Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro imetoa dawa za kinga tiba ya ugonjwa wa kichocho na ya tumbo jumla ya watoto 32,000, wenye umri wa miaka mitano 5 hadi 14 ikiwa ni juhudi za serikali za kutokomoza magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Zoezi la ugawaji wa dawa hizo lilianza mwanzoni mwa Machi mwaka huu, katika shule za msingi za serikali na za binafsi zilizopo Manispaa ya Moshi ambapo pia zoezi hilo liliwahusisha watoto wale ambao hawajaandikishwa shule, kuanzia miaka 5 hadi 14.
Akizungumza jana na mwandishi wa habari, ofisini kwake kwa njia ya mahojiano Afisa afya Manispaa hiyo Sebastian Mgeta alisema kuwa mchakato wa utoajia kinga tiba uliofanywa na idara ya afya ulifanikiwa kuwafikia watoto 32,000 wa shule za msingi zilizopo katika Manispaa hiyo.
”Ni kweli tulikuwa na zoezi la utoaji kinga tiba kwa kwa watoto wa shule za msingi, huduma hii ilifanyika Machi 4 hadi Machi 5, lakini pia zoezi hilo lilihusisha watoto wale ambao hawajaandikishwa shule, kuanzia miaka mitano hadi 14,”alisema.
Mgeta aliendelea kusema kuwa ugonjwa wa kichocho ni tatizo kubwa kwa watoto na usipopata tiba kwa haraka husabisha madhara na wakati mwingine vifo, hivyo ni vema wazazi kuchukua tahadhari kwa kuwapa watoto dawa hizo pindi serikali inapoendesha zoezi la kuwapatia watoto dawa za kinga tiba.
“Serikali imekuwa ikitoa huduma ya kinga tiba bure kwa nchi nzima, hivyo niwaombe wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao, wanapata kinga tiba hizo muhimu na kuwaondoa hofu wale wanaodhani dawa hizo zina madhara kwa watoto,”alisema Mgeta.
Aidha Mgeta aliiomba jamii kuunga mkono utoaji wa kinga tiba ya minyoo kwa watoto hao wenye umri wa miaka mitano hadi kumi na nne kwani ni muhimu kwa walengwa hao.
”Kinga hiyo zinaua vimelea ya magonjwa ya minyoo lakini pia inaimarisha ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili, kinga hiyo pia inapunguza utapiamlo, kuepusha upungufu wa damu mwilini, hivyo tunasisistiza watoto wameze dawa hiyo kwa wakati mmoja kwa sababu vinaua ule mzunguko wa ile minyoo.
Kwa mujibu wa afya huyo wa Manispaa ya Moshi, alisema serikali imekuwa ikisimamia utoaji wa kinga tiba ya minyoo kwa watoto wenye umri wa miaka mitano na sasa imeonyesha mafanikio makubwa.
0 Comments:
Post a Comment