Thursday, March 19, 2020

Covid-19 yaahirisha mkutano wa Kimataifa KCMC

Mkurugenzi mtendaji hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Profesa Gileard Masenga.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), ukishirikiana  na taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (KCRI), umelazimika kuaihirisha mkutano wake wa Kimataifa uliokuwa ufanyike kuanzia Aprili moshi hadi Aprili nne mwaka huu, mkoani Kilimanjaro  kutokana na kuwepo kwa virusi vya Corona.
Mkutano huo ambao  ulikuwa ukitajwa kuwa wa kisayansi ambao ulikuwa ufanyike katika hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), ulilenga kuwashirikisha wataalamu wabobezi wa magonjwa ya saratani kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Italia na Ujerumani.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Profesa Gileard Masenga, alisema kuwa hospitali hiyo ilitarajia kuwa na mkutano wa siku nne kwa ajili ya wataalamu hao kutoa mada mbalimbali  zinazohusiana na magonjwa ya saratani.
“Kuanzia Aprili mosi hadi aprili 4 mwaka huu, tulitegemea kuwa na semina ya kimataifa  ambayo ililenga kutoa elimu juu ya  ugonjwa wa saratani, semina hii ilikuwa ifanyike mkoani Kilimanjaro, lakini kutokana na kuwepo kwa virusi vya Corona uongozi wa hospitali imetulazumu kuuairisha mkutano huu hadi hapo dunia itakapokuwa salama,”alisema Prof Masenga.
Alisema katika mkutano huo wa kimataifa  kulikuwa na Maktari Bingwa 15  ambao wamebobea katika magonjwa ya saratani  ndio walikuwa washiriki kwenye mkutano huo, kwa ajili ya kutoa mada mbalimbali zinazohusu magonjwa ya saratani.
“Na sisi kama taasisi tunao wajibu wa kuwakinga Watanzania wenzetu wasipatwe na maambukizi ya virusi vya Corona Covid 19, tulitarajia kuwa na wataalamu kutoka nchi  nne duniani kama Marekani, Uingereza, Italia na Ujerumani,  tumeamua kuuairisha mkutano huu  hadi hapo dunia itakapokuwa salama,”alifafanua.
Vile vile uongozi wa hospitali ya (KCMC), umeona ni vyema kwa kipindi hiki kuwaomba wagonjwa na ndugu za wagonjwa, kuwa na ndugu mmoja ambaye atakuwa akimtembelea mgonjwa au kumuuguza kwa wakati wote atakapokuwa hospitalini hapo.
“Ndugu huyo atapatiwa kitambulisho maalumu, kwa sababu hiyo ndugu zaidi ya mmoja hawataruhusiwa kumtembelea mgonjwa kwa kipindi chote hiki atakapokuwa amelazwa hospitalini hapo,”alisema.
Aidha kwa mgonjwa ambaye hatahitaji msaada wa ndugu wa karibu hospitali imependekeza kuwa atumie simu kuwasiliana na ndugu na jamaa zake kuhusu mwenendo wa afya ya mgonjwa wake pindi akiwa hospitalini hapo. 
“Tuwaombe wagonjwa wanaokuja kliniki ama kuanza matibabu kuja peke yao  ama ikiwezekana aje na ndugu mmoja kwa yule aliyezidiwa  au ambae anahitaji msaada zaidi,”alisema.
STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EMAIL: eliaskisena@gmail.com
DATE: Machi 18, 2020



0 Comments:

Post a Comment