Wednesday, March 18, 2020

Unaikumbuka siku Fulham ilipoiadhibu Juventus?


Machi 18, 2010 klabu ya soka ya Fulham iliweka rekodi muhimu katika michuano ya Ulaya pale ilipoizabua miamba ya soka ya Italia Juventus kwa uwiano wa mabao 5-4. 

Fulham ilikuwa ikishiriki Ligi ya Europa kwa mara ya pili lakini katika mchezo huo Fulham ilikuwa na uzoefu mkubwa dhidi ya Juventus kutokana na kwamba hapo kabla ilikuwa imeshakutana ikiwamo katika hatua ya makundi. 

Katika hatua ya makundi Fulham ilikuwa tayari imekwisha shinda  dhidi ya FC Basel mara mbili na CSKA Sofia na ushindi dhidi ya Shakhtar Donetsk. 

Katika mchezo wa kwanza Fulham ilipoteza mjini Turin kwa kichapo cha mabao 3-1 sasa mchezo wa pili ulikuwa ukichezewa Magharibi mwa London katika viunga vya Craven Cottage. 

Katika dakika ya pili ya mchezo nyota wa Juventus David Trezeguet alizidisha machungu kwa Fulham pale alipotupia bao hivyo kufanya uwiano kuwa mabao 4-1. 

Hata hivyo dakika saba baadaye Bobby Zamora alitupia bao. Katika dakika ya 27 mlinzi machachari Fabio Cannavaro alionyeshwa kadi nyekundu na kutolewa nje baada ya kumchezea faulo Zoltan Gera ambaye katika dakika ya 39 alifunga bao hivyo uwiano kuwa mabao 4-3. 

Muda mfupi baada ya mapumziko Gera aliisawazishia Fulham kwa mkwaju wa penati baada ya mpira kushikwa na mkono katika dakika ya 49 ya mchezo hivyo uwiano kuwa 4-4. 

Hakika ilikuwa mechi ya kustaajabisha. Katika dakika ya 83 Fulham iliushangaza ulimwengu baada ya mchezaji wa akiba aliyeingia akitokea benchi kupigilia msumari wa mwisho nje ya 18 kwa mkwaju wa kupinda na kuukwamisha mpira wavuni.

Licha ya Fulham kufika fainali ya Ligi ya Europa lakini ilishindwa kuhema mbele ya Atletico Madrid.

0 Comments:

Post a Comment