Siku hizi uhusiano wa umaskini na uharibifu wa mazingira unaeleweka vizuri. Mathalani, uharibifu wa mazingira husababisha umaskini kwa kupunguza upatikanaji wa maji safi, rutuba katika udongo, mazao na huduma nyingine muhimu kwa afya na maisha ya binadamu. Aidha umaskini nao husababisha uharibifu wa mazingira kwa kudhoofisha juhudi na uwezo wa binadamu kusimamia na kutumia rasilimali kwa njia endelevu.
Sera ya Taifa ya Mazingira ya 1997 imeainisha changamoto sita ambazo ni: uharibifu wa ardhi; uharibifu wa misitu; kupotea kwa makazi ya viumbe-pori na bioanuai; kukosekana kwa maji salama mjini na vijijini; kupungua kwa ubora wa mifumo ya maji; na uchafuzi wa mazingira hasa katika maeneo ya mijini. Changamoto hizi zinachangia kuzorotesha ukuaji wa uchumi na juhudi za serikali katika kupunguza umaskini, na hivyo kuathiri maisha na ustawi wa jamii.
Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imeeleza wazi wajibu na majukumu ya wadau mbalimbali kuanzia serikali za mitaa hadi taifa. Mambo yanayosisitizwa katika Sheria hii ni mipango na usimamizi wa matumizi endelevu ya mazingira: kudhibiti uchafuzi wa mazingira; utunzaji wa taarifa na takwimu za mazingira; utafiti na ushiriki wa jamii, utekelezaji wa majukumu yatokanayo na mikataba ya kimataifa, utii na utekelezaji wa sheria pamoja na matumizi ya dhana mbalimbali za kusimamia hifadhi ya mazingira
0 Comments:
Post a Comment