Monday, March 23, 2020

Mgonjwa wa Covid-19 agunduliwa Kilimanjaro

Mgonjwa mwingine amegunduliwa kuugua homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Covid-19 mkoani Kilimanjaro na kufanya idadi ya wagonjwa kufikia 13 nchini kote.

Mgonjwa huyo amegunduliwa jana Jumapili katika eneo la Shant town Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, akitokea nchini Marekani.

Mgonjwa huyo Frida Marealle, raia wa Sweden ameolewa na mmoja ya watoto wa familia ya Chief Marealle.

Mgonjwa huyo aliingia Moshi akitokea nchini Marekani kuja kuhudhuria shughuli za mazishi ya Mama mzazi wa familia hiyo.

Taarifa hizo zimethibitishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt Anna Mghwira wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari, alisema kuwa Frida Marealle,alibainika kuugua ugonjwa huo baada ya kuwasilia uwanja wa ndege wa Kimataifa KIA.

“Katika mkoa wetu wa Kilimanjaro  kuna mtu mmoja aliyebainika kuwa na ugonjwa wa (COVID-19) ambaye ni raia wa  Sweden ambaye ameolewa na Mtanzania, mgonjwa huyo  alikuwa ameenda kwao likizo, wakati anarudi alikutana na  tatizo,”alisema Dkt. Mghwira.

Alisema mgonjwa huyo aligundulika alipofika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa KIA  na kwamba kwa sasa amewekwa katika karantini kwa siku 14 katika Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

“Kwa sasa mgonjwa huyo sampuli zake, vimepelekwa katika maabara kuu ya taifa kwa ajili ya uchunguzi zaidi,”alisema.

STORY BY: Kija Elias
EMAIL: eliaskisena@gmail.com
DATE: Machi 22, 2020

0 Comments:

Post a Comment