|
Hekaheka katika lango la Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Machi 11, 2020 uliochezwa katika Uwanja wa Ushirika Mjini Moshi, Kilimanjaro. Polisi Tanzania 0-0 Mtibwa Sugar. (Picha zote Na. Jabir Johnson) |
Timu ya Polisi Tanzania imeweka bayana kuwa viporo vya mechi zake katika Ligi Kuu Tanzania (VPL) hususani wanavyopangiwa kucheza asubuhi vimekuwa kikwazo kikubwa kufikia malengo waliyojiwekea msimu huu.
Hayo yalijiri baada ya mchezo wa Jumatano asubuhi Machi 11 mwaka huu dhidi ya Mtibwa Sugar kumalizika kwa sare tasa, ikiwa ni siku moja baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Akizungumza kocha Malale Hamsini wa Polisi Tanzania alisema sare dhidi ya Mtibwa imemuuma sana licha ya kwamba hana budi kuwapongeza wachezaji wake hususani washambuliaji kwa kujitahidi kufanya wanaloweza bila mafanikio.
Hata hivyo Malale amelalamikia mechi za asubuhi kuwa ni kikwazo kikubwa kufikia malengo msimu huu waliyojiwekea hasa ikizingatiwa wamepatia kusalia katika 10 bora katika msimamo wa ligi kuu.
"Mechi za asubuhi zimekuwa mwiba kwetu hazitupi matokeo mazuri, zinapoteza sana mwelekeo wetu wa kujiimarisha kwenye Top 10 ya msimamo wa Ligi Kuu," alisema Malale.
Polisi Tanzania ilipoteza dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0 huko Mabatini mechi ambayo ilichezwa asubuhi katika mzunguko wa kwanza.
Katika mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu huu ilipoteza dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga kwa kichapo cha mabao 2-1.
Pia sare tasa dhidi ya Mtibwa iliyochezwa asubuhi ni miongoni mwa viporo ambavyo ni mwiba mkali kwa Malale.
STORY & PHOTO BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment