Thursday, March 5, 2020

Watanzania watakiwa kutumia bidhaa za ngozi za Tanzania


Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa, amewataka Watanzania kutumia bidhaa zinazotokana na ngozi zinazotengenezwa kwenye viwanda vya ndani ili kuongeza ajira kwa vijana.

Wito huo ulitolewa jana, wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Himo Tanners & Planters Ltd, ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Katika ziara hiyo Waziri Bashungwa  alishuhudia uwekezaji mkubwa  uliofanywa na mmiliki na mzawa Sabas Woiso wa uzalishaji wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa na malighafi zinazotokana na mifugo ya hapa nchini na kuwataka watanzania kutumia bidhaa hizo ili kukuza uchumi wa taifa.

Aidha  Waziri Bashungwa, alisema katika Bunge la bajeti, Serikali inalenga kuongeza kodi kwenye viatu vya mitumba, mikoba, mikanda na pochi zinazoingizwa hapa nchi ili kuvilinda viwanda vya ndani.

“Tutakapo leta kodi kwenye viatu vinavyo ingizwa kutoka nje ya nchi, yaani (mitumba), tunaomba Watanzania mtuelewe kwa sababu tukiendelea kuingiza mikanda, viatu, begi na mikoba ya Mitumba, maana yake ajira itaendelea kubakia nje ya nchi na sisi kama nchi tunataka kujenga uchumi wa viwanda ambao utaajiri vijana wetu wengi wanaohitimu kwenye vyuo,”alisema Waziri Bashungwa.

Vile vile Waziri huyo aliongeza kusema kuwa  “Nitakaa na Waziri wa Fedha na Mipango, kuangalia uwezekano wa shule zote hapa nchini kuanza kununua viatu vinavyotengenezwa hapa nchini, ili   kusaidia kuinua uchumi wa nchi.

“Kwa sasa tupo kwenye mazungumzo na Wizara ya elimu, mwanafunzi hataruhusiwa tena kuvaa viatu vya mitumba vinavyoingizwa hapa nchi na badala yake tutakwenda kuwataka wanafunzi wote kuanza kuvaa viatu ambavyo vinatengenezwa kwenye viwanda vyetu vya ndani,”alisema.

Aidha alitoa wito kwa wawekezaji wengine hapa nchini kujenga mazingira ya uwekezaji utakaolenga malighafi zinazopatikana hapa nchini ili wananchi waweze kunufaika na uchumi wa Taifa kukua huku akiupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuzingatia mpango wa 50-50 unaolenga kuajiri wafanyakazi kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia, mfano ambao alisema ni wa kuigwa na waajiri wengine.

Katika ziara hiyo mmiliki wa Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Himo Tanners & Planters LTD Sabas Waiso, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwaunga mkono na kuwajali katika kuhakikisha sera na  lengo la kufikia uchumi wa kati  nchini ifikapo 2025, kwani mpaka sasa kiwanda hicho kimeanza kunufaika na sera ya Tanzania ya viwanda.

Hata hivyo Woiso alitoa rai kwa Serikali kupitia mamlaka husika kuandaa mpango utakaotoa elimu kwa baadhi ya wafugaji kuachana na tabia ya kuweka alama kwenye mifugo yao maeneo ambayo yanaharibu ubora wa ngozi.

“Maeneo mengi tunapata ngozi ambazo ubora wake unakuwa si mzuri kutokana na mifugo kuwekewa alama maeneo yasiyofaa au ngozi kuchunwa vibaya, hili linapuguza idadi ya malighafi za ngozi tunazozitegemea, ingawa tunaipongeza mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu na Kagera imekuwa ikitoa  malighafi  za ngozi zenye ubora”, alisema.

Katika ziara hiyo  Waziri Bashungwa alipata fursa ya kutembele kiwanda cha kusindika ngozi cha Moshi Leather industries Ltd, kiwanda cha magunia Moshi na kiwanda cha Ngozi cha Karanga.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EMAIL: eliaskisena@gmail.com
DATE: Machi 4, 2020

0 Comments:

Post a Comment