Wednesday, March 25, 2020

Covid-19: Kanisa la KLFT lafunga makanisa yake

Kutokana na kuenea kwa kasi ya virusi vya Corona duniani, Kanisa la Furaha Tanzania (KLFT), limetangaza kuyafunga makanisa yake yote  na kuwataka waamini wake kusali wakiwa majumbani mwao.

Katazo hilo lilitolewa juzi  jumapili   na  Askofu Mkuu wa kanisa hilo Jones Molla,  kwenye Ibada iliyofanyika katika kanisa la Shia lililopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa mahubiri yake.

Akinukuu kitabu cha Kumbukumbu la Torati 28:22 alisema “Bwana atakupiga kwa kifua kikuu na kwa homa na kwa kuwashwa na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie,”alisema Askofu Molla.

Askofu Molla amewaagiza viongozi wote wa makanisa hayo kuwa mikusanyiko ambayo inafanyika kwenye makanisa hayo isitishwe hadi hapo hali itakaporejea huku akiwataka pia waamini waweze kujikinga na ugonjwa huo wa Covid-19 uliolikumba taifa la Tanzania na duniani kote.

“Ninaagiza Ibada zote za Jumapili zifanyike nyumbani wanakoishi na watu waendelee kujitakasa mikono yao na kuwa mbali na mtu anayeshukiwa kuwa na virusi hivyo, tumuombe Mungu atuokoe na janga hili la kidunia,”

Askofu Molla  aliwataka  watanzania kwa ujumla kutokuwa na hofu wala kujengeana hofu kutokana na ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona na badala yake wawe na Imani na Matumaini ya kuwa utakwisha muda usio mrefu,.

Alisema ugonjwa  Covid-19 umekuja ghafla na kuzua hofu miongoni wa nchi nyingi Duniani ikiwemo na Tanzania, hivyo njia ya kupambana nao ni kuondoa hofu na kujenga Imani na matumaini ya kuwa utakwisha kwa Kusali na Kutubu bila ya kukoma.

Wengine wameacha kusalimiana kwa kushikana mikono na kukumbatiana, huku wengine wakibuni namna mpya ya kusalimiana kwa kugonga miguu, lakini pia taratibu za kwenye Makanisa, misikiti na mahekalu pia zimebadilika, zikiwa ni jitihada za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

STORY BY: Kija Elias
DATE: Machi 24, 2020

0 Comments:

Post a Comment