Machi 6, 1997 alifariki dunia mwanasiasa na waziri Mkuu wa kwanza wa Guyana. Jina lake halisi ni Dkt. Cheddi Berret Jagan ambaye aliwahi kushika wa wadhifa wa Waziri Mkuu wa taifa hilo mwaka 1953 na baada ya uhuru wa taifa hilo kutoka mwaka 1961 hadi 1964.
Aidha mnamo mwaka 1992 hadi kifo chake aliliongoza taifa hilo akiwa Rais. Nchini Guyana Jagan amekuwa akichukuliwa kuwa ni Baba wa Taifa hilo. Mnamo mwaka 1953 Jagan aliweka rekodi ya kuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya India kushinda uchaguzi na kuliongoza taifa hilo kutoka nje ya Asia ya Kusini.
Februari 15, 1997 Jagan alipelekewa katika hospitali ya Georgetown. Siku hiyo alipelekwa na ndege ya kijeshi kutoka katika Uwanja wa Kijeshi wa Andrews hadi Walter Reed mjini Washington D.C nchini Marekani.
Siku iliyofuata alifanyiwa upasuaji wa moyo na alifariki dunia Machi 6, 1997 ikiwa ni siku 16 kabla ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake ambapo angekuwa anafikisha miaka 79.
Waziri Mkuu Sam Hinds alipokea mikoba ya kuliongoza taifa hilo na alitangaza siku sita za maombolezo huku akimwelezea kuwa Jagan alikuwa mtu mkubwa na mzalendo wa kweli katika ardhi ya taifa hilo.
Enzi za uhai wake mnamo mwaka 1943 alimwoa Janet Rosenberg na kuzaa watoto wawili Nadira na Cheddi Jr. ambao baadaye walikuja kumletea wajukuu watano.
Janet alikuja kukanyaga nyayo za mumewe kwani mwaka huo huo alishika wadhifa wa Waziri Mkuu na Rais wa taifa hilo mnamo mwaka 1999 alipomkabidhi Bharrat Jagdeo.
Aidha Jagan alikuwa mwandishi mzuri wa vitabu, miongoni mwa kazi zake ni Forbidden Freedom: The Story of British Guiana (Hansib, 1954), The West On Trial: My Fight for Guyana's Freedom (Harpy, 1966), The Caribbean Revolution (1979) na The Caribbean: Whose Backyard? (1984).
Pia aliandika Selected Speeches 1992-1994 (Hansib, 1995), The USA in South America (Hansib, 1998), A New Global Human Order (Harpy, 1999) na Selected Correspondences 1953-1965 (Dido Press, 2004)
Jagan alishinda uchaguzi wa mwaka 1953. Licha ya ushindi huo Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo Winston Churchill alionyesha wasiwasi wake kuhusu Jagan kuwa ni mwamini wa sera za Marx na Lenin.
Kwa kuwa mfuasi wa sera za Marx na Lenin huenda angewaleta Warusi katika ardhi hiyo na kuiweka kuwa ya Kisovieti kitu ambacho kingekuwa hatari kwa Uingereza na washirika
Kiuhalisi hakukuwa na ushahidi wowote kuhusu mafungamano ya Jagan na upande huo wa Kikomunisti au makundi ya Ukombozi.
Lakini hofu hiyo ililifanya jeshi la Uingereza kuingilia kati ushindi wake siku chache baada ya kukalia wadhifa kuwa Waziri Mkuu wa Guyana.
Hata hivyo Jagan alijiuzulu nafasi hiyo ikiwa ni siku 133 tangu akalie kiti hicho. Uingereza ilivunja katiba ya taifa hilo ambalo lilikuwa koloni lake na kuweka serikali ya mpito.
Jagan hakuishia hapo licha ya vikwazo vingi alivyowekea na Uingereza ushindi wa Chama cha PP mnamo Agosti 1961 Jagan aliteuliwa tena kushika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa mara ya pili na alihudumu kwa miaka mitatu.
Baada ya hapo Jagan alisalia kuwa mwanaharakati na kiongozi wa upinzani nchini humo.
Jagan alizaliwa Port Mourant, Berbice, British Guiana (ambayo kwa sasa ni East Berbice-Corentyne, Guyana) Machi 22, 1918.
Alikuwa ni mtoto wa kwanza kati ya 11 kutoka kwa wazazi wafanyakazi wa Kihindu waliohamia Guyana wakitokea Uttar Pradesh nchini India. Wazazi waliingia katika taifa hilo wakiwa wadogo.
0 Comments:
Post a Comment