Meneja Masoko na Mauzo wa Bonite Bottlers Christopher Loiruk |
Tahadhari imeendelea kuchukuliwa katika makampuni mbalimbali kuhusu kusambaa kwa virusi vya Covid-19 ambapo Kampuni ya Vinywaji Baridi ya Bonite Bottlers Ltd mjini Moshi, Kilimanjaro imekuwa miongoni mwa washiriki wa mwanzo kuchukua tahadhari hiyo katika eneo la kiwanda hicho kwa kuweka vifaa mbalimbali vikiwamo dawa za kunawia mikono kwa ajili ya wafanyakazi na wateja wake.
Hapo jana ulionekana msururu mrefu wa wateja katika milango ya kuingilia kiwandani hapo wakikaguliwa kwa ulinzi madhubuti huku wakitakiwa kunawa mikono katika vifaa vilivyowekwa katika kuta.
Haya yamejiri ikiwa ni siku moja baada ya mgonjwa wa Covid-19 kubainika jijini Arusha na kuletwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mjini Moshi pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzifunga shule zote na maeneo ya mikusanyiko mikubwa.
Hata hivyo uongozi wa Bonite Bottlers Ltd umesisitiza umuhimu wa wateja wake kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya Covid-19 kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kujikinga na maambukizi hayo
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi za washindi wa Shindano la V.I.P Club 2019 iliyofanyika kiwandani hapo Meneja Masoko na Mauzo wa Bonite Bottlers Christopher Loiruk alisema hawana budi kuchukua tahadhari zote kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi na wateja.
Wateja 25 waliojishindia pikipiki kutoka Manyara, Karatu, Singida, Arusha na Kilimanjaro walikabidhiwa zawadi zao na kuondoka nazo.
Wateja wengine 18 waliojishindia kreti 50 na 100 za soda walikuwa miongoni mwa waliokabidhiwa zawadi zao katika hafla hiyo.
DATE: Machi 17, 2020
STORY & PHOTO BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment