Wednesday, March 25, 2020

Unaikumbuka siku Italia ilipoweka rekodi ya kuwa nchi mwenyeji Kombe la Dunia kufuzu?

Machi 25, 1934 Italia ilicheza mchezo wake wa kwanza wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia. 

Kinachostaajabisha katika mchezo huo katika historia ya Kombe la Dunia hadi sasa ni pale nchi mwenyeji ambaye ilikuwa ni Italia iliitandika Ugiriki kwa mabao 4-0 rekodi ambayo imekaa hadi sasa kwa nchi mwenyeji kucheza mchezo wake wa kwanza na kushinda idadi hiyo ya mabao. 

Nchi nyingi zimewahi kuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia lakini rekodi ya mchezo wa kwanza wa kufuzu haijawahi kwa idadi hiyo ya mabao. Italia ilicheza mchezo huo katika Uwanja wa San Siro jijini Milan mbele ya watazamaji 20,000. 

Kwa ufupi soka limepitia mabadiliko mengi kwani Kombe la Dunia la mwaka 1934 ilikuwa ni kwa mara ya kwanza nchi zote zilitakiwa kupambana kuwania kucheza fainali hizo.  

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA)ilizialika nchi wanachama kushindana  katika mashindano ya mwaka 1930 lakini ni nchi 13 pekee ziliitikia wito huo. Hatua hiyo ilisababisha mashindano hayo ya kwanza kusiwepo na hatua ya kufuzu. Kwa mwaka 1934 nchi wanachama 32 zilipeleka mwaliko wa kutaka kushiriki michuano hiyo.

FIFA ilikaa chini na kuangalia uwezo wa kusimamia ambapo timu 16 ndizo zilizotakiwa, hivyo makundi 12 yaliwekwa kwa nchi hizo kuwania kufuzu. Makundi yaliyo mengi yalikuwa na timu mbili au tatu na kundi moja lilikuwa na timu nne. 

Makundi yaligawanywa kwa kuangalia jiografia ya nchi husika ambapo Italia iliangukia katika kundi la tatu ambalo lilikuwa na Ugiriki. Machi 25, 1934 Italia ilikutana na Ugiriki jijini Milan na Azzuri walifanikiwa kumiliki mchezo huo mwanzo mwisho. 

Ugiriki waliwakamata waitaliano kwa dakika 40 za kwanza huku wakitengeneza nafasi chache za kufunga bila mafanikio. Katika dakika  ya mchezo Italia ilivunja kitasa cha Ugiriki kwa bao kupitia kwa nyota wake mwenye asili ya Brazil Anfilogeno Guarisi. 

Bao hilo liliwachanganya Ugiriki ambapo mafuriko ya mabao yalianza kuliandamana lango la Ugiriki kwani Giuseppe Meazza alifunga katika dakika ya 44 na 71 ya mchezo huo. Pia kiungo wa Azzuri Giovanni Ferrari aliifungia timu yake katika dakika ya 69 ya mchezo. 

Ugiriki ilivunjika moyo kwa kichapo hicho licha ya kwamba ilikuwa na mchezo wa pili jijini Athens lakini nafasi yake ilikuwa finyu ya kufuzu kucheza fainali hizo. Katika fainali hizo zilizochezwa nchini Italia, Azzuri ilisonga mbele katika mzunguko wa kwanza kwa kuizabua Marekani kwa mabao 7-1 ikiwa ni njia ya kulitwaa taji hilo.

Baada ya michuano hiyo ambayo Italia iliibuka bingwa mnamo mwaka 1936 FIFA ilikaa kitako na kuamua kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia atafuzu moja kwa moja bila kupitia mchujo, utaratibu ambao unatumika hadi sasa na ndio sababu ya kukueleza kuwa Italia ndio nchi mwenyeji pekee katika historia ya Kombe la Dunia kucheza mechi ya kuwania kufuzu.

0 Comments:

Post a Comment