Saturday, March 14, 2020

Polisi Tanzania yaizabua Ndanda FC 1-0 mjini Moshi

Polisi Tanzania imeendelea kujiimarisha katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Bao pekee la Polisi Tanzania lilifungwa kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 13 ya mchezo na kiungo mshambuliaji Marcel Kaheza.

Mlinda mlango Ally Mustapha Mtinge 'Barthez' hakuweza kuzuia mkwaju huo kutinga wavuni katika mchezo huo ulikuwa na kasi kwa timu zote mbili.

Adhabu hiyo ilitokana na makosa ya walinzi wa kati wa Ndanda FC kumvuta mabega winga wa Polisi Tanzania Mateo Anthony aliyekuwa katika harakati za kuukwamisha mpira huo wavuni baada ya kuwalazimisha walinzi hao kuingia katika eneo la hatari.

Katika kipindi cha kwanza Polisi Tanzania ilipata nafasi nyingine muhimu ambayo iligonga mhimili wa goli upande wa chini  kaskazini katika kipindi cha kwanza baada ya Iddi Mobby kuupokea mpira uliomiminwa na kiungo Jimmy Shoji kutoka wingi ya kulia na kuukandamiza kwa kichwa.

Kaheza, Mohamed Mkopi, Andrew Chamungu walikosa nafasi muhimu za kukwamisha mpira wavuni katika kipindi cha pili.

Aidha Polisi Tanzania imepata ushindi huo bila winga wake mahiri Sixtus Sabilo ambaye ameitwa kikosi cha timu ya Taifa kwa wachezaji wa ndani kwa ajili ya michuano ya Afrika.

Pia mabadiliko yalionekana hii leo katika safu ya ulinzi kushoto baada ya nafasi ya Yassin Mustapha kuchukuliwa na chipukizi linalokuja kwa kasi Juma Hadji.

Kiungo mkabaji Pato Ngonyani alianzia benchi huku Baraka Majogoro akichukua nafasi yake.
Nafasi ya mlinda mlango hii katka mchezo huo ilichukuliwa na Peter Manyika Jr. ambapo mzoefu Mohamed Ali Yusuf alipumzishwa katika mchezo huo.

Shoji alipata majeruhi katika kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Chamungu.
Kocha Malale Hamsini wa Polisi Tanzania amesema katika mchezo huo timu yake licha ya ushindi ni lazima akubali kwamba ilicheza chini ya kiwango lakini cha msingi ni kuendelea kupambana kufikia malengo.

Kikosi cha Polisi Tanzania kiliundwa na;  Peter Manyika Jr. Shaban Stambuli, Juma Haji. Iddy Mobby, Mohamed Kassim, Baraka Majogoro, Jimmy Shoji, Hassan Maulid, Mohamed Mkopi, Marcel Kaheza na Mateo Anthony.

Wa Akiba; Mohamed Ali, Pato Ngonyani, Andrew Chamungu, Mohamed Mmanga, Pius Buswita, Henrico Kayombo na Krote Samson.

Kikosi cha Ndanda kiliundwa na; Ally Mustapha, Aziz Sibo, Hemed Khoja, Samweli John, Paul Maona, Geodfrey Molibiche, Abdul Hamis, Taro Joseph,  Hussein Javu, Vitalisi Mayanga na Kigi Makasy.
Wa Akiba; Ismail Rajabu, Shafii Mdimu, Salum Chubi, Abdulaziz Mohamed, Omary Hamis.

STORY & PHOTO BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
DATE: Machi 14, 2020

Manahodha wa Polisi Tanzania (Iddy Mobby) na Ndanda FC (Kigi Makassy) kabla ya mchezo wa VPL Machi 14, 2020.

Polisi Tanzania wakiomba dua kabla ya kuanza mchezo dhidi ya Ndanda FC

Ndanda FC wakiomba dua kabla ya kuanza mchezo dhidi ya Polisi Tanzania

Polisi Tanzania vs Ndanda FC Machi 14, 2020

Baraka Majogoro 

Mateo Anthony akitolewa njiani na mlinzi wa Ndanda FC.

Vitalisi Mayanga akizuiwa na wachezaji wenzake kumvaa mwamuzi wa mchezo dhidi ya Polisi Tanzania.

Marcel Kaheza akichuana na Samwel John


0 Comments:

Post a Comment