John Henjewele |
Viongozi wa Vyama vya Ushirika waliotumikia vyama vyao kwa vipindi vya miaka sita wamezuiwa kugombea nafasi za ujumbe wa bodi ya uongozi.
Hayo yamebainishwa jana na mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Kilimanjaro John Henjewele, wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na uchaguzi wa viongozi wa vyama vya ushirika kwa mwaka 2020.
John alisema viongozi wa bodi za vyama vya ushirika, ambao wametumikia vyama vyao kwa kipindi cha miaka sita mfululizo hawatakuwa na nafasi za kuomba tena nafasi za ujumbe wa bodi ya uongozi ndani ya vyama vya ushirika.
“Ni kweli tunafanya chaguzi za viongozi wa bodi za vyama vya ushirika katika mkoa wetu wa Kilimanjaro na chaguzi hizi hazifanyika katika mkoa wa Kilimanjaro pekee zinafanyika nchi nzima kwa maana ya Tanzani Bara,” alisema John.
Aidha mrajisi msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Henjewele John amewakumbusha viongozi wa vyama vya ushirika ngazi ya wilaya kuzingatia suala la kufanya chaguzi za viongozi wa vyama kwa mujibu wa sheria, inayoelekeza vyama kufanya chaguzi kila baada ya miaka mitatu ya uongozi.
John alisisitiza kuwa kufanya chaguzi na kupata viongozi wapya ni njia bora ya kuwajengea uwezo wengine katika uongozi, kukuza vipaji na kuhakikisha uendelevu wa vyama.
Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege, umewaagiza Warajisi wasaidi wa mikoa kuhakikisha kuwa chaguzi katika vyama vya msingi ambavyo ni wanachama wa vyama vya upili zinakamilisha uchaguzi kabla ya kufanya kwa chaguzi hizo kwenye ngazi ya vyama vikuu na miradi ya pamoja inayohusika.
“Kwa mamkala niliyopewa chini ya kanuni ya 81 ya kanuni za vyama vya ushirika za mwaka 2015, ninaagiza kuwa vyama vyote vya ushirika ambavyo viongozi wake wanamaliza kipindi chao cha uongozi mwaka huu 2020, kufanya uchaguzi wa viongozi wa vyama hivyo kupitia mikutano mikuu maalumu kabla ya Juni 30 mwaka huu, bila kujali mwezi ambao viongozi hao wamekamilisha miaka mitatu ya kuwa madarakani,”alisema Dkt. Ndiege.
Alifafanua kuwa “Vyama vya ushirika nchini vinaongozwa na viongozi waliochaguliwa kwa kuzingatia sheria ya vyama vya ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015.
Wilaya ya Same ndio wilaya pekee ambayo imekamilisha uchaguzi wake wa viongozi wa bodi za vyama vya ushirika, ambapo vyama vya Amcos 9 vimefanya uchaguzi, Saccos 2, walaji na shughuli maalum 1.
DATE: Machi 19, 2020
STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EMAIL: eliaskisena@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment