya Siha kuzingatia sheria na taratibu za nchi kwa sababu ubomoaji unaofanyika siyo kwa makusudi bali ni kwa sababu tu watu wamekiuka sheria zilizopo,”alisema

Jani alifafanua kuwa  yapo malalamiko, mengi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa  mengine kwa barua ofini kwake  ikiwemo barua kutoka kwa mtu mmoja aliyemtaja kwa  majina ya Zakaria Materu, akilalamikia ujenzi  usiofuata taratibu.

“Wapo  baadhi ya watu wamejenga vibanda vya biashara huku wengine wakijenga  ukuta  kwenye hifadhi ya barabara inayoelekea  kwenye majengo ya halmashauri ya zamani na kuifanya  barabara hiyo kupitika kwa shida licha ya kuagizwa kuibomoa lakini hadi leo agizo hilo halijatekelezwa,”alisema.

Alisema ni vyema Wananchi wakazingatia sheria kabla hawajaanza kujenga makazi yao husika kwa kutoa taarifa kwenye ofisi ili kuepuka ukiukaji wa sheria  za nchi katika ujenzi wa makazi

Akiongea na waandishi wa habari jana Zakatia Materu, alisema amemuandikia barua ya malalamiko diwani wa eneo hilo, Mkuu wa wilaya na Mkurungenzi mtendaji  wa halmashauri hiyo, kuhusu barabra hiyo ya kuelekea halmashauri ya zamani waiangalie kwani wapo baadhi ya wafanyabiashara wenye fedha zao wameamua kujenga hadi kwenye hifadhi ya barabara jambo ambalo limesababisha adha kwa watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Mwandishi wa habari hizi alimtafuta Mkurugenzi  mtendaji wa  halmashauri hiyo  Ndakio Muhuli, ili kupata kauli yake juu ya  kushindwa kutekeleza agizo lililotolewa na baraza la madiwani.

Akiongea Mkurungezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndaki Muhuli,  alisema taarifa hizo  kwanza amezipata  hivyo, atatuma wataalamu wake, ili kwenda kulitembelea eneo hilo linalololalamikiwa ili  kujua ukweli wake kabla hajatekeleza maagizo yaliyotolewa.

STORY BY: Kija Elias
PHOTO: Maktaba
EMAIL: eliaskisena@gmail.com
DATE: Machi 22, 2020

0 Comments:

Post a Comment